Makamu Mkuu Shule ya Sekondari Kivesa, Faustine Mrosso, shule hiyo
iliyopo Kata ya Chanika inahudumia vijiji vya Kwediyamba, Kwedizando na
Kwekambara maeneo ambayo ni mbali na shule hiyo
Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Kata ya Komnyang'anyo
wakitembea barabarani kuelekea kwenye makazi yao vijiji mbalimbali
vinavyoizunguka shule hiyo.
Na Joachim Mushi, Thehabari.com- Handeni
WANANCHI wilayani Handeni wameilalamikia mazingira magumu
kimiundombinu ya shule za sekondari za kata katika wilaya hilo na kudai ndiyo chanzo cha kuongezeka kwa
mimba kwa wanafunzi na kukatisha masomo. Kauli hiyo imetolewa kwa nyakati tofauti katika mahojiano ya
baadhi ya wakazi wa Handeni na mwandishi wa habari hizi ndani ya uchunguzi
uliofanywa hivi karibuni maeneo anuai ya wilaya hiyo kwa ushirikiano na Chama
cha Wanahabari Wanawake (TAMWA).
Abdulah Mwamponda Mkazi wa Kijiji cha Msasa, wilayani
Handeni alisema shule nyingi za kata zimejengwa mbali na makazi ya wanafunzi
jambo ambalo linawapa mzigo wazazi na wanafunzi kujitafutia usafiri wa kwenda
na kurudi shuleni. Alisema katika kijiji hicho wapo wanafunzi ambao hutembea
umbali wa kilometa 12 na hata 20 kila siku kuanzia Jumatatu hadi Ijumaa kwenda
na kurudi shuleni, umbali ambao umekuwa na vishawishi vingi hasa kwa wanafunzi
wa kike kiusafiri.
Alisema usafiri katika vijiji hivyo ni wa baiskeli na
pikipiki (bodaboda) ambao wazazi wengi wanashindwa kugharamia hivyo watoto
kutembea kwa umbali huo, huku wakati mwingine wakishawishika kupewa msaada wa
lifti na madereva wa bodaboda ambao baadaye huanza kushirikiana nao kimapenzi.
Mzazi Fatuma Shaban kutoka Kijiji cha Komnyang’anyo alisema
wanafunzi wengi huondoka nyumbani kwao saa 10 za asubuhi na kurudi usiku
kutokana na umbali huo huku wengine wakishinda shuleni bila chochote kutokana
na uduni wa maisha ya kaya nyingi eneo hilo.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Kilimani, Rajab Nyange alisema
katika shule hiyo iliyopo Kata ya Vibaoni nje kidogo ya Mji wa Handeni wapo wanafunzi
wanaotoka vijiji vya mbali takribani kilimeta sita hadi 10 kutoka nyumbani
kwao, ambao hutembea kilomita 20 kila siku yaani kwenda na kurudi shuleni jambo
ambalo linaibua vishawishi kwa wanafunzi.
“Mzazi anashindwa
hata kumpa mtoto wake sh. 100 au 200 kila siku ya shule kwa ajili ya kula
chochote awapo shuleni, je ataweza kumlipia mtoto huyo gharama za usafiri
ambazo ni za juu zaidi kutokana na umbali kutoka kijiji kimoja hadi kingine,” alihoji
Nyange. Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Hassan
Mwachibuzi anasema Ofisi yake haina taarifa za ubakaji wa moja kwa moja
japokuwa anakiri kuwepo kwa vitendo vya utoro kwa wanafunzi wote kwa sababu
mbalimbali. Anasema pamoja na hayo
utoro waweza kuingiliana na ukatishwaji masomo kwa mimba.
Kiongozi huyu
anakiri suala la umbali wa shule huchangia vishawishi kadhaa vya wanafunzi hasa
wa kike kukumbwa na vikwazo kadhaa katika masomo yao. Hata hivyo anabainisha
kuwa uongozi unajitahidi kulitatua suala hilo kwa kuongeza ujenzi wa hosteli
kwa wanafunzi katika shule za kata ili wanafunzi waondokane na vikwavyo anuai.
Aliongeza kuwa tayari
wamejenga hosteli katika maeneo ya Kisasa, Kwamsisi, Misima, na kudai kuwa wanaendelea
maeneo mengine kwa kushirikiana na wananchi na wahisani huku lengo ni
kuhakikisha kila kata inakuwa na hosteli zake kwa ajili ya wanafunzi wanaotoka
maeneo ya mbali na shule.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)