WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe amesema wizara hiyo inaharakisha kukamilisha kwa kanuni zitakazo simamia mitandao ya kijamii inayoendesha shughuli zake kama vyombo vya habari vya kieletroniki (Tv na Redio).
Waziri Dk. Mwakyembe aliyasema hayo jana alipokuwa akizungumza na wadau mbalimbali wa vyombo vya habari na wanataaluma wa vyombo vya habari katika maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani zilizofanyika kitaifa mkoani Mwanza.
"Hii media nyingine hii ambayo inafanya kazi zilezile kama za vyombo vya habari vya eletroniki, lakini nadhani tulikuwa hatujaamka kutunga kanuni, lakini nauhakika ndani ya muda si mrefu hilo litafanyika...lakini litakuwa zoezi shirikishi kama nilivyo ahidi...," alisema Waziri Dk. Mwakyembe.
Hata hivyo aliwataka wananchi kutumia taarifa za kwenye mitandao kwa tahadhari na kama tetesi ili kuondoa mikanganyiko ambayo imekuwa ikitokea kwenye mitandao hiyo.
Kwa upande wake Mtaalamu wa Mawasiliano, Innocent Mungy akiwasilisha mada ya 'Mchango wa Mitandao ya Kijamii katika kukuza Uhuru wa Kujieleza' kwenye kongamano hilo ilisema mitandao ya kijamii kupitia intaneti imeleta mapinduzi makubwa katika sekta ya mawasiliano licha ya uwepo wa changamoto zake.
Alisema mitandao kama blogu imekuwa ikisambaza taarifa kwa kiasi kikubwa na kutumiwa na idadi kubwa ya watu nchini katika kupata taarifa. "Bloggers wamekuwa sehemu kubwa ya mawasiliano...hadi taasisi mbalimbali zimeona umuhimu wake nazo zimeingia na kuwa zikitumia mitandao hiyo katika kutoa taarifa...," alisema mtaalamu huyo wa mawasiliano nchini.
Akifafanua alisema kutokana na wimbi la kukua kwa mitandao hiyo na kusambaza taarifa wakati mwingine imekuwa vyanzo vya taarifa hata katika vyombo rasmi vya habari. Alisema licha ya mafanikio hayo mitandao hiyo imekuwa na changamoto kubwa ikiwepo uwepo wa taarifa za uongo kupitia mitandao hiyo, matumizi mabaya ya mitandao hiyo.
Aidha akijibu moja ya swali lililoulizwa na Mwenyekiti wa Umoja wa Wamiliki wa Mitandao ya Kijamii (TBN) juu ya mvutano wa mitandao ya kijamii 'Blogu' na vyombo rasmi vya habari kuchukuliana taarifa basipo utaratibu kwa pande zote, alizitaka pande zote kukaa na kuzungumza kwa pamoja kuangalia namna zinaweza kutatua mvutano huo wa chini chini kwa maendeleo zaidi ya tasnia.
"...Nianze kwa kupongeza kuwa kwa sasa bloga wanavyofanya kazi kunamabadiliko makubwa ukilinganisha na hapo nyumba, sasa hivi hadi wao (bloggers) wanaumoja wao unaowaunganisha (TBN). Kaeni chini mzungumze naamini mtayamaliza, mnaweza kuwatumia hata waandishi wa habari wakongwe na hata bloga wazoefu ili kumaliza mgogoro huo wa chini chini na vyumba vya habari," alisema.
Hata hivyo alisema kuwa mitandao ya kijamii sio mibala bali watumiaji wake ndio wabaya na kuongeza mitandao hiyo imekuja na mabadiliko makubwa katika sekta ya mawasiliano.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)