Msimu
mpya wa Ligi Kuu ya Vodacom 2011/2012 unaanza kesho (Agosti 20 mwaka
huu) ambapo timu 10 kati ya 14 zinazoshiriki katika ligi hiyo zitakuwa
viwanjani. Mechi za kesho ni Coastal Union v Mtibwa Sugar (Mkwakwani,
Tanga), Kagera Sugar v Ruvu Shooting (Kaitaba, Bukoba), Toto Africans v
Villa Squad (Kirumba, Mwanza) na Polisi Dodoma v African Lyon (Jamhuri,
Dodoma).
Mechi
nyingine ni Azam v Moro United itakayochezwa Chamazi, Dar es Salaam
wakati mechi za Jumapili (Agosti 21 mwaka huu) ni Oljoro JKT v Simba
(Sheikh Kaluta Amri Abeid, Arusha), na Yanga watakaokuwa wenyeji wa JKT
Ruvu.
WAAMUZI WA KATI
Waamuzi
wa kati (centre referees) 16 wameteuliwa kuchezesha Ligi Kuu. Waamuzi
hao ni Ronald Swai (Arusha), Isihaka Shirikisho (Tanga), Peter Mujaya
(Mwanza), Amon Paul (Mara), Mathew Akrama (Mwanza), Ibrahim Kidiwa
(Tanga), Dominic Nyamisana (Dodoma), David Paul (Mtwara), Hashim
Abdallah (Dar), Martin Saanya (Morogoro), Orden Mbaga (Dar), Kennedy
Mapunda (Dar), Israel Mujuni (Dar), Alex Mahagi (Mwanza), Abdallah
Kambuzi (Shinyanga) na Thomas Mkombozi (Kilimanjaro).
Pia
wameteuliwa waamuzi wa akiba (reserve referees) sita ambao watatumika
wakati wowote watakapohitajika. Waamuzi wasaidizi (assistant referees)
walioteuliwa kuchezesha ligi ni 34. Kwa upande wa waamuzi wasaidizi wa
akiba walioteuliwa ni kumi. Hivyo jumla ya waamuzi watakaotumika kwenye
ligi hiyo ni 50.
MAKAMISHNA WA MECHI
Jumla
ya makamishna (match commissioners) 24 wameteuliwa kusimamia mechi za
ligi hiyo. Kati ya hao 20 ni wa zamani na wanne ni wapya. Makamishna
wapya ni Charles Ndagala, Victor Mwandike, Godbless Kimaro na Hamis
Tika.
Makamishna
wa msimu uliopita walioteuliwa tena ni Hamis Kissiwa, David Lugenge,
Abdallah Mitole, Charles Komba, George Komba, Jimmy Lengwe, Amri Kiula,
James Mhagama, Fulgence Novatus, Pius Mashera, Michael Bundara, Gabriel
Gunda, Mohamed Nyange, Mwijage Rugakingira, Arthur Mambeta, Paul Opiyo,
Edward Hiza, Salim Singano, William Chibura na Omary Mwamela.
Uteuzi
wa makamishna kama ilivyo kwa waamuzi ulifanyika baada ya kuhudhuria
kozi na kufanya mitihani. Kwa upande wa makamishna ambao hawakufanya
vizuri, watalazimika kurudia mitihani kabla ya kuteuliwa tena.
NAULI KWA TIMU ZINAZOSHIRIKI LIGI
Kila
timu inayoshiriki ligi itapata jumla ya sh. milioni 26.3. Fedha hizo
zitatolewa kwa awamu tano tofauti kuanzia mwezi huu. Agosti kila timu
itapata sh. 4,732,142, Septemba (sh. 4,732,142), Oktoba (sh. 5,622,321),
Januari (sh. 5,622,321) na Machi (sh. 5,622,321).
Jumla
ya fedha kutoka kwa mdhamini wa ligi, Kampuni ya simu za mkononi ya
Vodacom ambazo zitatumika kwa ajili ya nauli kwa timu zote katika msimu
mzima ni sh. 368,637,458.
MECHI YA STARS, ALGERIA
Tumeiandikia
barua Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kuomba iruhusu
mechi ya mchujo ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika zitakazofanyika
mwakani Equatorial Guinea na Gabon kati ya Taifa Stars na Algeria
(Desert Warriors) ichezwe Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Ombi
letu limetokana na ukweli kuwa tulishaliarifu Shirikisho la Mpira wa
Miguu Afrika (CAF) miezi mitatu iliyopita kuwa mechi hiyo itachezwa
katika uwanja huo. Taarifa hiyo pia tuliipa Algeria ambayo imeshatuma
ujumbe wake kukagua hoteli ambayo timu yao itafikia.
Kwa
upande wa CAF uamuzi wa kubadili uwanja hivi sasa maana yake kuwa
itatupiga faini, lakini vilevile TFF tutalazimika kuingia gharama za
kusafirisha kwa ndege timu zote mbili pamoja na waamuzi kwenda Mwanza
kwa ajili ya mechi hiyo.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)