Baadhi ya wakazi wa Majoe Gongolamboto, wakipita karibu ya moja ya mabaki ya bomu lililotua maeneo hayo wakati wa mlipuko uliotokea kwenye Kambi ya kuhifadhia Silaha ya Jeshi la Wananchi (JWTZ) 511 KJ iliyopo Gongolamboto Dar es Salaam jana usiku. Mabaki ya mabomu hayo yalisambaa katika mitaa mbalimbali ya Gongolamboto na Vitongoji vyake, ambapo imeelezwa kuwa baadhi ya mabaki ya mabomu hayo pia yaliokotwa mitaa ya Kimara, Mbagala na Kisarawe, katika mitaa ya majoe mabomu hayo yamebomoa nyumba kadhaa na kuharibu mali za wakazi wa maeneo hayo kiasi cha nyumba nyingine kubaki magofu.Mkazi wa Majoe, Rose Kayombo, akionyesha nyumba yake jinsi ilivyoharibiwa na bomu lililopiga nyumba hiyo na kusababisha moto mkubwa uliowaka na kuunguza kila kilichokuwamo ndani ya nyumba hiyo. Watu waliokuwamo katika nyumba hiyo wote waliweza kusalimika kwani baada ya kishindo cha bomu hiyo wote walifanikiwa kukimbia na kupoteana huku kila mmoja akienda na uelekeo wake.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Mohamed Gharib Bilal, akitembelea sehemu ya Ghala la kuhifadhia Silaha iliyoathirika kwa milipuko ya Mabomu jana jioni katika kambi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania Gongolamboto jijini Dar es salaam leo. wa pili kulia Mnadhimu Mkuu wa JWTZ Lt General Abrahamani Shimbo. Waziri wa Ulinzi, Hussein Mwinyi, akizungumza na viongozi wa Jeshi, wakati walipofika kutembelea katika Kambi hiyo leo mchana.Rais Jakaya Kikwete, akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutoka kukagua Ghala la kuhifadhia silaha la Kambi ya 511 KJ, lililopo Gongolamboto Dar es Salaam leo mchana. Kushoto ni Mkuu wa Majeshi, Jenerali Davis Mwamunyange (kulia) ni Mkuu wa Kambi hiyo, Kanal, Aloyce Mwanjile. Baadhi ya wakazi wa Gongolamboto, walioathirika ma mlipuko wa mabomu, wakiuchapa usingizi wakati wakiwa wamekusanyika kwenye Uwanja wa Uhuru kwa ajili ya kusubiri taratibu za kuweza kuwatambua ndugu zao waliopoteana.
Hapa si Kigoma, na hawa si Warundi waliokuwa wakihama nchi yao ya Burundi kuja nchini kupata hifadhi, bali ni wakazi wa Gongolamboto jijini Dar es Salaam, wakitembea kwa miguu kutoka maeneo mbalimbali yaliyoathirika na mabomu, kuelekea maeneo ya katikati ya mji ili kukwepa uwezekano wa mabomu hayo kuanza kulipuka upya baada kusikia matangazo eti kuwa huenda mabomu hayo yangeanza kulipuka tena mida ya saa saba mchana, jambo ambalo lilikanushwa na Rais Kikwete na viongozi wa Jeshi na kuwataka wananchi hao kurejea katika makazi yao jambo ambalo halikuwa rahisi kuwashawishi baada ya kujionea jinsi usiku ule ulivyokuwa mrefu na wa taabu, uliowafanya wanandugu kupoteana na wengine wakijikuta wanabeba viatu huku wakizani ni mtoto. Si kwamba wapo tayari kwa kuangalia mchezo wa soka uwanjani hapa, la hasha bali ni hifadhi ya muda waliyoipata wananchi hawa waathirika wa mabomu waliokesha katika taabu za kuhaha huku na huko kusalimisha maisha yao.
Hawa ni baadhi tu ya waandishi wa habari, wakiwa nje ya geti la kuingilia katika Kambi hiyo, kwa ajili ya kupata ukweli wa kuwataarifu wananchi, hapa ni baada ya kuzuiliwa kuingia na kuamua kumsubiri Rais, jambo ambali walifanikiwa kwani baada ya rais kuwasili kambini hapo waliweza kuruhusiwa wote kuingia ndani isipokuwa hawakuweza kuruhusiwa kufika eneo la tukio.
Baadhi ya mahema yaliyojengwa kwenye Uwanja wa Uhuru kwa ajili ya kutoa huduma ya kwanza.
Usafiri nao pia wa kutoka na kuingia Gongolamboto, ulikuwa ni wa tabu, hapa Daladala, likiwa limejaza abiria hadi nyuma ya Keria wakielekea maeneo ya Mjini kutoka Ukonga.Si mifugo pekee inayoweza kupakiwa katika magari haya, bali wakati ya shida kama huu hata binadamu huona ni jambo la kawaida sana kukwea katika usafiri kama huu tena kwa kugombea, haya ni baadhi ya magari yaliyokuwa yakitoa huduma ya kusafirisha wananchi kutoa Gongolamboto, lakini bado wananchi wa majoe walisikika wakilalamika kuwa "mbona wakati wa Kampeni walikuwa wakiona magari kibao ya viongozi yakifika katika maeneo yao, lakini wakati wa shida kama hii hayaonekani kufika kutoa huduma ya kuwasaidia kuwasafirisha", kwani wengi wao walikuwa wakitembea kwa miguu kutokana na kukosekana usafiri wa kwenda na kutoka maeneo hayo ya Majoe.
Wananchi wakishangaa mabaki ya mabomu....
Chuma hiki kilitua katika ukuta wa nyumba ya Bwana, Samuel Kitundu, iliyopo maeneo ya Majoe Kichangari.
Duka la vifaa vya ushonaji, likiwa limeteketea kwa moto maeneo ya Majoe Kichangari.
Baadhi ya wananchi wa Majoe, wakitembea kwa miguu kutoka katoka makazi yao kuelekea maeneo ya katikati ya mji.
Baadhi ya majeruhi wakiwa katika gari la wagonjwa wakihamishwa kutoka katika Hospitali ya Amana, kuelekea Hospitali ya Muhimbili baada ya kuzidiwa. hapa wakisaidiwa na ndugu zao waliowashikia chupa za Drip.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Brandina Nyoni, akiwajulia hali baadhi ya wagonjwa wanamama, waliolazwa kwenye Hospitali ya Amana.
Mtoto, Getrude Ikonko, akiwa amejilaza kwenye benchi baada ya kupatiwa matibabu kwenye hospitali ya Amana.
Baadhi ya wakazi wa maeneo ya Gongolamboto, wakitembea kwa miguu kuelekea maeneo ya katikati ya mji wakihama makazi yao baada ya kusikia uvumi kuwa huenda mabomu hayo yangeanza kulipuka upya leo mchana.
Hii ndiyo ilikuwa hadha ya usafiri kutoka na kuelekea maeoneo ya Gongolamboto leo asubuhi. Hapa wanaonekana wananchi wakigombea Pick Up hii ili kuweza kufika mahala wanapokusudia kufika.
Hili ndilo nyomi la wananchi waliokuwapo Uwanja wa Uhuru, wakisubiri kuwatambua ndugu na watoto wao waliopotea.
Hili ndilo nyomi la wananchi waliokuwapo Uwanja wa Uhuru, wakisubiri kuwatambua ndugu na watoto wao waliopotea.
Na Sufiani Mafoto.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)