KATIKA kile kinachoonekana kuwa ni kumshinikiza Rais Jakaya Kikwete kutekeleza ahadi alizotoa wakati wa kampeni za urais mwaka jana, Chadema kimesema kitatumia kura za maoni kumwajibisha ikiwa atashindwa kuzitekeleza.Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa aliwaambia maelfu ya wakazi wa Mji wa Songea mkoani Ruvuma kuwa wamegundua kwamba katika nchi nyingine, akitolea mfano, Japan, kama waziri mkuu wao akishindwa kutimiza ahadi zake, wananchi hupiga kura za maoni.
Akihutubia mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Shule ya Msingi Kibulangoma, Dk Slaa alisema chama chake kilipoanza kuandamana, Rais Kikwete alisema kuwa wanapanga njama za kumwondoa madarakani na kutokana na hilo, kiliamua kuchunguza sababu za Rais kutoa kauli hiyo.
"Serikali ikichaguliwa si lazima akae miaka mitano ikiwa ni kama hajatekeleza ahadi za wananchi na kama hatupi elimu bora na bure kushusha bei ya sukari na mabati. Kama ameshindwa hilo tutamwondoa kwa kura za maoni," alisema Dk Slaa."Tutaandamana na kupiga mchakamchaka ili hoja zetu tulizoahidiwa zitekelezwe kupitia Bunge kwa kuwa nchi itakalika kama wananchi wana amani na maisha mazuri," alisema Dk Slaa.
Alidai kuwa Rais Kikwete amekuwa hawajali wananchi ikiwa ni pamoja na kutokuwashukuru kwa kumpigia kura, akidai kwamba tangu aingie madarakani katika awamu hii, amekuwa akisafiri nje ya nchi badala ya kuwatembelea wananchi wake."Kikwete atueleze alichaguliwa na Ulaya au Tanzania, anasafiri nje kila mwezi badala ya kuwashukuru wananchi waliomchagua," alisema Dk Slaa.
Katika hatua nyingine, Dk Slaa alisema kuwa CCM kimekuwa kikiishambulia Chadema kuwa kinafanya ufisadi kwa kununua magari yaliyotumika, akisema walishasema kwamba watanunua malori ya Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe kwa kuwa wamekuwa wakiyatumia tangu yakiwa mapya.Kwa Habari zaidi
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)