AZAM YAISHUSHA SIMBA KILELENI - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

AZAM YAISHUSHA SIMBA KILELENI

Na Erasto Stanslaus
AZAM FC imekwea mpaka nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom baada ya jana kuifumua JKT Ruvu mabao 2-0, katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Bao la kwanza la Azam lilipatikana katika dakika ya 42 kupitia kwa kiungo Ibrahim Mwaipopo aliyepiga shuti kali kutoka umbali wa mita 20 na kujaa wavuni moja kwa moja, huku la pili likipatikana katika dakika ya 72 baada ya beki Stanley Nkomola kujifunga alipokuwa akijaribu kuokoa hatari langoni kwake.

Kwa matokeo hayo, Azam sasa imefikisha pointi 35 sawa na Yanga lakini watoto hao wa  Jangwani wakiendelea kukaa kileleni kutokana na wastani wa mabao ya kufungwa na kufunga huku Simba ikitupwa nafasi ya tatu.

Azam waliuanza mchezo kwa kushambulia ambapo katika dakika ya 15 timu hiyo ilikosa bao la wazi kufuatia mshambuliaji John Boko kushindwa kuitumia vizuri pasi ya Mrisho Ngassa baada ya kupiga shuti hafifu lililopanguliwa na mlinda mlango wa JKT, Shaban Dihile.

Katika dakika ya 60 Azam walipata pigo baada ya Mwamuzi Oden Mbaga kumtoa nje kwa kadi nyekundu Mwaipopo, baada ya kumchezea rafu kiungo wa JKT, Nashon Naftar.

Katika michezo mingine, Toto African ilifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi AFC Arusha, pambano lililofanyika kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Huko Dodoma, Polisi Tanzania iliibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Majimaji ya Songea na kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kubaki kwenye Ligi Kuu ya Vodacom.

Kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba, Kagera Sugar na African Lyon zilitoka suluhu.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages