RAISI WA TFF LEODEGAR TENGA AULA CAF - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

RAISI WA TFF LEODEGAR TENGA AULA CAF


 RAIS wa Shirikisho la soka Tanzania (TFF) Leodegar Tenga
---
RAIS wa Shirikisho la soka Tanzania (TFF) Leodegar Tenga amechaguliwa kuwa mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la soka Afrika (CAF) katika uchaguzi uliofanyika jana jijini Khartoum, Sudan.
Tenga aliyekuwa akiwania nafasi hiyo kupitia Kanda ya Mashariki na Kati, alimshinda Celestine Musabiyima wa Rwanda aliyekuwa akitetea nafasi hiyo, Tenga ambaye pia ni rais wa Baraza la Vyama vya soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) alipata kura 34 dhidi ya 19 za mpinzani wake.

Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura, anakuwa Mtanzania wa pili kuingia kwenye Kamati ya Utendaji ya CAF baada ya Said Hamad El Maamry ambaye aliwahi kushinda nafasi hiyo mwanzoni mwa miaka ya 1980 kwa vipindi viwili mfululizo.

Wambura alisema alishindwa kutetea nafasi hiyo katika kipindi cha tatu baada ya TFF wakati huo ikiitwa Chama cha Mpira wa Miguu (FAT) kutoidhinisha jina lake CAF. El Maamry hivi sasa ni mjumbe wa heshima wa CAF.

Wambura alisema Mtanzania mwengine aliyewahi kuwania nafasi hiyo mara mbili, lakini hakufanikiwa kushinda ni Muhidin Ndolanga ambaye aliwania wakati huo akiwa Mwenyekiti wa FAT sasa TFF.
Kalusha Bwalya naye amefanikiwa kwa mara ya kwanza kuingia kwenye Kamati ya Utendaji ya CAF baada ya kuchaguliwa jana akiwakilisha Kanda ya Kusini mwa Afrika. Bwalya ambaye alikuwa mwanasoka bora wa Afrika mwaka 1988 aliwashinda wagombea wengine wanne.

Aliwashinda Adam Mthethwa wa Swaziland, Walter Nyamilandu (Malawi), John Muinjo (Namibia) na Justino Fernandes wa Angola.Nafasi ya Kanda ya Magharibi mwa Afrika ilitwaliwa na Kwesi Nyantakyi wa Ghana.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages