Ufaransa imeahidi Kuendelea Kuisaidia Tanzania katika Shughuli za Kijamii ikiwemo maji, Elimu na Afya. - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

Ufaransa imeahidi Kuendelea Kuisaidia Tanzania katika Shughuli za Kijamii ikiwemo maji, Elimu na Afya.

 Rais Jakaya Kikwete akimkaribisha kwa mazungumzo Bwana Dov Zerah,Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa(Director General of French Development Agency).Rais Kikwete alikutana na mgeni huyo wakati wa mkutano wa 5 wa EITI uliofanyika huko Paris nchini Ufaransa tarehe 3.3.2011.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akifanya mazungumzo na Rais wa umoja wa wadau wa sekta ya uchumi ya Ufaransa (MEDEF) Bwana Philippe Gautier. Rais Kikwete alikutana na mgeni huyo baada ya kuhudhuria kikao cha 5 cha Mpango wa Uhamasishaji wa Uwazi na uwajibikaji katika Fasnia ya uziduaji (Extractive Industries Transparency Iniative),EITI,huko Paris nchini Ufaransa tarehe 3.3.2011.Picha na John Lukuwi
----
Ufaransa imeahidi kuendelea kuisaidia Tanzania katika shughuli za kijamii ikiwemo maji, elimu na afya.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa Bwana Dov Zerah amemueleza Rais Jakaya Kikwete walipokutana mjini Paris, Ufaransa tarehe 3 Machi, 2011.

“Tuko tayari kuwasaidia zaidi, leteni mahitaji yenu nasi tutawasaidia katika Nyanja za elimu, maji na afya” amesema Bw. Zerah na kueleza kuwa Ufaransa inaridhika na kufurahishwa na uhusiano wake mzuri na Tanzania.


Rais Kikwete yuko mjini Paris kuhudhuria mkutano wa 5 duniani juu ya Tasnia ya Uziduaji, Extractive Industries Transparency Initiative (EITI) ambayo ni taasisi ya kidunia inayoangalia na kuhakikisha kuwa raslimali za madini, gesi na mafuta zinanufaisha nchi na kwamba makampuni yanayowekeza katika nchi hizo hayazizulumu nchi husika.

Katika kikao hicho cha siku mbili, Rais Kikwete amezungumzia juu ya hali ya baadae ya taasisi hiyo na uwazi katika kukusanya kodi ambapo, hususan matokeo ya uwazi katika kodi na uwajibikaji nchini Tanzania ambapo ameelezea changamoto za ulipaji kodi katika sekta ya madini na juhudi zinazofanywa na serikali yake katika kuhakikisha kuwa nchi inanufaika na madini hayo ambayo ni raslimali kubwa katika nchi ya Tanzania.


“Tumekuwa tukiwasiliana na wananchi juu ya mambo yanayoendelea katika sekta ya madini na mwaka 2006, tuliunda tume ya kuangalia na kupitia mikataba ya madini kwa minajili ya kuona mapungufu na kuhakikisha kuwa pande zote mbili zinanufaika katika mikataba hii” amesema.

Juhudi zingine ni pamoja na taasisi ya ukaguzi wa madini, Tume ya Rais ya Madini na kwamba moja ya mapendekezo ya Tume ya Rais ya Madini, ni Tanzania kujiunga na EITI ili kuleta uwazi katika sekta ya madini.

Akiwa mjini Paris, Rais pia amekutana na Naibu Waziri masuala ya Bunge Bw. Stephen O’brien, viongozi wa Umoja wa Wafanyabiashara wa Ufaransa, ambao wanatarajia kufanya ziara nchini Tanzania mwezi wa Julai na Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Ufaransa, Bw. Alain Juppe.

Rais anaondoka Paris tarehe 4, Machi kuelekea Nouakchott, Mauritania ambapo atakutana na jopo la Marais wenzanke kutoka Mauritania, Afrika Kusini, Burkina Faso, Chad, Nigeria na Equatorial Guinea pamoja na wawakilishi wa Jumuia ya Uchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS), Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AU) Balozi Jean Ping na Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa (UN).
Viongozi hao kwa pamoja wanatarajia kufikia uamuzi wa Umoja wa Afrika kuhusu mgogoro wa Ivory coast na kupendekeza namna ya kuutatua.


Mwisho.

Imetolewa na Premi Kibanga,

Mwandishi wa Habari wa Rais,Msaidizi

Paris-Ufaransa

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages