Neno La Leo: Tunaangamia Kwa Kukosa Hekima! - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

Neno La Leo: Tunaangamia Kwa Kukosa Hekima!

Ndugu Zangu,
MFALME Suleiman aliambiwa ndotoni aombe kitu chochote kwa Mola wake, naye akajibu; “ Ewe Mola wangu, nipe mimi mtumwa wako moyo wa adili ili niwahukumu watu wako, na kupambanua mema na mabaya, maana ni nani awezaye kuwahukumu hawa watu wako walio wengi?”

Hivyo basi, Mfalme Suleiman alichagua hekima. Maana, ni Mfalme Suleiman huyo anayekaririwa na vitabu vya dini akitamka, kuwa; “ Watu wangu wanaangamia kwa kukosa hekima”.


Naam, hekima ndilo jambo lililo bora kabisa kwa mwanadamu kuwa nalo. Mwanadamu aliyepungukiwa hekima ana hasara kubwa maishani. Hekima ni tunu na kipaji ambacho Mwenyezi Mungu amewajalia waja wake, ili nao waweze kupambanua na kuamua kati ya yaliyo mema na maovu. Duniani hakuna shule ya hekima.


Nakumbuka nilipokuwa kijana mdogo nilitamani sana kilimo. Marehemu babu yangu alimiliki ardhi kubwa kijijini kwetu Nyeregete, Mbarali. Nilimwomba anipe ardhi ya kulima, naye alinipa kipande kidogo cha ardhi, chapata robo eka.


Akaniambia huku akinionyesha kwa mikono; ” Hapa utachagua mwenyewe, ama ulime mpunga au mahindi”. Kisha akanikabidhi jembe kubwa jipya mfano wa kopa. Hakunipa mpini, na jembe halikunolewa. Nikamwomba anisaidie na vyote viwili, mpini na kunolewa jembe. Naye akanijibu; ” Mpini utautafuta mwenyewe, na jembe hunolewa ardhini”. Kwangu mimi, ile inabaki kuwa shule kubwa ya juu ya nini maana ya maisha na namna ya kupambana ili kuishi.


Naam. Duniani hakuna shule ya hekima. Kuwa na hekima ni kuwa na tunu, kuwa na kipaji ambacho binadamu hujaliwa nacho. Na mwingine atajiuliza; hekima ni nini? Ni ule uwezo wa mwanadamu kuwa na maarifa ya kufahamu kipi cha kufanya, kwanini afanye, wapi na kwa wakati gani. Hivyo basi, hekima ni maarifa, tunaangamia kwa kukosa maarifa, kukosa hekima. Na tuitafute hekima. Na hilo ni Neno La Leo.


Maggid,


Dar es Salaam

Machi 13, 2011

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages