Mwili wa kijana anayedaiwa kuwa jambazi ukiwa kwenye gari la Polisi baada ya kuuawa wakati akijaribu kuiba katika duka la sonara Mjini Morogoro leo.
NA DUNSTAN SHEKIDELE, MOROGORO
JESHI la polisi mkoani hapa limefanikiwa kumuua kijana mmoja aliyedaiwa kuwa jambazi na kumkamata mwingine baada ya kuvamia duka la sonara na kuiba fedha kiasi cha shilingi laki saba pamoja na vito mbalimbali vya thamani kwa kutumia bastola.
Tukio hilo limetokea leo majira ya saa 10 jioni katika duka hilo mali ya Chuwa lililopo jirani na benki ya CRDB Tawi la Morogoro barabara ya zamani ya Dar es Salaam.
Akizungumza mara baada ya tukio hilo, kamanda wa Polisi Mkoani hapa, Adolphina Chialo alisema, “Majambazi hayo yapatayo manne yalivamia duka hilo kisha kuwaweka chini ya ulinzi wafanyakazi wa duka hilo na kisha kupora fedha pamoja na vito mbalimbali ambavyo thamani yake bado haijafahamika.”
Aliongeza kuwa, "baada ya kuporwa wafanyakazi hao walipiga kelele na ndipo askari waliokuwa lindo katika benki hiyo walipopuliza filimbi na kuanza kuwarushia risasi ambapo baadaye askari wengine waliongezeka na kuanza kuwafukuza huku wakirushiana risasi na majambazi hayo. "
Katika majibizano hayo jambazi mmoja aliuawa baada ya kupigwa risasi kichwani na mwingine walifanikiwa kumkamata akiwa na begi lililokuwa na fedha pamoja na vito hivyo ambapo kwa sasa yuko chini ya ulinzi akihojiwa na polisi huku wengine wakiendelea kutafutwa.
Baada ya jambazi huyo kuuawa wananchi waliandamana kutoka eneo alilouawa hadi katika kituo cha polisi mjini kati huku wakiwa wamembeba askari mwenye namba G2481 PC Fanuel aliyejitoa mhanga kwa kurushiana risasi na jambazi huyo hadi pale alipofanikiwa kumuua.
Wakiwa wamembeba juu juu wananchi hao, walisikika wakiimba “Fanuel apewe cheo” huku wengine wakipongeza kazi nzuri iliyofanywa na askari kwani waliweza kufika haraka katika tukio hilo na kutawanyika ambapo jambazi huyo aliuawa eneo la Mji Mpya baada ya bastola aliyokuwa nayo kuishiwa risasi.
Hakuna askari yeyote aliyejeruhiwa katika tukio hilo na kwamba uchunguzi zaidi unafanywa kubaini majina ya majambazi hayo na sehemu walikotoka.
Mwili Wa Kijana Anayedaiwa Kuwa Jambazi Ukiwa Umeharibika Vibaya Usoni Baada ya Kupigwa risasi Na Askari Wakati wa Majibishano Baina ya Polisi na Jambazi Hilo.
Kufa Kufaana Kijana Huyu Akiwa amebeba Jeneza Kwenye Mkokoteni akilipeleka Eneo la Tukio Kwaajili Ya Kubebea Mwili Wa Jambazi hilo.
Mwili Wa Jambazi Ukiwa Umebebwa Kwenye Gari la Polisi
Bastola iliyokuwa Ikitumiwa na Jambazi Morogoro Jioni hii.
Umati Wa Watu Ukiwa Umekusanyika Kuangalia Mwili Wa Jambazi Uliopigwa risasi na Polisi wakati wa Majibishano ya Risasi.
Askari Wa Jeshi La Polisi Akielezea Jinsi Alivyokua Akipambana Na Jambazi hilo jioni hii.
Wananchi Wa Moro Wakiwa Wanaangalia Maiti Ya Jambazi Uliopo Kwenye Gari Ya Polisi.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)