TAARIFA YA SERIKALI KUHUSU MILIPUKO YA MABOMU YA GONGO LA MBOTO - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

TAARIFA YA SERIKALI KUHUSU MILIPUKO YA MABOMU YA GONGO LA MBOTO

Watu 24 wamethibitika kufa katika ajali ya milipuko ya mabomu iliyotokea katika kambi ya Jeshi la Wananchi Tanzania kikosi cha 511, Gongo la Mboto Dar es Salaam tarehe 16/02/2011.

Taarifa ya Serikali imeeleza kwamba marehemu wote 24 walitambuliwa na Serikali kugharamia mazishi yao kama ilivyoahidi. Baadhi ya marehemu walisafirishwa kwenda kuzikwa makwao katika Mikoa ya Kagera, Mara, Tanga, Kilimanjaro, Pwani, Lindi, Mbeya, Mtwara na Dar es Salaam.

Hata hivyo maiti moja ya kichanga cha miezi minane mpaka sasa haijathibitika kuwa kifo chake kilitokana na milipuko ya mabomu, kutokana na taarifa zake za awali kutopatikana katika orodha ya majeruhi waliopokelewa katika dispensari ya Kitunda, Hospitali ya Amana na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.


Taarifa ya awali kutoka chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospital ya Muhimbili ilimworodhesha Bwana Abdallah Magadi kuwa ni miongoni mwa marehemu wa milipuko hiyo, wakati yeyé ndiye aliyepeleka mwili wa marehemu Itato Madafu ambaye kifo chake kilitokana na ajali ya gari tarehe 29/1/2011 maeneo ya Chalinze Wilaya ya Bagamoyo.


Katika milipuko hiyo ya mabomu zaidi ya watu 512 walijeruhiwa, ambapo Hospitali ya Amana iliwapokea majeruhi 256, Temeke 139, Muhimbili 87, na Zahanati ya Chanika 30.

Katika tukio hilo hadi sasa nyumba 75 zimethibitika kubomolewa, nyumba hizo zilikuwa na kaya 115 zenye watu 539.

Aidha, hadi taarifa hii inaandaliwa jumla ya watoto 140 hawajulikani mahali walipo na hivyo Serikali inatoa wito kwa wananchi pindi wawaonapo watoto ambao wanasadikiwa kupotea kufuatia tukio ya milipuko hiyo kutoa taarifa katika vituo vya Polisi, Ofisi za Serikali za Mitaa na katika vyombo vya habari ili kurahisisha utambuzi wao.

Hadi hivi sasa Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu imetoa fedha taslim shs.

500,000,000/= kwa ajili ya kulipia huduma za awali zikiwemo gharama za mazishi, rambirambi na kununua vyakula kwa ajili ya waathirika. Pamoja na fedha hizo ofisi hiyo imetoa vifaa vifuatavyo mahema (101), magodoro (538), vyombo vya kupikia makasha (80), seti ya vifaa vya usafi wa mwili (100) Blanketi za wakubwa (400) na Blanketi za watoto (200).


Wakati huo huo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam inayoratibu shughuli za maafa ya milipuko ya mabomu ya Gongo la Mboto imepokea misaada mbalimbali fedha na vifaa ikiwemo magodoro, blanketi, shuka, mito, vyandarua, nguo mchanganyiko sabuni, dawa mbalimbali, vyakula kwa ajili ya kuvigawa kwa waathirika.


Serikali kwa namna ya pekee inatoa shukrani za dhati kwa wale wote waliotoa misaada ya hali na mali kusaidia waathirika wa janga hili.


Aidha, Serikali inawahakikishia kuwa kazi ya ukusanyaji mabomu inaendelea na inawaomba wananchi kutoa taarifa pindi wayaonapo katika maeneo yao.


Imetolewa Na:
IDARA YA HABARI (MAELEZO)
24 Februari, 2011

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages