REX ATTONEY YAHUSISHWA NA MALIPO YA SH7 BIL. YA UENDESHAJI KESI, DHAMANA YA SH8 BIL. NAYO YALIPWA LONDON
Neville Meena, Dodoma
WAKATI nchi ikiwa gizani kutokana na makali ya mgawo wa umeme, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limelipa mabilioni ya shilingi yanayotokana na kesi baina yake na Kampuni ya Dowans Holdings ya Costa Rica na mshirika wake, Dowans Tanzania Ltd.Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi umebaini kuwa hadi kufikia Machi mwaka huu, Tanesco ilikuwa imelipa Sh7.05 bilioni kwa Kampuni ya Uwakili wa Rex Attorneys kwa ajili ya kugharamia shughuli mbalimbali katika kesi dhidi yake na Dowans kwa upande mmoja na Kampuni ya Richmond kwa upande mwingine.
Neville Meena, Dodoma
WAKATI nchi ikiwa gizani kutokana na makali ya mgawo wa umeme, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limelipa mabilioni ya shilingi yanayotokana na kesi baina yake na Kampuni ya Dowans Holdings ya Costa Rica na mshirika wake, Dowans Tanzania Ltd.Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi umebaini kuwa hadi kufikia Machi mwaka huu, Tanesco ilikuwa imelipa Sh7.05 bilioni kwa Kampuni ya Uwakili wa Rex Attorneys kwa ajili ya kugharamia shughuli mbalimbali katika kesi dhidi yake na Dowans kwa upande mmoja na Kampuni ya Richmond kwa upande mwingine.
Malipo hayo kwa Kampuni ya Rex Attorneys yaliyofanywa kati ya Oktoba 6, 2008 na Machi 23, 2011 ni kwa ajili ya kesi namba 15910/VRO ambayo ni baina ya Tanesco na Richmond pamoja na kesi namba 15945/VRO ambayo ni baina ya Tanesco dhidi ya Dowans.
Moja
ya taarifa rasmi za Tanesco ambayo Mwananchi limeiona, inathibitisha
kwamba shirika hilo limekuwa likilipa fedha hizo kwa Rex Arttoneys
katika vipindi tofauti kutokana na huduma ambazo hutolewa na kampuni
hiyo ya uwakili.
Taarifa
hiyo iliyosainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, William Mhando,
inabainisha baadhi ya huduma ambazo Tanesco imezilipia na gharama zake
kwenye mabano.
Kupitiwa
kwa Mkataba wa Tanesco na Richmond (Sh29 milioni), gharama za
uwakilishi kwenye mahakama (Sh67.8 milioni) na gharama za uwakili
(Sh4.13 bilioni).
Hata
hivyo, Meneja Uhusiano wa Tanesco, Badra Masoud alipoulizwa kuhusu
malipo hayo, hakukanusha wala kuthibitisha, huku akitaka apewe muda hadi
jana saa nane mchana kwa ahadi kwamba angetoa majibu wakati huo.
Ulipofika
wakati huo Badra alisema: “Nimefuatilia lakini tumeshauriana hapa
kwamba muandike barua mkiuliza maswali yenu, halafu tutawajibu kwa
maandishi.”
Mmoja
wa mawakili katika Kampuni ya Rex Attoneys, Dk Thomas Nguluma alisema
jana kuwa, kampuni yao haikunufaika na kiasi chote cha Sh7 bilioni na
kwamba fedha nyingine zilikuwa zikipitia mikononi mwao kwa ajili ya
kulipia gharama nyingine za kuwezesha uendeshaji wa jumla wa kesi hiyo.
"Sidhani
kama hizo fedha zote zimelipwa kwetu. Japokuwa sina takwimu kwa sasa,
lakini mnatakiwa kufanya uchambuzi ili kufahamu ni kiasi gani cha fedha
ambacho kimetumika na fedha hiyo imetumika kwa ajili gani," alisema Dk
Nguluma na kuongeza:
"Kesi
hii ilikuwa ni kubwa sana na si kesi ndogo kama wengi wetu
tunavyodhani. Ni kesi ambayo ilituchukua zaidi ya mwaka mmoja na wakati
huo ilibidi tusitishe kazi zetu zote. Hatukuweza kufanya kazi nyingine,
ilikuwa ni hiyo Dowans tu."
Alitoa
mfano wa Sh111.4 milioni ambazo zilitumika kukodi ukumbi kwa ajili ya
kuendeshea usuluhishi huo wa kimahakama, kwamba fedha zote hizo
zililipwa katika Hoteli ya Kilimanjaro Kempinsk ambako kikao hicho
kilifanyika kwa siku nane mfululizo.
“Hizo
ni gharama za ukumbi, hapo kampuni yetu haikugusa hata senti tano, hapo
ni kila kitu pamoja na vifaa vyote vya kurekodia mwenendo wa kesi,
inawezekana pia majaji wale waliokuja kutoka huko ICC, kwa ufupi kuna
mambo mengi sana,” alisema Nguluma.
Alipotakiwa
kueleza kuhusu Sh67.8 milioni ambazo zimeandikwa kuwa ni ada ya
uwakilishi wa Tanesco/Dowans, alisema kuwa fedha hizo ni gharama za
mawakili wa nyongeza kutoka Uingereza ambao walikuwa wakiongoza jopo la
watetezi wa Tanesco.
"Tukichukua
mawakili kutoka Matrix Balisters nchini Uingereza ambao walitupa
mawakili wawili, hawa ndiyo waliokuwa wakiongoza jopo letu katika kesi
hii. Sasa hizo zote ni gharama hivyo hiyo (ada ya uwakilishi) ndiyo kazi
yake hiyo," alisema Dk Nguluma.
Utata Rex Attorneys
Hoja
zimekuwa zikitolewa kuhusu sababu za Tanesco kuendelea kufanya kazi na
kampuni hiyo ya uwakili hali kukiwa na taarifa kwamba imeshindwa kufanya
vizuri katika kesi dhidi ya Dowans.
Kadhalika,
kumekuwa na hoja kwamba Rex Attorneys ndiyo iliyoishauri Tanesco kulipa
tuzo hiyo badala ya kwenda mahakamani na kwamba kama hivyo ndivyo,
kampuni hiyo haifai kuendelea kufanya kazi na Tanesco katika mchakato wa
kukata rufaa.
Hata
hivyo, Dk Nguluma alikanusha taarifa hizo akisema Rex Attorneys ndiyo
iliyowezesha tuzo iliyotolewa kwa Dowans kupungua kutoka madai ya awali
ya Dola za Marekani 149 milioni hadi kufikia Dola 65 milioni.
Kuhusu
kukata rufaa, alisema taarifa yake kwenda Tanesco baada ya hukumu ya
ICC ilikuwa na ushauri wa kitaalamu unaoonyesha pande mbili ambazo
Serikali ilikuwa na uwezo wa kutumia mojawapo.
Alisema
baada ya Tanesco kuamriwa kulipwa fedha hizo, Rex Attorneys iliandika
waraka wa kisheria unaoishauri ukieleza wazi hasara na faida za kulipa
fedha hizo au kinyume chake. Hivyo Serikali kupitia shirika hilo kuamua
kupinga tuzo hiyo mahakamani.
“Sisi
tuliweka wazi faida na hasara za pande zote, kwamba kama wanaamua
kulipa basi watakuwa wametekeleza hukumu ya mahakama na kuachana na
suala hilo lakini pia tuliwaeleza udhaifu wa hukumu ambao wangeutumia
kukata rufaa,” alisema.
Malipo ya Sh8 bilioni
Taarifa
za malipo hayo zimekuja wakati Tanesco imeshalipa Sh8 bilioni katika
Mahakama Kuu, Uingereza ikiwa ni dhamana ya kutaka kuchelewesha ukazaji
wa hukumu dhidi yake baada ya maombi yaliyowasilishwa katika mahakama
hiyo na Kampuni ya Dowans.
Uamuzi
wa kutaka kulipwa kwa fedha hizo ulitolewa na Jaji Burton wa mahakama
hiyo baada ya Tanesco kupitia kwa mawakili wa kampuni ya Matrix kutaka
uamuzi dhidi ya ombi la Dowans la kupewa tuzo uahirishwe hadi kesi
iliyopo Mahakama Kuu ya Tanzania itakapotolewa uamuzi.
Rex
Arttoneys pia inadaiwa kwamba ndiyo iliyokuwa mtetezi wa Tanesco katika
kesi hiyo ambayo Dowans ilitaka Mahakama Kuu ya Uingereza kukazia
hukumu ili ilipwe tuzo iliyopewa na ICC ya Dola za Marekani milioni 65
sawa na wastani wa Sh104 bilioni kwa viwango vya sasa vya kubadilisha
fedha.
Hata
hivyo, Dk Nguluma alikanusha kwamba Rex Attorneys inahusika na utetezi
katika shauri hilo ambalo limeahirishwa hadi Novemba 22, mwaka huu
kusubiri uamuzi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, lakini akakiri kwamba wao
hushirikiana na mawakili wa Matrix katika kazi zao.
“Sisi
hapa ni mawakala tu na hatulipwi hata senti tano labda kama zitakuwa ni
gharama za upatikanaji wa nyaraka za kusaidia hao mawakili wa Kampuni
ya Matrix ambao wametafutwa na Tanesco,” alisema Dk Nguluma na kuongeza:
“Ila
kwa sababu sisi ndiyo tunafanya kazi ya huo uwakala, nina taarifa
kwamba Tanesco wamelipa hiyo dola milioni tano kwa ajili ya kuwezesha
shauri lililofunguliwa na Dowans kuahirishwa hadi Novemba 22, mwaka
huu.”
Habari
zilizopatikana zinadai kwamba mawakili wa Matrix pia walidai kulipwa
fedha za utangulizi kutoka Tanesco kiasi cha Paundi 500,000 za Uingereza
zaidi ya Sh1 bilioni na kwamba fedha hizo zilikuwa katika mchakato wa
kulipwa.
Hata
hivyo, kwa mujibu wa taratibu za kisheria iwapo Tanesco watafanikiwa
kuzuia malipo ya Dowans pale Mahakama Kuu itakapotoa uamuzi wake, basi
fedha zilizowekwa kama dhamana nchini Uingereza zitarejeshwa.
Dk
Nguluma alisema ikiwa Tanesco itashindwa basi fedha hizo zitakuwa mali
ya Dowans na kwamba Tanesco italazimika kulipa fedha nyingine
zilizobaki, gharama za kesi husika na riba ya fedha zinazopaswa kulipwa
Dowans.
Hali ya Umeme
Jana,
Serikali iliwasilisha bungeni taarifa kuhusu hali upungufu wa umeme
ikisema kuwa tatizo kubwa ni kuharibika kwa mfumo wa kusafirisha gesi
kutoka Songosongo na uhaba wa mafuta ya kuendeshea mitambo ya IPTL.
Juzi,
Spika wa Bunge, Anne Makinda aliitaka Serikali kutoa maelezo bungeni
kuhusu sababu za hali hiyo nchini kutokana na hoja iliyotolewa na Mbunge
wa Nyamagana (Chadema), Ezekia Wenje.
Wenje
alitaka bunge kuahirisha mjadala wa Bajeti ya Wizara ya Maliasili na
Utalii, ili kujadili dharura ambayo alisema ni maeneo mengi nchini
kutokuwa na umeme.
Sambamba
na tatizo hilo, Serikali hivi sasa inasaka Sh408 bilioni kwa ajili ya
kutekeleza mpango wa dharura wa kuondokana na giza ambao uliowasilishwa
bungeni Agosti 13, mwaka huu na kupigiwa vigelegele na wabunge wengi.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)