Philemon Luhanjo
Yaliyomo
kwenye ripoti ya ukaguzi wa tuhuma zinazomkabili Katibu Mkuu Wizara ya
Nishati na Madini aliyesimamishwa kazi, David Jairo, hadi sasa
hayajulikani, kutokana na Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi, kushindwa
kuweka ripoti hiyo hadharani.
Ukaguzi
wa tuhuma hizo, ambazo Jairo anadaiwa kuchangisha fedha ili
kuwashawishi wabunge kupitisha bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha
wa 2011/2012, ulifanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali (CAG) kwa siku kumi mfululizo.
Ukaguzi huo kwa mujibu wa aliyekuwa Kaimu CAG, Jumaa Mshihiri, ulianza rasmi Julai 26, mwaka huu.
Ulikamilika Agosti 4 na ripoti hiyo ilikabidhiwa kwa Katibu Mkuu Kiongozi, Agosti 9, mwaka huu.
Hata
hivyo, kuanzia wakati huo, Luhanjo amekuwa ama akikwepa kujibu lini
ripoti hiyo itawekwa hadharani au akitoa majibu yanayoonyesha uwezekano
wa suala hilo kuwa ni ndoto.
Mara
ya kwanza, NIPASHE iliwasiliana na Luhanjo kwa njia ya simu na
alipoulizwa lini ripoti hiyo itawekwa hadharani, alikataa kuzungumzia
suala hilo kwa maelezo kwamba yuko kwenye kikao.
NIPASHE
iliendelea kumtafuta na kila ilipofanikiwa kupata simu yake, ilikuwa
ikipokelewa na mtu, ambaye mara zote alidai kuwa Luhanjo yuko kwenye
kikao.
Juzi
NIPASHE kwa mara nyingine ilifanikiwa kumpata Luhanjo kwa njia ya simu,
alipoulizwa lini ripoti hiyo itawekwa hadharani, alijibu kwa ufupi:
“Itakapokamilika tutawaita (waandishi wa habari) wote.” kisha akakata
simu.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)