NGORIKA NA HIACE YAUA WATU 10 ARUSHA - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

NGORIKA NA HIACE YAUA WATU 10 ARUSHA


 
Basi la Ngorika aina ya Scania likiwa limepinduka baada ya kuligonga ubavuni Hiace na kusababisha watu tisa waliokuwepo ndani ya gari hilo kufariki papo hapo.

 
Dereva  wa basi  la Ngorika, Emmanuel Mchoro(30) akiwa amebebwa kutoka ndani ya basi hilo akiwa amekufa, baada ya kulaliwa na basi hilo kwa muda wa masaa matano.
 
Baiskeli inayodaiwa kusababisha ajali hiyo ikipakiwa kwenye gari.  Hata hivyo, mpanda baiskeli hiyo, Elvisa Msukuma, alifariki dunia kwa kugongwa na Haice.
 
Umati wa watu wakiwemo wasafiri wakishuhudia  ajali hiyo.
 
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Isdore shirima (kulia), akipokea maelezo kutoka  kwa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Arusha (RCO) Lenard Paulo, eneo la tukio baada ya kushuhudia gari aina ya Hiace likiwa limeharibika vibaya baada ya kugongwa na basi la Ngorika.

Na Joseph Ngilisho, Arusha
WATU  10 wamefariki dunia na wengine wanane  kujeruhiwa -- wanne kati yao wakiwa katika hali mbaya -- baada ya  magari waliyokuwa wakisafiria kugongana na kupinduka katika eneo la  Makumira  wilaya ya Arumeru mkoani Arusha majira ya saa 12.20 asubuhi.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha,Thobias Andengenye, ajali hiyo imehusisha gari aina ya Toyota Hiace lenye namba za usajili T 773 BGT   lililokuwa likiendeshwa na Selemani Juma (30) mkazi wa Kijenge,  na basi la Ngorika aina ya Scania lenye namba T 633 ANF lililokuwa likiendeshwa na Emmanuel Mchoro (30) mkazi wa Mwanga Kilimanjaro.

Andengenye alisema chanzo cha ajali hilo kimetokana na Hiace kutaka kulipita gari lililokuwa mbele yake ambapo alikuweko pia mwendesha baiskeli. Hata hivyo, kabla ya kufikia uamuzi huo aliona basi hilo la Ngorika likija kwa kasi ndipo alipoamua  kulikwepa ili asigongane nalo uso kwa uso.

Kabla hajamaliza kufanya hivyo basi la Ngorika liliigonga Hiace hiyo ubavuni na kusababisha  watu tisa waliokuwa ndani ya gari hilo kufariki dunia papo hapo.

Andengenye aliwataja marehemu hao kuwa ni: Kizo  Rafael Ndosi (35) mkazi wa Arumeru, Patriki Temba (28) mkazi wa Usa River, Samsoni Emanuel Minja (60), Hamisi Charles(30) mkazi Usa River, John Kess(38) mkazi wa Majichai na Huruma  Safiel (28) mkazi wa Usa River.

Wengine ni Emmanuel Mchoro (30) mkazi wa Mwanga ambaye yeye ni dereva wa basi la Ngorika na Fatuma Msuya (35) mkazi wa Usa River ambaye ni mwanamke pekee aliyefariki katika ajali hiyo na mpanda baiskeli aliyejulikana kwa jina moja la Elvisa.


Alisema mpaka sasa jeshi la polisi linamshikilia dereva wa Hiace mpaka pale upelelezi utakapokamilika.


Mganga Mkuu Mkoa wa Arusha, Salashi Toure, alisema wamepokea majeruhi 16 ambapo kati ya hao mmoja amehamishiwa hospitali ya Seliani kutokana na mapafu yake kuvuja damu nyingi.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages