ASKOFU MABUZA AMSHAURI MFALME MSWATI III KUACHIA MADARAKA YA KISIASA - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

ASKOFU MABUZA AMSHAURI MFALME MSWATI III KUACHIA MADARAKA YA KISIASA

         Mfalme Mswati III

Askofu Meshack Mabuza, ambae ni Kiongozi mwandamizi wa Kianglikana wa Swaziland, amemtaka Mfalme Mswati III kuachia madaraka ya kisiasa ili kutoa nafasi Serikali ya kidemokrasia nchini humo.

Askofu Mabuza ameiambia BBC mfumo wa Serikali wa “mambo ya kale” unaofuatwa sasa umeiingiza nchi katika mgogoro mzito wa fedha na uchumi.

Taarifa zinasema Serikali imekiri kuwa mishahara ya wafanyakazi wa Serikali itacheleweshwa mwezi huu kutokana na upungufu wa fedha. Mfalme Mswati, mwenye wake 13, ni kiongozi pekee ambaye hushilikia mamlaka yote Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Kiongozi huyo amekuwa akishutumiwa kwa kiasi kikubwa kuhusishwa na ufisadi, lakini akaahirisha sherehe zake za kufikisha miaka 25 madarakani mwaka huu kutokana na msukosuko wa fedha nchini humo.Mpaka sasa Swaziland imekataa kupokea mkopo wa dola za kimarekani milioni 355 kutoka Afrika kusini kuisaidia kulipa gharama mbalimbali, baada ya Pretoria kuitaka nchi hiyo kufanya mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi.
         Askofu Meshack Mabuza wa pili kulia
 
‘Visababu’Askofu Mabuza, askofu wa Kianglikana wa Swaziland, aliiambia BBC kuwa matatizo ya Swaziland hayatokwisha iwapo uongozi huo utaendelea kuwepo madarakani. Alisema, “Jawabu kwa hakika litatokana na mabadiliko ya uongozi wa serikali ya kiutamaduni, kikabaila, na mambo ya kale.” “Lazima ibadilishwe na uongozi wa kidemokrasia wa vyama vingi.”

Taarifa ya serikali iliyoonekana kabla ya kutolewa rasmi- iliyotiwa saini na mhasibu anayekaimu, AF Mabila- ilisema malipo ya mishahara ya wafanyakazi wa serikali ya Novemba imesogezwa hadi Desemba. Msemaji wa serikali Percy Simelane aliiambia BBC baraza la mawaziri limekuwa likijadili suala hilo tangu Jumamosi, lakini mpaka sasa hamna muafaka wowote uliofikiwa.

Serikali imesema mgogoro wake wa fedha umesababishwa na msukosuko wa uchumi duniani na kuporomoka kwa mapato ya uongozi huo kutoka umoja wa ushuru wa forodha wa kusini mwa Afrika (sacu), kufuatia makubaliano mapya ya ushuru wa forodha mwingi. Lakini askofu Mabuza, anayetarajiwa kuachia madaraka mwezi ujao, alisema hivyo ni “visababu”.
         Baadhi ya wake wa Mfalme Mswati wa III
 
Alisema, ” Matatizo ya kiuchumi yalikuwepo hata kabla ya kuporomoka kwa uchumi wa dunia kwasababu imekuwa kama hakuna ukuaji wa kiuchumi.” “Nchi hii imefika hatua ya kuporomoka kabisa.” Kumekuwa pia na wasiwasi kuwa hospitali za taifa zinaweza kuishiwa na dawa za kufubaza ukimwi ARVs kutokana na upungufu wa fedha. Swaziland, yenye jumla ya watu milioni 1.2, ni miongoni mwa nchi zenye idadi kubwa ya walioathirika na ukimwi duniani.

Takriban watu 230,000 wanaishi na virusi vya ukimwi, ambapo 65,000 wanategemea hospitali za taifa kuwapa dawa hizo za ARV. Vyama vya kisiasa vinazuiwa Swaziland, ambapo Mfalme Mswati amekuwa madarakani tangu mwaka 1986. Wakosoaji wanaishutumu familia hiyo ya kifalme kwa kuwa na matumizi makubwa kupita kiasi, licha ya idadi kubwa ya watu wake wakiishi maisha ya kimaskini.

Msukosuko wa kiuchumi umechochea maandamano dhidi ya uongozi wa mfalme Mswati, lakini wachambuzi wamesema ufalme huo bado unapewa heshima kubwa na Waswaziliand wengi wanaothamini mila na desturi zao.
Baadhi ya wanawake Bikra wa Kiswazland wakiwa kwenye sherehe za jadi kwa ajili ya Mflame Mswati kuchagua mke mwingine wa kuoa!

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages