Mussa Juma, Samunge
MCHUNGAJI Ambilikile Mwasapila anayetoa tiba ya magonjwa sugu huko Samunge Loliondo, juzi jioni aliondoka hapa kwenda Babati, Manyara kuhudhuria mazishi ya mtoto wake huku safari yake hiyo ikiratibiwa na Serikali na akipewa ulinzi mkali wa maofisa usalama na polisi.
Aliondoka Samunge saa 12:20 jioni na gari la Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro akiwa na maofisa hao wa usalama, polisi na wasaidizi wake.
Kabla ya kuondoka Samunge, watu mbalimbali walikuwa wamejitolea kumpatia usafiri mchungaji huyo lakini walizuiwa kutokana na sababu za kiusalama.
"Tulikaa kama kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya, tukaona ni busara tuchukue jukumu la kumsafirisha Mchungaji hasa kutokana na sababu za kiusalama," alisema ofisa mmoja mwandamizi wa serikali wilayani hapa.
Alisema mchungaji huyo atalindwa akiwa msibani na atakaporejea Samunge.
Warundi, Wakenya, Waganda wakwama
Zaidi ya raia 100 kutoka Kenya, Burundi na Uganda, wamekwama Samunge kutokana na kusitishwa kwa tiba hiyo hadi Ijumaa.
Licha ya hatua hiyo ya kusitishwa kwa huduma kutangazwa mapema, maelfu ya watu, wakiwamo raia hao wa kigeni, waliendelea kumiminika Samunge kupata matibabu hayo.
Profesa Hakizimana Godefroid kutoka eneo la Muyumba, Burundi akiwa na ujumbe wa watu saba alisema wametumia siku saba kufika hapa na kwamba hatua hiyo imewasikitisha."Gari hili tumekodi kutoka Burundi hadi hapa, tunasikitika sana kukuta hakuna huduma na tunaambiwa ilitangazwa hapa Tanzania pekee kitu ambacho si kizuri," alisema Godefroid.
Alisema kutokana na taarifa ya tiba ya Mwasapila kusambaa karibu nchi zote za Afrika na nje ya bara,Serikali ilipaswa kutoa taarifa za kusitishwa kwa huduma hiyo katika balozi zake zote zilizopo nchini."Tumeondoka Burundi tukijua kuwa huku Tanzania tiba inatolewa tena tulijua hata siku za Pasaka tiba inaendelea. Taarifa zingesambazwa mapema tusingekuja sasa," alisema Godefroid.
Ofisa Uhamiaji ambaye yupo Samunge, Suleiman Saanane akishirikiana na polisi, juzi na jana walitumia muda mwingi kuwaelimisha raia hao wa nchi jirani juu ya kusitishwa kwa tiba hiyo na namna Serikali inavyoisimamia. Raia wa Kenya na Uganda, Peter Kimath na Joram Batengi, walishauri Serikali ya Tanzania kuipa hadhi tiba inayotolewa na Mchungaji Mwasapila wakisema, inawaponya watu na inavyoonekana, maelfu ya watu watafika Samunge.
"Hatuoni kama huyu mzee anapewa usaidizi ila tunachoona ni Serikali kukusanya kodi tu hapa ya magari na helikopta. Sasa kama wanapata fedha nyingi waitambue rasmi hii tiba na kuweka utaratibu mzuri," alisema Kimath. Batengi aliishauri Serikali kuboresha mazingira ya Samunge hasa barabara na eneo la tiba ili watu wanaotoka nchi za nje waamini kwamba tiba hiyo inaponya.
"Uganda wengi wanajua tiba hii na kuna ambao wanasema kuwa wamepona ila ukifika hapa huwezi kuamini kama tiba hii ni nzuri kwani mazingira ya hapa siyo mazuri na hata njia za kufika hapa ni mbaya sana," alisema Batengi.
Raia hao wanalazimika kubaki Samunge hadi Ijumaa siku ambayo Mchungaji Mwasapila atarejea na kuendelea kutoa tiba. Mchungaji Mwasapila anatarajiwa kurejea Samunge leo baada ya kushiriki katika mazishi ya mtoto wake Jackson (43), yaliyofanyika jana.
Msaidizi wa Mchungaji huyo, Frederick Nisajile aliliambia gazeti hili jana kuwa baada ya kurejea, wataanza maandalizi ya kuchemsha dawa ambayo itatumika Ijumaa.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)