POLISI YAJIPANGA VIZURI KUZUIA VURUGU SIKU YA UCHAGUZI KALENGA - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

POLISI YAJIPANGA VIZURI KUZUIA VURUGU SIKU YA UCHAGUZI KALENGA

Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa Ramadhani A. Mungi akizungumza na waandishi wa habari kwenye makao Makuu ya Jeshi la Polisi mkoa wa Iringa na kuwambia namna Jeshi hilo lilivyojipanga kulinda amani na kuwasihi wananchi wote wa Kalenga kujitokeza na kwenda kupiga kura kwa Amani.
Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Polisi mkoani Iringa  Ramadhani A. Mungi akizungumza na waandishi wa habari na kuwaeleza namna walivyojipanga kulinda amani siku ya uchaguzi Kalenga na kuhakikishia wananchi wa Kalenga kuwa jeshi la Polisi limejipanga kupambana na wahalifu ,leo tarehe 14 Machi 2014.

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NDANI
JESHI LA POLISI TANZANIA
“PRESS RELEASE”
 
 Ndugu waandishi wa habari , kwa niaba ya askari Polisi wa Mkoa wa Iringa, nitumie fursa hii kuwakaribisha hapa ofisini kwetu.
 
Ndugu zangu tumeitana hapa asubuhi hii ili niweze kuwapa taarifa ya usalama katika Mkoa wetu wa Iringa hususani katika Jimbo la Kalenga katika kipindi hiki cha kampeni za uchaguzi wa Jimbo la Kalenga na usalama wa siku ya uchaguzi wenyewe.Ili iwe rahisi kueleweka taarifa hii nitaitoa kwa kifupi sana kwa kuigawa katika maeneo matatu. Eneo la kwanza ni juu ya wapi tunataka tupafikie  ( Where we want to go ), eneo la pili ni lile la wapi tulipo ( Where are we? ) na eneo la tatu ni jinsi gani tutafika huko ( How do we get there ). Tuanze na wapi   tunataka   tupafikie. Sisi  Polisi Mkoa  wa  Iringa tunataka  wananchi  wa  Kalenga  wapige kura  kwa  amani na  utulivu  mkubwa siku  ya   jumapili tarehe  16/3/2014. Hii   ndio  dira yetu  na  tutahakikisha tunafika  hapo.
 
Kuhusu  wapi tulipo  sasa, naomba   niwaelezeni kwa  ufupi  sana matukio  ya  kijinai  kuanzia  tarehe  19/02/14  mpaka  leo.  Ndugu  zangu, kuanzia   tarehe hiyo  mpaka  tarehe 2/03/2014  takribani wiki mbili  hakukuwa na tukio lolote la uvunjifu wa amani  lililokuwa limepokelewa katika vituo vyetu vya  Polisi.  Hali ilianza  kubadilika  tarehe 3/3/2014 ambapo baadhi  ya waandishi walifika ofisi kwangu na kunieleza kuwa kumetoka kwenye mkutano wa  CHADEMA  ambapo wameelezwa  na  chama hicho  kuwa   usiku wa  siku  hiyo  walimkamata  mtu  mmoja kwa  kosa  la  kujaribu  kuchoma  moto nyumba  waliokuwa  wakiishi wafuasi   wao  katika kijiji cha  WASA.
 
Waandishi  hao walinitaka  nithibitishe  kutendeka  kwa  kosa  hilo na  walieleza  kuwa wameelezwa  kuwa  bado halijaripotiwa  kituoni. Mimi  nilikataa kusema  lolote  kuhusu  hilo  kwani   lilikuwa bado  halijaripotiwa  Polisi. Tarehe 4/03/2014 nilifuatwa  tena na baadhi ya waandishi na kunieleza  kuwa siku  hiyo  waliitwa na  CCM   na kuelezwa  kuwa  siku ya  tarehe  27/2/2014 walitegewa misumari katika kijiji cha WASA ili mabasi  yaliyokuwa  yamebeba  wafuasi  wao  yaweze kutobolewa  magurudumu  yake, pia
nao  walisema tukio
 hilo halijaripotiwa Polisi.Mimi nilikataa kulizungumzia   swala hilo.
            Nduguwanahabari, vitendo  vilivyofanywa na vyama hivyo vililenga kuanzisha
propaganda  za   kisiasa
  kwa   kutumia  uhalifu kwa   kupitia  vyombo vya   habari. Sisi  Polisi tulibaini  hali hiyo na ndiyo sababu tuliamua  kuwa kimya
na  nyinyi  wenzetu
 kwa  kuzingatia  maadili ya  kazi  zenu pia   mlikaa  kimya.   
Kuanzia  hapo  vyama   vilianzisha   mashindano  ya  kuripoti  kesi  zao
Polisi. Leo  hii  vyama
 hivyo  vimeripoti  kesi ishirini  na  moja 
ambazo  zilisababisha kukamatwa kwa wafuasi (19) wa vyama hivyo viwili.
                Ndugu waandishi, kati ya kesi hizo ishirini na moja, kesi kumi na tisa (19) zile ambazo hazina madhara ya moja kwa moja kwa binadamu ama mali, kesi hizo ni  zile ndogondogo sana, kama vile kuchan mabango, kuteremsha bendera, kuchana vipeperushi, kutukanana n.k. kesi tatu zilikuwa zile zenye madhara kwa binadamu na mali ambazo ni kupigana hadharani, kujeruhi na kuharibu mali. Kati ya kesi ishirini na moja (21), kesi kumi upelelezi wake umekamilika na majalada yake yamefikishwa kwa mwanasheria wa serikali.
 
                Ndugu waandishi, katika kesi hizo Polisi tumeibaini mengi mfano CHADEMA kilikuwa kikitoa malamiko kuwa tumeacha kumkamata ndugu hassan mtenga mtuhumiwa wa kesi moja iliyokuwa imefunguliwa dhidi yake. Shutuma hizo hazina msingi kwani kesi iliyofunguliwa dhidi ya mtu huyo haikuwa ya jinai bali ya madai na tuliwajulisha hivyo. Nia ya kufanya hivyo ilikuwa kuifanya jamii iamini kuwa Polisi ni dhaifu na wenye kuonyesha upendeleo katika kushughulikia kesi za uchaguzi Nashukuru Polisi tulikuwa watulivu, hatukujibu na jamii imetuelewa sana.
 
                Ndugu waandishi, sijui mlijulishwa na nani kwamba Padri mmoja alifungwa kamba na alipingwa na kuburuzwa. Nanyi bila ya kuthibitisha kwetu mkaandika habari hiyo. Tuwaeleze kuwa mtu huyo ni miongoni mwa watuhumiwa tuliowakamata katika moja ya makosa yaliyotendeka, tulimhoji, aliandikwa maelezo yake na alipewa dhamana. Hata siku moja hajawahi kutoa taarifa Polisi juu ya matukio aliyotendewa. Nia ya kutangaza taarifa hiyo ni kuzua hofu kwa wananchi na kutaka kuchochea chuki kwa wafuasi wa dhehebu lake na wale wa dini yake.
 
                Ndugu waandishi, pamoja na matukio hayo polisi tumekuwa tukipokea taarifa za vitisho vya kuwepo kwa watu mbalimbali kutoka kwa vyama vyote walioingizwa mkoani humu kwa nia ya kutenda vitendo vya uvunjifu wa amani. Aidha, tumewasikia viongozi wa vyama
wakitamba kuingiza maelfu ya watu mkoani mwetu. Kutoka mikoa mbalimbali ikiwemo Arusha, Mbeya kwa visingizio vya kulinda kura.
                Sasa nataka niwaeleze kuwa sheria iko wazi kabisa, kila kituo cha kupigia kura kitakuwa na wakala wa chama kinachoshiriki katika uchaguzi huo na hao ndio wawakilishi wa chama hicho na walinzi halali wa uchaguzi ni askari wa Jeshi la Polisi. Kufuatia hali hiyo mambo yafuatayo yanasisistizwa sana.
 
1.   Hatutaki kuona walinzi wa chama  chochote  katika Jimbo la Kalenga. Jukumu la kulinda uchaguzi, maisha na mali ya wana Kalenga ni la JESHI LA POLISI.
 
2.   Hatutaki kuona watu wasiokuwa na shughuli maalumu wanapitapita katika maeneo ya kupigiakura.
 
3.   Siku ya uchaguzi si siku ya kampeni. Hatutaki kuona helikopita za  vyama  vyote  zenye kuashiria kufanya kampeni.

Nawaasa watu wote hasa wale waliotoka nje ya Iringa, sisi huku Iringa tunapenda sana amani kuliko kitu chochote kile hivyo ikiwa wameletwa kama MAJESHI YA KUKODIWA ili kuharibu amani ya Kalenga kama walivyozoea kufanya huko walikotoka, Sisi Polisi na wana Kalenga tupo imara, tumejipanga vizuri kukabiliana nao.
 
Aidha, napenda kuwatoa hofu wana kalenga, wasiwe na wasiwasi kabisa, sisi Polisi Iringa tupo imara na tumejipanga vizuri katika kuwalinda kikamilifu. Nawaomba wajitokeze kwa wingi sana siku ya kupiga kura na wapige kura zao kwa uhuru kabisa.
 
Ndugu waandishi, nawashukuru sana kwa jinsi mlivyofanya kazi zenu kwa ueledi mkubwa. Hata siku moja hatujawahi kusikia ama kusoma habari za uchochezi kwa kushabikia chama chochote kile.

AHSANTENI SANA.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages