TAHADHARI LA TISHIO LA MLIPUKO WA UGONJWA WA KUPOOZA (POLIO) - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

TAHADHARI LA TISHIO LA MLIPUKO WA UGONJWA WA KUPOOZA (POLIO)

\ff30Hussein-Mwinyi

TAARIFA KWA UMMA

Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imepokea taarifa mnamo tarehe 22 Mei 2013 kutoka Shirika la Afya Ulimwenguni, (WHO) ya kuwepo kwa mlipuko wa ugonjwa wa kupooza (Polio) katika Wilaya ya Fafi nchini Kenya. Mpaka sasa kuna mgonjwa mmoja bila kifo.
 
Ugonjwa wa Polio ni ugonjwa wa kuambukiza unaosababishwa na virusi vijulikanavyo kama “Polio Virus”. Ugonjwa huu unaathiri misuli na mfumo wa fahamu hivyo kusabisha kupooza kwa viungo hasa miguu na hata kifo. Ulemavu huu ukishajitokeza huwa ni wa kudumu. Waathirika wakuu wa ugonjwa huu ni watoto hasa walio na umri chini ya miaka mitano. Hata hivyo ugonjwa huu unazuilika kwa chanjo ya Polio ambayo ni salama na inatolewa bure na Serikali katika vituo vyote vya huduma ya afya. Mtoto aliyepata chanjo ya Polio anakuwa amekingwa na ugonjwa wa Polio kwa maisha yake yote.

Kutokana na taarifa hiyo ya kutoka nchini jirani ya Kenya, baadhi ya mikoa ina uwezekano mkubwa wa kupata maambukizo ya ugonjwa huo kufuatia ushauri wa kitaalam. Aidha, mikoa hii mingine inapakana na nchi jirani ya Kenya na mingine ina mapungufu yaliyopo katika hali ya chanjo ya Polio. Mikoa hii ni pamoja na Dar es Salaam, Pwani, Tanga, Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Mara na Mwanza.

Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, imechukua hatua zifuatazo katika kukabiliana na tishio la ugonjwa huu:

 ·        Kutoa taarifa ya tahadhari ya ugonjwa huu kupitia kwa Waganga Wakuu wote wa Mikoa na Wilaya.
     ·        Kuimarisha ufuatiliaji wa ugonjwa huu kupitia kwa Wataalamu wa Afya katika Mikoa, Wilaya na maeneo ya mipaka
 ·        Kufuatilia kwa karibu hali ya chanjo mikoani na wilayani hususan ya Polio hususani iliyo katika hatari ya maambukizi
 ·        Kuhamasisha watoto ambao hawajakamlisha ratiba yao ya chanjo hususani ya Polio au ambao hawajapata ya chanjo hii waweze kwenda vituo vya karibu vya afya vya kutolea chanjo
 Wizara inapenda kuchukua fursa hii kutoa wito kwa Viongozi na Watendaji wa ngazi zote kutoa ushirikiano ili kuhakikisha kila mtoto mlengwa anapata chanjo ya Polio. Aidha Wizara inatoa rai kwa wadau wetu, taasisi za dini, taasisi zinazofanya kazi katika jamii na vyombo mbalimbali  kuhamasisha watu wapeleke watoto wao kwenye vituo vya huduma wakapewe chanjo hii muhimu. Chanjo hii ni salama na inatolewa bila malipo.

 Wananchi wanashauriwa kutoa taarifa kwenye kituo cha huduma za afya kilicho karibu mara wanapoona au kupata taarifa ya mtoto yoyote anayepata ulemavu wa ghafla pasipo sababu yoyote. Mtoto huyo apelekwe katika kituo cha huduma za afya kwa uchunguzi na hatua za haraka.

 Imetolewa na;
Nsachris Mwamwaaja
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
30/05/2013

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages