Wizara
ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto inatarajia Kuzindua Mpango Kazi
wa Kitaifa wa Kuzuia Ukatili dhidi ya Watoto, utakaohusisha wadau
mbalimbali wanaosimamia ustawi wa watoto nchini mpango utakaotekelezwa
kwa kipindi cha miaka mitatu Lengo la uzinduzi wa mpango
huu ni kuandaa mazingira mazuri ya kisera, sheria, mikakati na miongozo
kuhusu upatikanaji wa haki za watoto hapa nchini ikiwemo kuzuia vitendo
vya ukatili dhidi yao, mpango utakaotekelezwa kati ya mwaka 2013 hadi
2016.
Uzinduzi wa mpango huu
unatarajiwa kufunguliwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Maendeleo ya Jamii, Mhe. Jenista Mhagama (Mb), utakaofanyika katika
ukumbi wa Hoteli ya Dodoma, mkoani Dodoma siku ya Ijumaa ya tarehe 12
Aprili 2013, saa 7:00 mchana.
Uzinduzi wa mpango huo utakwenda
sanjari na semina ya siku mbili itakayowashirikisha adau mbalimbali wa
idara za ustawi wa watoto nchini ikiwamo Wizara ya Maendeleo ya Jamii,
Jinsia na Watoto; Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii; Wizara ya Elimu na
Mafunzo ya Ufundi; Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi; Ofisi ya Waziri
Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, TACAIDS, UNICEF, asisi
zisizo za kiserikali na za dini.
Mpango kazi huu umeandaliwa
mahususi kufuatia kuwapo kwa matukio megi ya kikatili yanayowakuta
watoto ikiwamo vitendo vya kutupa na kutelekeza watoto, kubakwa na
kulawiti, kukata viungo vya watoto wenye ulemavu wa ngozi, watoto kuchwa
moto sehemu za miili yao, vitendo vinavyoashiria mmomonyoko wa maadili
katika jamii.
Utafiti wa kina wa hali ya
ukatili wa watoto hapa nchini wa mwaka 2009-2011 umebainisha kukithiri
kwa matukio ya ukatili dhidi ya watoto ambapo watoto wa kike 3 kati ya
10 na mvulana 1 kati ya 7 wamefanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Ongezeko hili kubwa la
unyanyasaji wa watoto kwa siku za hivi karibuni lilipelekea Serikali
kuandaa Sera ya Maendeleo ya Mtoto ya mwaka 2008 na kutunga Sheria ya
Mtoto Na. 21 ya 2009 kwa lengo la kuendeleza, kuboresha, kuhifadhi na
kulinda haki za mtoto.
Wizara inatoa wito kwa wananchi
na watendaji wote hasa katika ngazi za mkoa, wilaya, kata na vijijini na
mtaa kutoa ushirikiano wa kutosha katika kuutekeleza mpango kazi huu
ili kuhakikisha kuwa watoto wanalelewa na kuishi kwa amani, upendo na
usalama.
E. T. Ching’oro
Kny: KATIBU MKUU
10/04/2013
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)