Ndugu zangu,
Nimetafakari sana na kujiuliza; kwanini hata katika miaka 50 ya uhuru wetu hatujaweza kubadilisha hata ladha ya ugali tunaokula?
Ndio, miaka 50 ya Uhuru na ugali ni ule ule. Hatujaongeza ubora wa
ugali wala wingi wake kwenye sahani. Kama jana kama leo, tunachemsha
maji, tunaweka unga na kisha tunasonga. Ni vile vile, tunasonga ugali kwa mazoea. Hivi, hatuwezi kuukamulia ndimu au limau ugali tunaousonga?
Ni swali linalokutaka ufikiri kwa bidii. Maana, kama tunaweza kunywa uji
wa ndimu au limau kwanini tusiweze kula ugali wa ndimu au limau? Naam,
ndimu inaweza kuchangamsha ugali tunaokula.
Na kama tunaweza kunywa uji wa chenga kwanini tusianze kusonga ugali wa
chenga? Na ugali wa chenga ukikamuliwa ndimu au limau unaweza kuwa mtamu
haswa.
Ndugu zangu,
Tunahitaji mabadiliko.
Tumekuwa
ni watu wa kuogopa mabadiliko. Ni watu tulioridhika na ugali ule ule,
miaka nenda miaka rudi. Kwanini? Tumekuwa kama watu wa Taifa la
Kusadikika. Maana, mwandishi yule mahiri, Mtanzania mwenzetu Shaaban
Robert anaandika; ” Wasadikika wana desturi ya kutafuta fimbo baada ya
kuumwa na nyoka. Tumekwisha umwa na nyoka wa matendo yetu mabaya ya zamani.
Nyoka mwenyewe amekwishakimbia. Hapatikani kwa kujilipiza kisasi, lakini, sumu yake imebakia katika jeraha tulilolipata. Sasa, shauri lililo jema ni kuzuia sumu hii isienee miilini mwetu ikaleta kifo.
Maovu
yana hatari kubwa kukaa kati yetu. Tumedumu nayo kwa muda mrefu.
Hayakutuletea faida ila hasara, huzuni na kilio siku zote.”- Shaaban Bin
Robert. Naam, na Shaaaban Robert naye alitutaka tubadilike, miaka 50 iliyopita!
Maggid Mjengwa,
Iringa
Januari 9, 2012
http://mjengwa.blogspot.com
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)