TAARIFA :Mwenge wa Uhuru Ulifikishwa Katika Kilele Cha Mlima Kilimanjaro kama ilivyoagizwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete tarehe 1 Desemba, 2011 - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

TAARIFA :Mwenge wa Uhuru Ulifikishwa Katika Kilele Cha Mlima Kilimanjaro kama ilivyoagizwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete tarehe 1 Desemba, 2011

Ndugu wananchi, Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, inachukua fursa hii kukanusha taarifa zinazoendelea kuchapishwa na gazeti la Dira ya Mtanzania kama zilivyotolewa kwenye gazeti lao toleo Na. 145 la Jumatatu Januari 2 – 4, 2012 na gazeti toleo Na. 146 la Alhamisi Januari 5 -8, 2012.

Katika matoleo hayo yote, Gazeti hili linadai kuwa, Mwenge wa Uhuru haukufikishwa kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro na kwamba Serikali imewadanganya wananchi.
Ukweli ni kwamba, Mwenge wa Uhuru ulifikishwa katika kilele cha Mlima Kilimanjaro kama ilivyoagizwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete tarehe 1 Desemba, 2011 wakati akiwakabidhi Mwenge huo wapandishaji wa Mwenge kileleni Kilimanjaro.

Ni vema wananchi mkapuuza taarifa hizi za uzushi zinazoendelea kutolewa na Gazeti hili kwa sababu hazina ukweli wowote kama inavyodaiwa. Wahariri wa Gazeti hilo wameshindwa kuthibitisha madai yao mbali na kung’ang’ania kusisitiza kuwa Mwenge huo haukufikishwa kileleni.

Gazeti hilo pia linadai kuwa, kulikuwa na kutoelewana kati ya wajumbe walioteuliwa kupandisha Mwenge huo kileleni Kilimanjaro. Habari ambazo si za kweli. Ukweli ni kwamba wajumbe hao walishirikiana kikamilifu kati yao na wasaidizi waliopangiwa kusindikiza msafara huo wa Mwenge kwenda kileleni.

Aidha, Mhariri alikuwa na fursa ya kuwahoji wajumbe wateule wa msafara huo lakini hakufanya hivyo na badala yake amekuwa akidai kuwa na vithibitisho kutoka kwa vyanzo mbalimbali na si kutoka kwa wale waliopandisha Mwenge.

Serikali inawakumbusha Wamiliki wa vyombo vya habari, Wahariri na Waandishi wa Habari kuwapasha wananchi habari za kweli na zilizofanyiwa utafiti wa kina.
Aidha Serikali inaviheshimu vyombo vya habari vinavyozingatia weledi katika kuwapasha habari za kweli wantanzania.

Kwa mara nyingine, Serikali inawahakikishia wananchi kuwa, Mwenge wa Uhuru ulifikishwa kileleni Kilimanjaro na hakuna utata wowote katika suala hilo.
 
Raphael Hokororo
KAIMU MKURUGENZI
IDARA YA HABARI – MAELEZO
TAREHE 05/01/2012

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages