Waasi wakishangilia
Picha za televisheni zinaonyesha waasi katika uwanja wa Green Square katika mji mkuu, huku makundi ya watu wenye furaha wakisheherekea kuwasili kwa waasi hao katika uwanja huo.
Inaripotiwa waasi wamemkamata mwanawe Gaddafi Saif al-Islam, huku kiongozi mwenyewe akiahidi kuwa ataendelea kupigana.
Mwendesha mashtaka wa mahakama ya uhalifu wa kivita, Luis Moreno Ocampo amethibitisha Saif al-Islam, mwanawe Gaddafi, na ambaye alitarajiwa kumridhi babake amekamatwa.
Mwanawe wa kifungua mimba Mohammed Al Gaddafi naye amejisalimisha kwa waasi na anazuiliwa ndani ya makaazi moja mjini Tripoli.
Serikali ya Libya imesema takriban wanajeshi elfu 65 watiifu kwa kanali Gaddafi wamebakia mjini Tripoli lakini ni wachache tu walioonekana wakati waasi walipokuwa wakielekea kuuteka mji huo.
Mapigano yameripotiwa katika maeneo mengine ya mji. Mwandishi wa BBC mjini Tripoli amesema waasi wanajaribu kushika udhibiti wa jengo ambalo waandishi wa habari wako.
Inaaminika kuwa bado Kanali Gaddafi ana maelfu ya wafuasi waliojihami, japo ripoti zinaashiria kuwa idadi kubwa wamejisalimisha kwa waasi.
Msemaji wa serikali ya Libya , Moussa Ibrahim, amesema takriban watu 1300 wameuwawa mjini humo.
Awali Kanali Gaddafi aliwataka raia kujitokeza na kuukomboa mji wa Tripoli. '' Jitokezeni, jitokezeni niko nanyi. Msirudi nyuma. Tutapigana hadi kuikomboa nchi yetu kuzuia uthibiti. Msiwakubalie wanyakuzi kuiteka nchi yetu, nitapigana pamoja nanyi kama nilivyoahidi'', Alisema Muammar Gaddafi.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)