SADAKA NA DHANA YA UTOAJI
(The concept of Giving and Offerings)
UTANGULIZI : MAANDIKO NA MISTARI YA KUSIMAMIA
Kumb 28: 1-14; “Itakuwa utakaposikia sauti ya Bwana, Mungu wako, kwa bidii, kutunza kuyafanya maagizo yake yote nikuagizayo leo, ndipo Bwana Mungu wako, atakapokutukuza juu ya mataifa yote ya dunia; na baraka hizi zote zitakujilia na kukupata, usikiapo sauti ya Bwana, Mungu wako. Utabarikiwa mjini, utabarikiwa na mashambani. Utabarikiwa uzao wa tumbo lako, na uzao wa nchi yako, na uzao wa wanyama wako wa mifugo, maongeo ya ng’ombe wako, na wadogo wa kondoo zako. Litabarikiwa kapu lako, na chombo chako cha kukandia unga. Utabarikiwa uingiapo, utabarikiwa utokapo. Bwana atawafanya adui zako wainukao juu yako, kupigwa mbele yako; watakutokea kwa njia moja, lakini watakimbia mbele yako kwa njia saba. Bwana ataiamuru baraka ije juu yako katika ghala zako, na mambo yote utakayotia mkono wako; naye atakubarikia katika nchi akupayo Bwana, Mungu wako. Bwana atakuweka uwe taifa takatifu kwake … na mataifa yote ya dunia watakuona umeitwa kwa jina la Bwana, nao watakuwa na hofu kwako. Bwana atakufanya uwe na wingi wa uheri, katika uzao wa tumbo lako … Bwana atakufunulia hazina yake nzuri … nawe utakopesha mataifa mengi, wala hutakopa wewe. Bwana atakufanya kuwa kichwa, wala si mkia; nawe utakuwa juu tu, wala huwi chini; utakaposikiza maagizo ya Bwana, Mungu wako ... kuyaangalia na kuyafanya; msipokengeuka … kwa lolote, kwenda mkono wa kuume wala kushoto…”
Kumb 8:10-20; “Nawe utakula ushibe, utamshukuru Bwana, Mungu wako, kwa nchi nzuri aliyokupa. Jihadhari usije ukamsahau Bwana, Mungu wako, kwa kutozishika amri zake, na hukumu zake, na sheria zake, ninazokuamuru leo. Angalia, utakapokuwa umekula na kushiba, na kujenga nyumba nzuri, na kukaa ndani yake; na makundi yako ya ng’ombe na kondoo yatakapoongezeka, na fedha yako na dhahabu yako itakapoongezeka, na kila kitu chako kitakapoongezeka; basi hapo moyo wako usiinuke, ukamsahau Bwana, Mungu wako, aliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa … Hapo usiseme moyoni mwako, nguvu zangu na uweza wa mkono wangu, ndio ulionipatia utajiri huo. Bali utamkumbuka Bwana, Mungu wako, maana ndiye akupaye nguvu za kupata utajiri; ili alifanye imara agano lake …”
SEHEMU YA KWANZA
KWANINI MUNGU ANATUPA UTAJIRI MALI NA FEDHA ?
1. ILI KUIMARISHA AGANO LAKE (UFALME WAKE)* Kumb 8:18 (12-18)
- Agano la Mungu kwa siku za leo, ni Agano JIPYA. Kuimarisha Agano lake maana yake; ni kuimarisha kazi ya injili ya Yesu Kristo, ili wokovu uwafikie watu wote.
- Gal 3:11,23-26,29; Rum 10:13 – 15; Fillip 4:15 –19
2. ILI KUVITUMIA KWA MAHITAJI YETU BINAFSI *Yoh16:24
Soma tena 1Timotheo 6:17 na 2Wakorintho 9:8 – 11
- Mungu kama Baba yetu na kama Mchungaji Mwema, anajali sana mahitaji yetu na haja zetu au shauku za mioyo yetu. (vitu vitupavyo furaha na kuridhika). Ndio maana hutupa utajiri, ili tufurahie maisha.
- Si mapenzi ya Mungu tuwe masikini. Ndio maana Yesu alifanyika maskini (kimwili) ili kwa umasikini wake, (sisi) tupate kuwa matajiri (kimwili)” 2 Kor 8:9
- Ni mapenzi ya Mungu tupate vitu vyote vitakavyotufanya tufurahie maisha yetu duniani. Nyumba nzuri, mavazi mazuri, chakula kizuri, kazi nzuri, magari mazuri, biashara nzuri, mifugo mizuri, mashamba mazuri, mshahara mzuri, n.k.
(Zab23:1- 2; Fil 4:6-7,19; Zab37:4; Zab145:17- 19)
3. ILI KUWAGAWIA WAHITAJI *2KOR 9:8-13;
Pia soma 1Timotheo 6:17-19; Waefeso 4:28 na Luka 6:38.
- Tunapowapa wahitaji fedha, nguo, viatu, chakula au vitu vya aina nyingine ili
kuwasaidia kimaisha, tunapata thawabu kubwa kwa Mungu. Kumsaidia mhitaji kitu, ni kumpa Mungu. Hebu soma vizuri Mathayo 25:31-40; Mathayo 10:40 – 42 na Yohana 13:20.
- Mungu ametupa mali, fedha na utajiri wa namna nyingi ili tuwasaidie wahitaji na masikini, wajane na yatima, wagonjwa na walemavu. Thawabu yake ni kubwa mbele za Mungu, na Mungu ataona sababu ya kukupa tena na kukuzidishia. Tena Mungu atakufanya uwe njia/mkondo wa baraka zake kwa watu wengine.
2Kor 8:14-15, Mdo 20:35
MAANA YA UTOAJI WA SADAKA
~ DHANA YA UTOAJI ~
Utoaji wa sadaka unasimama katika kweli zifuatazo;
1. KUTOA SADAKA NI NAMNA YA KUMHESHIMU MUNGU, KUMTAMBUA MUNGU NA KUMTHAMINI MUNGU KUWA NDIYE ATUPAYE UTAJIRI/VITU.
*Kumb 8:10 –20, Mith 3:9 – 10
“Mheshimu Bwana kwa mali yako, na kwa malimbuko ya mazao yako yote. Ndipo ghala zako zitakapojazwa kwa wingi, na mashinikizo yako yatafurika divai mpya”… Tena “hawatakuwepo masikini kwenu, kwakuwa Bwana atakubarikia kweli, katika nchi akupayo Bwana Mungu wako, uimiliki, iwe urithi wako.” Kumb 15:4. Mungu ndiye chanzo cha baraka zote tulizonazo. Sadaka ni ishara ya kumtambua na kumthanini kuwa yeye Mungu tunayemtolea sadaka, ndiye mpaji wa hizo mali na vitu vyote. Kwa ufahamu huu, tunatakiwa kumpa Mungu kile cha kwanza kabisa, tena kile kilicho bora zaidi. (“The first and the best”).
2. SADAKA NI NAMNA YA KUONYESHA SHUKURANI KWA MUNGU.
*Zab 116:18,12-13, Zab103:1-5, Zab 136:1-3
Sadaka ni namna ya kumshukuru Mungu kwa wema wake, fadhili zake na matendo yake makuu katika maisha yetu. Matendo ya Mungu kwetu ni mengi na makuu. Sadaka zetu ni njia tu ya kumshukuru, ni kiwakilishi cha shukurani zetu kwake, kwa maana hatuwezi kumlipa kwa mema anayotutendea *2Nyak 20:21 (1-30)
3. SADAKA NI NAMNA YA KUMUABUDU MUNGU
*Mwa 8:15-22; Ebr 7:1-3; Mwa 4:1-7
Utoaji ni heshima kwa anayepewa. Ndio maana washindi hutunukiwa zawadi/tuzo, kwasababu wanastahili. Vivyo hivyo kwa Mungu wetu; kwa kuwa yeye ni Mkuu, Mtakatifu, na Muweza wa yote, anastahili kuabudiwa. Hivyo sadaka zetu ni ishara ya kumtukuza, kumheshimu na kumuabudu Mungu.
4. UTOAJI WA SADAKA NI NAMNA YA KUONYESHA UPENDO
WAKO KWA MUNGU *Luk 7:36-48
Utoaji ni ishara ya Upendo. Unaweza kutoa bila kupenda, lakini huwezi kupenda bila kutoa. Utoaji mwingi, husukumwa na upendo mwingi. Upendo kidogo husababisha utoaji mdogo. Kwasababu ya upendo wa Mungu kwetu, alimtoa mwanaye.(Yoh 3:16; Rum 5:8). Kwasababu ya upendo wa Yesu kwetu, aliutoa uhai wake (Yoh 15:13.) Kwasababu ya kusamehewa dhambi nyingi sana, Yule kahaba akapenda sana, na ndio maana akatoa sana yaani nyingi/kubwa (Luk 7:36-48). Utoaji ni ishara ya Upendo.
Katika *Mith 8:17 Mungu anasema “Nawapenda wale wanipendao, nao wanitafutao kwa bidii, wataniona.” Je, unadhani Mungu anawatambuaje wale wanaompenda sana? Moja ya ishara ya wazi wazi ya upendo ni ‘utoaji’ (giving & offering). Upendo si kwa maneno tu, ni kwa matendo zaidi. Kama kweli unampenda Mungu, hauhitaji kutuambia, wenyewe tutaona jinsi unavyojishughulisha na mambo yake. Kumbuka kuwa matendo yetu yanaongea kuliko maneno yetu. Tunajua kuwa Mungu anawapenda watu wote (hata wenye dhambi pia) kama ilivyoanndikwa katika Yohana 3:16 na Warumi 5:8 kwamba Mungu alitupenda tungali wenye dhambi.
Lakini kwa kusoma Mithali 8:17 inayosema “nawapenda wale wanipendao…” tunagundua Mungu anawapenda watu fulani zaidi kwa upendo mwingine tofauti na ule wa watu wote (Yoh 3:16). Hii ni ngazi nyingine kabisa ya upendo. Ni ngazi ya juu zaidi au class ya juu zaidi. Ni upendo wa ‘kirafiki’. Kupewa upendo wa ngazi ya juu, upendo wa kirafiki, ni lazima nawe ufanye kitu cha ziada kwa Mungu. Hivyo ukimpenda Mungu kwa upendo wa ziada, naye atakuonyesha upendo wa ziada, tofauti na ule wa kijumla anaowapenda nao watu wote (Yoh 3:16 na Rum 5:8). Atakupenda kipekee, upendo wa kirafiki, kwasababu Mungu anawapenda wale wamendao.
5. UTOAJI WA SADAKA NI USHIRIKA WETU KATIKA KAZI YA MUNGU.
* Malaki 3:7-12; Rum 10:13-15;* Hagai 1:3-11
Mungu ametupa mali na utajiri, ili tushiriki katika ujenzi wa ufalme wake duniani Mungu anatutaka tutoe sadaka nzuri “Ili kiwemo chakula nyumbani mwa Mungu” (Kanisani / Huduma ya Injili) Kama kweli unampenda Mungu, hauhitaji kutuambia, wenyewe tutaona jinsi unavyojishughulisha na mambo yake. Matendo yanaongea kuliko maneno.
Moja ya sabau kwanini Mungu amepitisha utajiri na fedha katika mikono yetu ni ili kuimarisha agano lake (ufalme wake) * Kumb 8:18 (12-18). Agano la Mungu kwa siku za leo, ni Agano JIPYA. Kuimarisha Agano lake maana yake; ni kuimarisha kazi ya injili ya Yesu Kristo, ili wokovu uwafikie watu wote. (Rum 10:13 – 15). Nyumba ya Mungu na kazi ya Mungu isipopungukiwa na kitu, injili itasonga mbele kwa kasi na kwa urahisi zaidi. Ndio maana Mungu ametupatia pesa, utajiri na mali. (2Kor 8:1-15)
6. UTOAJI WA SADAKA NI UPANDAJI WA MBEGU ILI KUPOKEA (KUVUNA) BARAKA NA UTAJIRI MWINGI ZAIDI
* 2Kor 9:6, 2Kor 9:8,Gal 6:7 – 10, Malaki 3:10 – 12, Luk 6:38,
Mtoaji wa sadaka ni kama mpanzi wa mbegu shambani. Mbegu moja huzaa nyingi zaidi kuliko ile iliyapandwa. Tunapotoa sadaka, tunatakiwa kutoa huku tukitarajia kupokea vingi kulilo tulivyotoa. Atakaye mavuno mengi ni lazima:-
i. Achague(atenge) mbegu bora zaidi (the best)
ii. Afuate masharti ya upandaji (Kilimo)(Isa 1:19)
iii. Apande mbegu nyingi (2kor 9:8)
Kwa kutokufuata maagizo na kanuni za Mungu katika utoaji wa sadaka, wengi hawavuni kama vile ahadi za Mungu zilivyo. Matokeo yake, hukata tama kutarajia baraka katika sadaka watoazo. Ndipo huanza kutoa kidogo kidogo sana kuepuka hasara. Lakini kama mpanzi alipanda kwa kufuata kanuni sahihi za kilimo, siku zote mavuno yake huwa mengi zaidi kuliko mbegu alizopanda. Vivyo hivyo, kila atoae matoleo (sadaka) vizuri, kwa kufuata maagizo na kanuni za Mungu, hupokea kwa wingi zaidi ya vile alivyotoa. Kila apandaye vizuri, huvuna vizuri.
Utoaji ni njia ya Mungu kutupa na kutujaza tunavyohitaji *1Fal 17:1-16. Mungu ndiye alieyewaka kanuni ya kupanda na kuvuna, kutoa na kupokea. Hivyo, mara nyingi tunapomwomba Mungu atubariki/atujaze mahitaji yetu, anatuletea mafasi ya kutoa kwanza, ili tupokee mahitaji yetu tumwombayo. Kwasababu, ndiyo kanuni ya kupokea. Ni ajabu, sicho tunachotegemea (kutoa wakati wewe binafsi unahitaji). Badala ya Mungu kukupa moja kwa moja kitu ulichomwomba, anakuletea nafsi ya kutoa hicho hicho kidogo ulichonacho, kiwe kama mbegu, ili hatimaye upokee (uvune) kile ulichomwomba, na hata zaidi ya ulivyoomba.
Biblia pia inasema hivi katika Waefeso 3:20 na Wafilipi 4:15-19; kwamba, “Basi atakuzwe Mungu awezaye kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yote tumwombaye au kuliko yote tuyawazayo, kwa kadri ya nguvu, itendayo kazi ndani yetu” (Efe 3:20; Fil 4:15-19).
1Wafalme 17:13-16; Eliya akamwambia (yule mama mjane); usiogope (kutoa hicho kidogo kilichobaki) … enenda ukafanye kwa ajili yangu (kwa maana ukinipa mimi, utakuwa umempa Mungu) na Mungu wa Isarael anasema, unga wako wala mafuta yako hayatapunguka kamwe, mpaka njaa itakapoondoka juu ya nchi. Yaani Mungu atavizidisha. Si ajabu anliongezea Kama ukikubali na kutii, utakula mema ya nchi. Lakini ukikataa, utaangamia (kama wengine wanavyoangamia). (Isa 1:19)
Si jambo rahisi kutoa wakati wewe mwenyewe umepumgukiwa au una uhitaji. Inahitajika imani kubwa kutoa kidogo kilichobaki, ili uhitai wako ujazwe. Hivyo, usishangae siku utakapomwomba Mungu pesa au vitu, halafu badala ya kukupa, anakuletea mhitaji ili umpe pesa au vitu, au analeta nafasi ya wewe kutoa sadaka. Kumbuka kanuni yake, huwezi kuvuna bila kupanda! Hivyo, ukikubali na kutii, utavuna na kupata mema, tena zaidi ya ulivyotarajia. Hii ni kanuni ya Mungu; ukipanda haba utavuna haba, ukipanda nyingi, utavuna nyingi. Huwezi kuvuna bila kupanda
*Malaki 3:10–12, Fil 4:10 – 20, 1Kor 4: 1-2, Mdo 20:35, Luk 6:38
7. UTOAJI WA SADAKA NI KUWEKA AKIBA MBINGUNI
*Luk 12:30-34; Math 6:19-20.
Imeandikwa kwamba “Hazina yako ilipo, ndipo moyo wako utakapokuwepo” Je ulishajiouliza? Hivi, akiba yako au hazina yako huko mbinguni ina kazi gani? Au inafanya nini? Mambo yafuatayo, ni baadhi tu ya kazi za hazina yako iliyoko mbinguni.
(i) Kutusaidia wakati wa uhitaji
“basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji” Ebr 4:16
Mtume Paulo alisema ninajua kupungukiwa na ninajua kuwa na vingi. Katika mambo yote nimefundishwa kushiba na kuona njaa (Wafilipi 3:12.) Katika maisha kuna vipindi vya kupungukiwa na kuna vipindi vya kujazwa. Katika nyakati zote tunayaweza yote kwa yeye Yesu anayetutia nguvu.
Huwa kuna neena maalum kutoka kwa Mungu, inayoachiliwa ili kutuvusha katika vipindi vigumu maishani mwetu, vipindi vya uhitaji. Sikia Neno linavyosema; “basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji” (Waebrania 4:16). Ni hii neema iliyomfanya Mtume Paulo kusema nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu (Wafilipi 4:13).
Ni kanuni ya Mungu kwamba, huwezi kuvuna bila kupanda. Hivyo, wakati wa uhitaji ukikufikia, Mungu atakutaka utoe kitu ili upokee mahitaji yako. Watu wengi wanashangaa kwamba, wakati wamepungukiwa, ule wakati wa uhitaji wao, ndio Mungu anaruhusu nafasi ya kutoa ije. Na wengi wanakosa baraka na msaada wa Mungu kwasababu hawaelewi utendaji wa kanuni za Mungu. Maana katika uhitaji wao, wamemwomba Mungu awajaze.
Lakini kitu cha kushangaza kabisa ni kwamba, badala ya kupokea, wanajikuta katika mazingira ambayo wanaombwa au wanatakiwa watoe kitu.
Wengi hawajuai kuwa nyakati hizo, ni Mungu aliyeleta nafasi hiyo ya kutoa hicho kidogo kilichobaki ili kanuni yake ifanye kazi na upako wa Mungu uingie kazini kuwaletea mavuno kwa kadri ya utii wao katika utoaji. Ukitii utakula mema ya nchi. Kumbuka kilichompata yule mama wa Sarepta katika 1Fal 17:8-16.
Hivyo, wakati wa uhitaji ukikufikia, Mungu atakutaka utoe kitu ili upokee mahitaji yako. Lakini, utafanyaje wakati umepatwa na mahitaji ya lazima (emergency) na nafasi ya utoaji imekuijia ili uote kitu, na hatimaye Bwana akufungulie madirisha ya mbinguni kukupa ulichokuwa unamwomba Mungu, lakini huna cha kutoa? Hapo ndipo ile akiba yako mbinguni inaingia kazini. Moyoni mwako Roho atakukumbusha kuwa umaweza kuomba neema maalum ya kutusaidia wakati wa mahitaji.
Kama una hahika na maisha yako ya utoaji wa sadaka katika kazi mbalimbali za Mungu hapa duniani, utajikuta unapewa au anapata ujasiri wa kumwendea Mungu katika kiti chake cha rehema, ili akupe neema ya kukusaidia wakati wa uhitaji kwasababu una hazina/akiba kule mbinguni. Kipindi unachotakiwa kutoa ili kuikamilisha kanuni ya Mungu ya kupanda na kuvuna, lakini una cha kutoa, hazina yako mbinguni inakupa ujasiri wa kuomba neema ya kukuvusha katika kipindi hicho kigumu cha ukata. Lakini kama hazina yako mbinguni iko tupu, then huwezi kupata ujasiri ndani yako, kwasabu unajua kabisa kuwa, akaunti yako mbinguni iko tupu.
Huwezi kuwa na uhakika wa msaada wa Mungu. Unaweza ukajikuta unateseka sana katika kipindi cha uhitaji.
Ila kwa mtu mtoaji mzuri wa sadaka, siku akiishiwa , ana ujasiri wa kwenda mbele za Mungu kuomba neema ya kumvusha wakati wa mahitaji yake na hakika atapata msaada wa Mungu. Mungu alisha sema katika Neno lake kwamba, vile tunavyo mfanyia yeye kuhusu kazi yake, naye atatufanyia sisi vivyo hivyo katika kazi zetu. Japo kuwa alikuwa anaongea na taifa takatifu la watu aliowaahidi baraka nyingi (kama sisi kanisa) alisema nao katika Malaki hivi...... Malaki 3:7-12; (Hebu tuisome mistari hii kwa utaratibu huu; tuanzie mstari wa 9)
9Ninyi mmelaaniwa kwa laana! Naam, taifa hili lote (kwasababu) 8naniibia mimi. Lakini mnasema tumekuibia kwa namna gain? Mmeniibia zaka na dhabihu (sadaka). 10Leteni zaka kamili ghalani…nami nitawafungulia madirisha ya Mbinguni na kuwamwagieni baraka hata isiwepo nafasi ya kutosha. 12Na mataifa yote watawaiteni heri, maana mtakuwa nchi yenye kupendeza sana, asema Bwana wa majeshi. (lakini) ikiwa baada ya yote hayo hamtaki kunisikiliza, bali mwaendelea kunishika kinyume, ndipo nami nitakwnda kwa kuwashika nanyi kinyume katika ghadhabu yangu; nami nitawaadhibu mara saba katika dhambi zenu. (Walawi 26:27-28). Kwahiyo, kama tunataka msaada wa Mungu katika mahitaji yetu, ni muhimu sana tuwe waaminifu pia na watoaji wazuri wa sadaka zetu, ili zile siku za kudhiliwa zikija, zitukute tuna neema ya kutusaidia katika siku hizo. Wakati tunapokuwa wa fedha za kutosha, watu wengi hawawi na moyo wa kupenda kutoa sadaka nyingi.
Wengine wanaona kutoa ni kupoteza. Na wako tayari kuchanga fedha nyingi katika maharusi na masherehe kwa wingi kuliko kutoa sadka katika kazi ya Mungu. Huko ni kutolijua Nemo la Mungu au ni kuto kumwamini Mungu. Hebu tubadili fikra zetu katika utoaji. Kutoa si kupoteza. Wala kutoa si kuchangia. Kutoa ni kuwekeza. Kutoa ni kweka akiba au hazina mbinguni. Neno la Mungu ni hakika. Na Mungu ni mwaminifu sana hasa kwa wale watu wanaomcha yeye na kuyashika maagizo yake. “Mungu Mkuu, mwenye kutisha, ashikaye maagano na rehema kwao wampendao, na kushika amri zake.”( Daniel 9:4)
(ii) Kutuandalia makao mazuri mbinguni (Yohana 14:1-2)
Yesu akasema “…nakwenda kuwaandalia mahali …” Mimi naamini kwamba, tutakapofika mbinguni, tutakuta majumba makubwa ya kifahari, yenye kuta na vitasa vya dhahabu, yameandaliwa kwa ajili yetu. (Ufu 21:1-4, 18,22) Lakini “binafsi” nina wasiwasi kuwa wengi wasiopenda kutoa sadaka nzuri hapa duniani, wakifika mbinguni, si ajabu watakuta hazina zao huko juu, ni ndogo sana, kiasi ambacho hakikutosha kuwezesha watengenezewe makao yao, yenye ubora na uzuri kama wa wengine walioweka “hazina kubwa” kwa utoaji wao wa hapa duniani. Tafakari: Math 20 : 21 – 23 vizuri. Utagundua kwamba, mbinguni kuna utaratibu wa kupangwa viti vya kukalia katika mahali ambapo tutakuwa na Bwana Yesu. Labda ni katika ukumbi wa ibada au pengine ni katika ukumbi wa sherehe/karamu ya Mwanakondoo.
Tafakari yangu mimi iko hivi; kama kuna watu watakaokaa karibu na Yesu, basi hii ina maana kwamba, pia wapo watu ambao watakaokaa mbali na Yesu. Ni wazi kwamba hayo ni madaraja (classes) tofauti, japo sote tuko mbinguni.
Hebu soma vizuri 1Kor 3:10-15. Kwasababu kazi zingine zitakuwa na ubora wa dhahabu, zingine chuma, udongo, miti na manyasi, haiwezekani hawa wote wakawa katika msatari mmoja. Mimi naamnini, atakaye mletea Bwana mavuno au talanta ya ubora wa dhahabu atalipwa thawabu kubwa zaidi kuliko mtumishi atakayemletea Bwana mavuno ya ubora wa shaba Na huyu wa shaba atalipwa zaidi kuliko yule wa udongo.
Hivyo basi, ukaribu wa kiti chako na Yesu kule mbinguni, unategemeana sana ubora wa kazi yako na utumishi wako (utendaji wako) wa kazi ya Bwana hapa duniani. Ubora wa kazi ya mtu ndio utakao mpa nafasi nzuri na tuzo nzuri zaidi mbinguni. Pia wapo watakaokosa kabisa tuzo, ni wale ambao kazi zao zilikuwa za ubora wa miti au manyasi, kwa maana kazi zote zitajaribiwa kwa moto, kazi ya mtu ikitoka katika moto, huyo mtu atapata thawabu/tuzo; lakini kazi ya mtu ikiteketea, mtu huyo atapata hasara, kwasababu hawakufanya kazi ya Mungu vizuri walipokuwa duniani, japo yeye mwenyewe ataokolewa na moto.
Kwahiyo, katika ile siku ya hukumu, moto wa Mungu utaijaribu kila kazi ya kila mtu kuona ipo katika ubora wa aina gani. Kama Mungu anashauku ya kufanya zaezi hilo, hivi unadhani anatafuta nini? Kama Mungu hajali ubora au madaraja ya kazi za watu, hili zoezi la upimaji kwa moto, ni la nini basi?
Ooh! Ni wazi kwamba; Mungu anajali sana ubora wa kazi zetu. Na ndio kusema anajali sana (yuko interested) na madaraja ya watenda kazi wake (classes). Ndugu yangu, usifanye mchezo. Ni waza na hakika ya kwamba kazi zetu zitapimwa na ni lazima kwamba, kazi zetu zitatofautiana. Hii ni inamaanisha kwamba, hata tuzo zetu na thawabu zetu hazitafanana. Zitatofautiana. Kuna wengine watakuwa na taji zinazong’aa sana kuliko wemgine. Kuna wengine, viti vyao vitawekwa wakae karibu sana na Yesu kuliko wengine.
Kama Yohana aliuona ule mji mtakatifu una upana una urefu wa maili 1500, (Yaani ki kama kutoka Cairo ya Misri, mpaka Johanersburg ya Afrika Kusini) Soma Ufu 21:10-16 utaona mwenyewe. Duh! Kwa lugha na mtazamo wa kibinadamu, ina maana kuna watu viti vyao vitawekwa umbali ambao hawataweza hata kumwaona Yesu mezani kwake (kama ni ibadani au ni chakulani). Labda kwasababu si duniani bali ni mbinguni, inawezekana kutakuwa na mwanda wa tofauti. Sina uhakika. Wewe je? Well, kwa ufupi, Hiki ndicho kinachonifanya niamini kwamba, si ajabu huko mbinguni kukawa na madaraja (classes) tofauti (nionavyo mimi). Basi, si ajabu pia, hata ubora wa nyumba zetu mbinguni zita tofautiana, kulingana na madaraja hayo. Inawezekana kabisa ubora wa nyumba zatu ukatofautiana katokana na utofauti wa “utoaji wetu” hapa duniani na “hazina zetu” mbinguni.(Nionavyo mimi). Basi nikupe tu ushauri binafsi; Angalia usije ukafika mbinguni, katika jumba la kifahari, lenye kuta na vitasa vya dhahabu, lakini kwa aibu, ukakalia stuli milele. Weka hazina yako mbinguni, kwa utoaji mzuri wa sadaka zako. Inalipa! Sadaka zako hazipotei, bali zinawekwa kama ‘akiba’ mbinguni.
“Msijiwekwee hazina duniani, nondo na kutu viharibipo, na wezi huvunja na kuiba; bali jiwekeeni hazina mbinguni, kusiko haribika kitu kwa nondo wala kutu, wala wezi hawavunji wala hawaibi; kwakuwa hazina yako ilipo, ndipoutakuwapo na moyo wako.” (Mathayo 6:19-21)
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)