MUAMMARAR GADDAFI : KIONGOZI WA LIBYA ALIYETAWALA TANGU 1969 - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

MUAMMARAR GADDAFI : KIONGOZI WA LIBYA ALIYETAWALA TANGU 1969


NI mwaka 1969!  Watu wengi wanaosoma safu hii sasa walikuwa hawajazaliwa.  Wengine walikuwa watoto wadogo au vijana ambao kwa leo si rahisi kukumbuka.

Ni tangu mwaka huo hadi leo Februari 26, 2011 kiongozi huyo wa Libya, Muammar al-Gaddafi, ambaye jina lake kamili ni Muammar Abu Minyar al-Gaddafi amekuwa madarakani tangu aongoze mapinduzi ya kijeshi kuung’oa utawala wa Mfalme Idris.

Alishika uongozi akiwa waziri mkuu hadi 1972 na baadaye taarifa za serikali zikawa zinamtaja kama “Kiongozi wa Mapinduzi Makuu ya Kisoshalisti ya Septemba Mosi ya Jamhuri ya Watu wa Libya” au “Kiongozi Mpendwa wa Mapinduzi”.

Baada ya kufa kwa aliyekuwa Rais wa Gabon, Omar Bongo, Juni 8, 2009, Gaddafi akawa kiongozi (asiye mfalme) aliyekaa madarakani kwa muda mrefu zaidi duniani, na mmoja wa viongozi waliokaa madarakani muda mrefu zaidi katika historia.

Pia, ni kiongozi wa Libya aliyekaa madarakani muda mrefu zaidi tangu nchi hiyo ilipokuwa jimbo la Himaya ya Ottoman (Uturuki ya leo) mwaka 1551.

Gaddafi alizaliwa Juni 7, 1942 katika familia ya Kibedui karibu na Sirt, akasoma na kupata mafunzo ya kijeshi nchini Uingereza.

Septemba 1, 1969, aliongoza kundi dogo la maofisa wa ngazi za chini jeshini kumwangusha Mfalme Idris wakati akitibiwa nchini Uturuki. 

Mpwa wa mfalme huyo, aliyekuwa mfalme mtarajiwa, Sayyid Hasan ar-Rida al-Mahdi as-Sanussi, alikuwa amekamatwa.  Ufalme ukafutwa na Jamhuri ya Kiarabu ya Libya ikatangazwa. Gaddafi aliyekuwa kijana mwembamba mwenye umri wa miaka 27 tu, akawa ndiye “Che Guevara” (mwanamapinduzi) wa Libya.

Libya ikawa nchi iliyopinga waziwazi ubeberu na uonevu duniani, kwa maneno na vitendo.  Matokeo yake Libya ikatengwa na mataifa ya kibeberu duniani.

Kwa nchi changa na na mataifa yenye kupinga ubeberu, Gaddafi akawa kipenzi chao, hususan wapigania uhuru wote duniani ambao aliwapa misaada kibao bila ya woga, jambo lililozidi kuwaudhi wababe wa dunia.

Baada ya kumpindua mfalme, Libya ilianzisha Baraza Kuu la Kimapinduzi, Gaddafi akiwa mwenyekiti wake ambapo mwaka 1970 akaanzisha cheo cha waziri mkuu alichokishika na kukiacha mwaka 1972.

Tofauti na wanamapinduzi wengine wa kijeshi, Gaddafi hakutaka kujipa cheo cha ujenerali, alijipandisha cheo kutoka kepteni na kuwa kanali tu – cheo ambacho ameendelea kuwa nacho hadi leo.

Pamoja na kuchekwa na watu wengi kwamba mtu hawezi kuitawala nchi na kuwa Amiri Jeshi Mkuu wakati akiwa kanali, Gaddafi aliwaambia wakosoaji wake akisema: “Nchi hutawaliwa na watu!”

Madai ya mabeberu kwamba anasaidia ugaidi duniani yalisababisha Libya kushambuliwa na ndege za Marekani Aprili 6, 1986 ambapo zaidi ya watu 60 waliuawa, akiwemo Hannah, binti wa kuasili wa Gaddafi.

Gaddafi  muumini wa  Umoja wa Afrika, Usoshalisti wa Kiislam na Umoja wa Waarabu, amefanya juhudi nyingi kupigania hayo japokuwa imekuwa ikishindikana.

Lakini, kimataifa, msimamo wake wa kupigania haki wakati mwingine umewakanganya hata marafiki zake, kwani kuna wakati amekuwa akiunga mkono vikundi ambavyo vimedhihirika kuwa ni vya wafanya vurugu tu.

Ndiye Gaddafi  aliyekuwa maarufu katika ulimwengu wa wapigania uhuru, maendeleo na haki tangu Palestina, Namibia hadi Cuba.

Ni serikali ya Gaddafi ambayo mwaka jana iliahidi kujenga bure nyumba zipatazo 500 kwa waathirika wa mafuriko huko Kilosa nchini Tanzania.
Ni kiongozi huyohuyo wa Libya ambaye leo yuko matatani na watu wake aliowatawala kwa miaka 42!

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages