BAGBO AKAMATWA BAADA YA PURUKUSHANI NA MPINZANI WAKE - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

BAGBO AKAMATWA BAADA YA PURUKUSHANI NA MPINZANI WAKE

 
Kiongozi wa Ivory Coast, Laurent Gbagbo (kushoto) na mkewe Simone wakiwa chini ya ulinzi baada ya kukamatwa hapo jana.
Kiongozi wa Ivory Coast, Laurent Gbagbo ametiwa kizuizini mjini Abidjan na kuwekwa chini ya ulinzi wa polisi wa Umoja wa Mataifa.

Alikamatwa wakati majeshi ya kiongozi anayetambulika kimataifa kuwa Rais wa nchi hiyo Alassane Ouattara na vifaru vya Ufaransa kuingia kwenye makazi yake.

Bw Gbagbo alikuwa akikataa kukabidhi madaraka, akisema alishinda uchaguzi wa Rais wa mwezi Novemba.

Ufaransa ilisema majeshi yanayomwuunga mkono Ouattara yalimkamata, lakini washirika wa Bw Gbagbo walisema ni majeshi maalum ya Ufaransa.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon alisema kukamatwa kwa Bw Gbagbo kumemaliza miezi kadhaa ya ghasia zisizo na sababu, na Umoja wa Mataifa utaunga mkono serikali mpya.

Majeshi ya kutunza amani ya umoja huo yaliyashutumu majeshi yanayomwuunga mkono Bw Gbagbo kwa kuhatarisha maisha ya raia na kuiomba Ufaransa, ambalo lilikuwa koloni lake, kuondosha silaha nzito za kiongozi huyo.
 
Kumekuwa na madai ya ukatili kufanywa na wote wafuasi wa Gbagbo na Ouattara, na umoja huo una taarifa ya zaidi ya watu 1,000 kuuawa na takriban 100,000 kukimbia nchi hiyo.

Wawakilishi wa kudumu wa Umoja wa Mataifa wa Ivory Coast, Youssoufou Bamba, walisema Bw Gbagbo atashtakiwa.

Mjini London, Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza William Hague alisema kama atafunguliwa mashtaka, basi ashtakiwe kwa kuzingatia njia zinazostahili.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Bi Hillary Clinton alisema mjini Washington kwamba kukamatwa kwa Bw Gbagbo kumepeleka ujumbe kwa "madikteta" ambao "hawatopuuza sauti za watu wao katika uchaguzi wa haki na huru."

Chanzo: BBC Swahili

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages