………………………………………………………………..
Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa
Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) imekamilisha mchakato na kuridhia viwango
vipya vya nauli kwa ajili ya usafiri wa mijini na usafiri wa kwenda
mikoani. Viwango hivi vipya vimefikiwa baada ya kufuata taratibu za
kisheria na za kiutendaji ambazo SUMATRA kama msimamizi na mdhibiti wa
sekta ya usafiri wa barabara inapaswa kuzifuata kabla ya kuridhia
viwango hivyo. Viwango vipya vya nauli vitaanza kutumika kuanzia tarehe
12 Aprili, 2013.
SUMATRA ina wajibu kisheria
kuhakikisha pamoja na mambo mengine kuwa maslahi ya watumiaji na watoa
huduma za usafiri yanalindwa ili kuwepo na huduma endelevu ya usafiri
ulio bora, salama na wenye kukidhi mahitaji. Aidha SUMATRA ina jukumu
la kujenga na kulinda mazingira mazuri na ya kuvutia kwa watoa huduma
ili huduma ya usafiri inayotolewa inakuwa katika kiwango na gharama
zinazoendana na huduma zenyewe.
Katika kipindi cha mwaka wa fedha
wa 2011/2012, SUMATRA ilipokea maombi rasmi kutoka kwa wamiliki wa
vyombo vya usafiri wa barabara yakiwemo makampuni ya usafirishaji abiria
ya Cordial Transport Services P.L.C, Happy Nation Co. Ltd, ABC Trans na
Mwesigwa Mtazaha Kazaula yakipendekeza mapitio ya viwango vya nauli za
mabasi yanayotoa huduma za usafiri mijini (Daladala) na mabasi yanayotoa
huduma katika Mikoa kufuatia ongezeko la gharama za uendeshaji kwa
mujibu wa mawasilisho yao.
Wakati maombi ya wamiliki wa
Daladala yalilenga katika kuongeza viwango vya nauli kwa 149% ya viwango
vya sasa, wamiliki wa mabasi ya masafa marefu waliomba nyongeza kati ya
35% na 48.5%.
Kwa mujibu wa Kifungu Na 18 cha
Sheria ya SUMATRA, 2001, SUMATRA iliwashirikisha wadau mbalimbali katika
kujadili na kupata maoni yao kuhusu maombi ya wamiliki ya kuongeza
viwango vya nauli kabla ya kufanya maamuzi ya mwisho.
Aidha Mamlaka iliridhia viwango
vipya kwa mujibu wa kifungu cha 16 Cha Sheria ya SUMATRA ambacho
kinaipa Mamlaka kufanya mapitio ya nauli mara kwa mara kwa kuzingatia
gharama za kutoa huduma, maslahi ya watoa huduma, faida, maslahi ya
watumia huduma ya kulipa nauli yenye uwiano na gharama za huduma
inayotolewa.
Kwa kuzingatia hoja za waombaji,
maoni ya wadau, uchambuzi wa menejimenti, haja ya kupunguza gharama
zisizo za lazima za uendeshaji na udhibiti wa vitendo vya uvunjaji wa
Sheria na taratibu za uendeshaji shughuli za usafirishaji, Mamlaka ya
SUMATRA iliamua kuongeza viwango vya juu vya nauli za Daladala kwa
wastani wa 24.46%.
Aidha kwa mabasi ya masafa
marefu, viwango vimeongezwa kwa 20.3% kwa mabasi ya kawaida, 16.9% kwa
mabasi ya daraja la kati na 13.2% kwa mabasi ya daraja la juu.
Mchanganuo wa viwango vipya vya nauli ni kama ifuatavyo:
- Nauli za Daladala – Jiji la Dar es Salaam
| Umbali wa Njia | Kiwango Kipya cha Nauli | Mfano wa Njia |
| Kilomita kati ya 0 – 10 (Na mipaka ya Jiji Kati) | Sh 400/= | Ubungo – Kivukoni |
| Kilomita kati ya 11 – 15 | Sh 450/= | Mwenge – Temeke |
| Kilomita kati ya 16 – 20 | Sh 500/= | Tabata Chang’ombe – Kivukoni |
| Kilomita kati ya 21 – 25 | Sh 600/= | Pugu Kajiungeni – Kariakoo |
| Kilomita kati ya 26 – 30 | Sh 750/= | Kibamba – Kariakoo |
Mamlaka imeandaa majedwali kwa njia zote za Dar es Salaam. Majedwali hayo yanaweza kupatika katika tovuti yetu www.sumatra.or.tz.
Nauli ya Mwanafunzi itakuwa Sh
200/= ambayo ni nusu ya nauli ya mtu mzima ya kiwango cha chini cha
nauli ya Sh 400/=. Nauli hii itatumika kwa njia zote za Jiji la Dar es
Salaam.
- Nauli za Mabasi ya Masafa Marefu
| Daraja la Basi | Nauli ya zamani kwa km-abiria | Nauli mpya kwa km-abiria | Mfano wa kiwango kipya cha nauli kwa baadhi ya njia | |
| Basi la Kawaida kwa njia ya lami | Sh 30.67 | Sh 36.89 | DSM–Mbeya Km 833 | Sh 30,700 |
| Basi la Kawaida kwa njia ya vumbi | Sh 37.72 | Sh 46.11 | S/wanga-KigomaKm 551 | Sh 25,400 |
| Basi la hadhi ya kati (Semi Luxury | Sh 45.53 | Sh 53.22 | DSM–Mwanza Km 1,154 | Sh 61,400 |
| Basi la hadhi ya juu (Luxury) | Sh 51.64 | Sh 58.47 | DSM–Arusha Km 616 | Sh 36,000 |
Ili kuhakikisha kuwa kuna uwiano
kati ya viwango vipya vya nauli na ubora wa huduma ya usafiri, Mamlaka
imetoa maagizo kwa wamiliki wa mabasi ya masafa marefu kuboresha maeneo
yanayohusiana na huduma ya usafiri kama ifuatavyo:
- Wamiliki wa mabasi kutokutumia wapiga debe katika kuuza tiketi za safari
- Wamiliki wa mabasi kuhakikisha wanafuata Kanuni za SUMATRA za Udhibiti wa Tozo na Nauli (SUMATRA Tarrif Regulations) ambazo zinahimiiza kuwepo kwa kumbukumbu sahihi za mahesabu ili kurahisisha mapitio ya viwango vya nauli
- Kufuata Sheria, Kanuni na Masharti ya Leseni ya usafirishaji abiria
- Kutoza nauli kwa mujibu wa daraja la basi lenye sifa kamili la daraja husika kama ilivyoainishwa katika Kanuni za Usalama na Ubora
Aidha kwa mabasi ya mjini, Mamlaka imetoa maelekezo yafuatayo:
- Kuhakiksha kuwa abiria wote wanapatiwa tiketi
- Kudhibiti vitendo vya ukiukwaji wa Sheria ikiwemo kutokamilisha safari maarufa kama kukata ruti, kubadili njia na unyanyasaji wa aina yoteyote kwa abiria
- Kutokutumia wapiga debe
- Wafanyakazi wa mabasi kuvaa sare nadhifu wakati wote.
Mamlaka ya SUMATRA inaendelea
kuimarisha ushirikiano kwa kufanya kazi kwa karibu na Mamlaka zingine
kama Wakuu wa Mikoa, Serikali za Mitaa, Mamlaka za Miji, Polisi, TBS,
TANROADS, Kamisheni ya Bima na wananchi kwa ujumla, katika kuleta
mageuzi kamili ya utoaji wa huduma za usafiri wa barabara kwa kiwango
cha juu.
A.S.K. Kilima
KAIMU MKURUGENZI MKUU
2 Aprili, 2013





No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)