Ndugu zangu,
Leo
ni mwisho wa mwezi wa mwaka mpya. Na mwaka ulivyo ni kama noti ya
shilingi elfu kumi ya Bongo. Ukiichenji tu, utashangaa inavyopukutika!
Ukae
sasa ukijua, kuwa kesho ndio Februari Mosi. Hivyo, mwaka mpya wa 2013,
kama ilivyo kwa noti elfu kumi, ndio tutakuwa tumeuchenji. Subiri sasa
uone siku, wiki na miezi inavyopukitika. Fumba na kufumbua utasikia
tumeshaingia Juni tinaelekea Bajeti ya Serikali ya Julai, na ukitoka
hapo utafikiri mwaka unateremsha milima ya Kitonga.
Inatukumbusha nini?
Umuhimu wa kupanga mambo yetu. Inahusu muda na matumizi ya muda. Na mwanadamu usipokuwa makini na muda, itakuwa sawa na kisa kile cha mzazi aliyeulizwa na wanawe; " Mbona nguo za Krismasi hatujanunuliwa?"
Mzazi akawajibu wanawe; " Jamani, Krismasi ya mwaka huu imekuja ghafla sana!"
Kana kwamba hakujua, kuwa kwenye kalenda ya mwaka tarehe ya Krismasi imeshawekwa, Desemba 25!
Ndio, Afrika mvua hainyeshi ghafla, huwa kuna dalili zake. Na katika maisha, mambo mengi hayaji ghafla, bali hutuka tukiwa hatujajiandaa. Jiandae na mwaka unaoanza kupukutika kuanzia kesho, kama noti ya shilingi elfu kumi. Kila la kheri.
Maggid Mjengwa,
Iringa.
0788 111 765
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)