Picha mbalimbali zilizopigwa kutoka ofisi za walimu (staff
room) zikionesha meza ya kuchezea table tennis ikiwa ndani ya ofisi hiyo
ya shule ya sekondari Bungu Korogwe Vijijini.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Bungu, Dismas Kimweli (kushoto)
akifanya mahojiano na Mhariri wa Thehabari.com, Joachim Mushi
alipotembelea baadhi ya Shule za msingi na sekondari Halmashauri ya
Korogwe juzi
---
WANAFUNZI wa Shule ya
Sekondari Bungu iliyopo Korogwe Vijijini wamelalamikia kitendo cha
baadhi ya walimu wao kucheza mchezo wa table tennis ofisini (staff room)
tendo ambalo limekuwa likifanyika hata wakati wa kazi/vipindi vya
masomo. Malalamiko hayo yametolewa juzi ambapo mwandishi wa
Thehabari.com alitembelea shule hiyo kuangalia changamoto mbalimbali za
elimu eneo la Korogwe Vijijini.
Wakizungumza kwa masharti ya kutotajwa majina yao kiusalama na
mwandishi wa habari hizi baadhi ya wanafunzi hao walisema wapo walimu
ambao wamekuwa wakicheza mchezo huo hata wanapokuwa na vipindi jambo
ambalo huwakatisha tamaa wanafunzi. "Wapo baadhi ya walimu wamekuwa
wakijisahau na kucheza table tennis hata kama ni muda wa vipindi...na
endapo akiwaanacheza na kiongozi wa darasa asimfuate kumkumbusha kipindi
anaweza asije kabisa," alisema mmoja wa wanafunzi hao.
Mwandishi wa habari hizi alifika shuleni hapo na kuingia hadi ofisi
ya walimu (staff room) na kushuhudia meza ya table tennis ikiwa
imefungwa katikati ya ofisi hiyo tena ikipewa nafasi kubwa zaidi ya
vifaa vingine vya kikazi vya walimu katika ofisi hiyo.
Hata hivyo mwandishi wa habari hizi alipozungumza na Mkuu wa Shule
ya Sekondari Bungu,Dismas Kimweli kutaka kujua sababu ya shule hiyo
kuweka uwanja wa table tennis ofisini hapo mwalimu huyo alisema
wameufunga kwa muda kutokana na kukosa eneo la kuuweka, lakini wanafanya
jitihada za kuutoa uwanja huo.
"Ni kweli eneo hili kufungwa uwanja kama huo si sahihi...hili
nalielewa lakini tuliufunga kwa muda tu na hivi sasa tunajiandaa
kuuamisha," alisema Kimweli. Akifafanua zaidi alisema kutofundishwa kwa
baadhi ya vipindi kwa wanafunzi hakutokani na michezo ya table tennis
shuleni bali uchache wa idadi ya walimu shuleni hapo. Alisema kutokana
na uchache huo wa walimu baadhi ya mwalimu huwa na vipindi karibia 70
kwa wiki jambo ambalo huwazidi baadhi yao hivyo kujikuta wakitupiwa
lawama.
Shule ya Sekondari Bungu iliyoanzishwa mwaka 1989 yenye jumla ya
wanafunzi 640 ina walimu 12 tu huku kati ya idadi hiyo walimu watatu kwa
wako masomoni.
*Imeandaliwa na Kuletwa hapa na Thehabari.com (www.thehabari.com) kwa kushirikiana na HakiElimu
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)