Wananafunzi wa Shule za Msingi jijini Dar es Salaam na Tanzania kwa ujumla, wametakiwa kujenga utamaduni wa kupenda kusoma vitabu vikiwemo vya kiada na ziada, ili waweze kupanua wigo wa uelewa wa mambo mbalimbali.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Dr. Ntuyabaliwe Foundation Mama Jacqueline Mengi, alipozungumza na wanafunzi, walimu na wajumbe ya Kamati ya Shule ya Msingi Makumbusho, wakati akizindua maktaba iliyokarabatiwa na mfuko huo.
Amesema upo umuhimu mkubwa kwa wanafunzi kusoma vitabu vya kielimu, historia na pia hadithi.
Awali Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Mwl. Bernadicta Lyimo, alitoa shukrani kwa Dr. Ntuyabaliwe Foundation kwa mchango wake wa vitabu kwa ajili ya maktaba hiyo, na kuomba kupatiwa mtaalam wa kutunza maktaba, ikiwezekana mwalimu mmoja akasomeshwe taaluma hiyo.
Naye Afisa Taaluma Fatma Mwiru akimwakilisha Afisa Elimu wa Wilaya ya Kinondoni, amewataka waalimu kuwasaidia wanafunzi kupata vitabu mbalimbali, kwa kuwashirikisha wadau wa elimu, wachapishaji vitabu pamoja na wahisani.
Aidha Mama Jaqueline Mengi amesema Dr. Ntuyabaliwe Foundation ilianzishwa mwaka jana ikiwa na lengo la kuchangia katika sekta ya elimu, ambapo iligundua shule nyingi za msingi zinakabiliwa na uhaba wa maktaba na vitabu.
Shule ya Msingi Makumbusho inakuwa ya shule ya pili katika wilaya ya Kinondoni na ya kwanza katika kata ya Makumbusho, kusaidiwa ujenzi wa maktaba na msaada wa vitabu na Dr. Ntuyabaliwe Foundation, ikitanguliwa na Shule ya Msingi Hananasifu.
- Picha juu na chini ni Mkurugenzi wa Dr. Ntuyabaliwe Foundation Mama Jacqueline Mengi akizungumza na wanafunzi wa shule msingi Makumbusho kabla ya uzinduzi huo.
- Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Mwl. Bernadicta Lyimo akimwongoza Mkurugenzi wa Dr. Ntuyabaliwe Foundation Mama Jacqueline Mengi kuelekea eneo la uzinduzi wa maktaba hiyo.
- Mkurugenzi wa Dr. Ntuyabaliwe Foundation Mama Jacqueline Mengi pamoja na Afisa Taaluma Fatuma Mwiru, aliyemwakilisha Afisa Elimu wa Wilaya ya Kinondoni wakikata utepe kuashiria uzinduzi wa jengo la maktaba hiyo.
- Mkurugenzi wa Dr. Ntuyabaliwe Foundation Mama Jacqueline Mengi akisoma moja ya vitabu vya hadithi kwa baadhi ya wanafunzi wa shule ya msingi Makumbusho waliowakilisha wenzao katika uzinduzi huo.
- Mkurugenzi wa Dr. Ntuyabaliwe Foundation Mama Jacqueline Mengi na Afisa Taaluma Fatuma Mwiru, aliyemwakilisha Afisa Elimu wa Wilaya ya Kinondoni kwa pamoja wakizundua rasmi eneo la kuhifadhia vitabu ndani ya maktaba hiyo.
- Baadhi ya wageni waalikwa akiwemo Miss Tanzania 2008 Nasreen Karim (wa pili kulia).
- Baadhi ya watoto wa shule ya msingi Makumbusho wakisoma vitabu mbalimbali vilivyotolewa msaada na Dr. Ntuyabaliwe Foundation.





No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)