Bw.
Thomas William Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano na hifadhi hati wakati
alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu idadi ya watu waliochukuliwa
alama za vidole kushoto ni Georgina Misama afisa habari wa Idara ya
Habari Maelezo. Meneja
wa Uchambuzi wa mfumo wa kompyuta NIDA Bw. Mohamed Mashaka akitoa
maelezo kwa waandishi wa habari jinsi mtambo huo unavyofanya kazi.
………………………………………………………………………………………
Mamlaka ya
Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imeanza zoezi la uchukuaji alama za
vidole, picha na saini za kielekroniki kwa waombaji wa Vitambulisho vya
Taifa katika mkoa wa Dar es Salaam ambapo watu wapatao milioni 2,900,000
wanatarajiwa kupatiwa huduma hiyo.
Zoezi hili
lilianza Julai 15 katika wilaya ya Temeke ambayo imegawanywa katika
kanda tano, itafuatiwa na Wilaya ya Ilala na kuhitimishwa na Kinondoni.
Kila Wilaya
imegawanywa katika kanda, ili kuhakikisha wananchi wanahudumiwa vizuri
na kurahisisha zoezi kwa kuwapunguzia wananchi usumbufu wa kukaa muda
mrefu kusubiri katika foleni.
Zoezi la
uchukuaji alama za vidole linakwenda sambamba na ujazaji fomu kwa
waombaji wapya ambao hawakupa fursa ya kujaza fomu wakati wa zoezi la
ujazaji fomu za maombi ya vitambulisho vya Taifa.
Waombaji
wanatakiwa kufika kwenye vituo vya usajili na nyaraka halisi za
kuthibitisha uraia na umri mathalan, cheti cha kuzaliwa, pasipoti, vyeti
vya elimu ya msingi na sekondari, leseni ya udereva, kitambulisho cha
bima ya afya na kitambulisho cha mpigakura.
Zoezi la
Utambuzi na Usajili wa watu lina hatua mbalimbali ambazo zinatakiwa
kufuatwa kwa lengo la kuweza kukusanya taarifa sahihi kwa lengo la
kutumika na mifumo mingine. Hatua hizo ni kama ifuatavyo:-
- Ujazaji wa fomu za Utambuzi na Usajili;
- Uhakiki wa awali wa fomu za maombi;
- Uingizaji wa taarifa kwenye mfumo wa kompyuta;
- Kuthibitisha taarifa za mwombaji zilizo katika mfumo wa kompyuta;
- Uchukuaji wa alama za vidole, picha na saini ya kielektroniki;
- Utengenezaji wa Daftari Kuu la Taarifa za Watu;
- Uhakiki wa mwisho;
- Uchapishaji na Ugawaji wa Vitambulisho.
Mfumo
huu una faida kubwa sana kwa taifa hili, hususan katika nyanja za
kiuchumi kijamii na kiulinzi. Baadhi ya faida hizo ni kama ifuatavyo:-
- Kumtambua Mtanzania, mgeni na mkimbizi
- Kusidia katika kuongeza wigo wa ukusanyaji kodi ya Serikali kwa njia ya kuwatambua wachangiaji wengi zaidi
- Kuondoa wafanyakazi hewa katika Mfumo wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara Serikalini
- Kusaidia suala la utambuzi hususan kwenye mabenki na hivyo kuwasaidia wananchi kupata mikopo kwa urahisi zaidi
- Kuisaidia Benki Kuu kuendesha credit reference bureau
- Kusaidia katika bodi ya mikopo ya wanafunzi kwa kuwatambua wananfunzi wote waliokopa na kuwafuatailia ili waweze kurejesha miko yao na kuufanya mfuko kuwa endelevu
- Kusaidia kuboresha Daftari la Kudumu la Wapigakura nchini
- Kusaidia kwenye mifuko ya kijamii katika kutambua wanachama wao
- Kusaidia kumtambulisha mhusika anapohitaji kupatiwa huduma katika taasisi mbalimbali kama vile benki, taasisi za mikopo na huduma za afya.
Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa inawashukuru
wanahabari kwa kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu Vitambulisho vya
Taifa, kwa juhudi za uelimishaji wa wanahabari, sasa wananchi wanafahamu
umuhimu wa Vitambulisho vya Taifa kutokana na umuhimu huo ndio maana
ukienda kwenye vituo vya usajili wanataka wapatiwe hapo hapo. Kwa kweli
mwitikio wa wananchi ni mkubwa na haya ni matunda ya wanahabari.
Umakini wa
hali ya juu unahitajika kufanya shughuli hii ili kuhakikisha kwamba
taarifa sahihi za watu zinapatikana na kutunzwa katika Mfumo kama
alivyosisitiza Mhe. Rais Kikwete katika hotuba yake siku ya Uzinduzi wa
Vitambulisho vya Taifa.
Kazi kubwa
iliyo mbele ya NIDA ni kuhakikisha kwamba kazi hii inafanywa kwa
uaminifu, uzalendo na weledi wa hali ya juu ili kuwa na taarifa sahihi
za watu na kutekeleza majukumu iliyokasimishwa kwa wakati.