Kwa
dhati ya moyo wangu nimesikitishwa sana na taarifa zilizozagaa kwenye
vyombo vya habari kuhusu kujiuza kwa dada zetu wa UDOM. Wasomi ambao
wana Dodoma na watanzania kwa ujumla walitegemea kujifunza kutoka kwao.
Taarifa hizi zimenichochea kukaa chini na kuandika waraka huu huku
nikizingatia ukweli kwamba UDOM ndipo nilikosomea masomo yangu ya
shahada ya kwanza; mbali na matatizo yote yaliyonikumba katika safari
hiyo ya kukamilisha shahada hiyo lakini nalazimika kusema kitu kwa faida
yetu wote.
Ikumbukwa moja ya mategemeo ya jamii ya wana Dodoma kutoka kwenye
chuo cha UDOM kilipo anzishwa mwaka 2007 ilikuwa ni kujionea jamii
staarabu iliyoelimika na yenye kila sifa ya kuigwa, na pia jamii ya
Dodoma ilitegemea watoto wao wangejionea namna wasomi hawa wanavyoishi
kwa kusadifu kwa vitendo elimu, maadili na mila za nchi yao. Zaidi
waliamini mambo hayo yangekuwa chachu ya kuwachochea vijana wao
kuzingatia masomo ili na wao siku moja wafikie elimu hiyo ya Chuo lakini
hali imekuwa tofauti kabisa. Leo jamii hii ya wana Dodoma wanashuhudia
wasomi wanaoshinda mitaani wakiranda randa na nguo za kuogelea na za
kulalia kana kwamba walikotoka hakuna wazazi, wanashuhudia wasomi
wanaojiuza kama njugu.
Ila kwa hali nyingine naweza sema kuna
kitu kilichofichika ndani kwani huwezi kuniambia mwanchuo ana akili
timamu akauze mwili wake kwa shilingi mia tano (500) za kitanzania
ukilinganisha na nauli ya kutoka chuo na kurudi tu ni shilingi mia sita
(600). Hapa nabaki na dukuduku kwani kuna watu wachache wanataka
kukichafua Chuo Kikuu cha Dodoma kwa maslahi yao binafsi. Hao wanabidi
wakemewe. huwezi kuniambia picha ndo kigezo tosha cha kusema huyu ni
mwanachuo wa UDOM kwani hajapatikana na kitambulisha na huwezi kuhukumu
wakati huna kithibitisho na ukilinganisha Dodoma kuna vyuo takribani
saba (7) kama vile St. John, CBE Dodoma, Chuo cha Madini, Chuo cha
Mipango n.k kwanini kila kitu waseme UDOM hapa mimi naweza sema kuna
kitu kilichofichika.
Kiukweli siwezi hata siku moja kuruhusu kulea au kuipamba tabia hizo
hata kama kuna sababu za msingi ambazo zinaweza zikawa zimesababisha
tatizo hili kutokea. Kinachofanywa na dada zetu hawa ni kitendo ambacho
kila mungwana anapaswa kukikemea kwa nguvu, na zaidi ya yote ni wajibu
wetu wote kama vijana kurudia maadili yetu kama watanzania na kulaani
kwa nguvu haya. Kama tutaruhusu tabia hii ikaota mizizi tutaandaa wasomi
wasio waadilifu na wasio jiamini, tutandaa wasomi wenye shahada za
kwenye chupi (nisamehewe kwa hiyo lugha lakini nimekosa neno linalokidhi
ninachomaanisha), tutaandaa wasomi walioathirika hivyo kupoteza nguvu
kazi ya taifa, tutaandaa taifa la wavivu na wasifikiri kwa ufanisi.
Tukumbuke kuruhusu tabia hii kubobea ni kuruhusu kuporomoka kwa elimu
ambayo ni msingi wa taifa lolote duniani. Na sidhani kama ni busara
kuangalia umauti wa taifa letu kwa kuruhusu tabia hii kuota mizizi,
kwani dhambi hiyo haitaishia chuoni tu, itaingia makazini na hapatakuwa
na kazi zaidi ya uzinzi tu, baada ya hapo dhambi hii itasambaaa hadi
kwa watoto na wajukuu wetu na hatimaye itakuwa ndio mfumo wetu wa
maisha. Lakini mbali na yote niliyoeleza hapo juu ninayo yangu kwa
serikali yangu, vijana hawa wa UDOM ni watoto wenu na wengine wameingia
pale wakiwa hawana hata elimu ya kimaisha au ya kujitegemea, wengine
wanakutana na kila aina ya tabia pale.
Mimi nilisha kuwa kiongozi wa mikopo UDOM-HSS kwa karibu miaka yote
ya masomo yangu ya shahada ya kwanza, naelewa kiasi sababu na wakati
dada zetu hawa wanapojiuza. Kipindi ambacho dada zetu hawa hujiuza huwa
ni pale Bodi ya mikopo inapochelewesha mikopo ya wanafunzi, hali huwa
mbaya kiasi dada zetu hawa ufika mahali wanalazimika kujidhalilisha
ilimradi wapate chochote cha kujikimu. Na ukizingatia majumbani kwao
hawana msaada wowote wanaoupata.
Mfano mzuri wa ucheleweshaji wa mikopo kwa wanafunzi wa kozi ya
Uhusiano wa Kimataifa (BA IR) hawajapewa mikopo yao mpaka leo, na
wanatakiwa kula, kunywa, kuwasiliana na kununua vitini vya masomo ili
hali familia walizotoka ni masikini wa kutupwa. Haya yote ni mazingira
hatarishi kwa dada zetu hawa. Serikali kama mzazi nakuomba mliangalie
kwa umakini sana suala hili ili tuwaepushie wale wanajihusisha na tabia
hii ya kuuza miili yao kutokana na kuishiwa au kukosa fedha za kujikimu
Muda mwingine unaweza kusema serikali inafanya makusudi kuwacheleweshea
mikopo yao wa sababu wanaonufaika sana na tabia hiyo ya dada zetu
kujiuza ni wabunge wanapokuja kwenye vikao vyao vya bunge.
Kujiuza kwa dada zetu hawa ni dhahiri ni matokeo ya mambo kadhaa
ambayo serikali haina budi kuyafuatilia kwa kina na hatimaye kutatua kwa
ustawi wa tafa letu la Tanzania. Hatupaswi kufurahia tabia hii hata
kidogo kwan kufanya hivyo kunaweza liathiri taifa letu kwa ujumla wake
siku za usoni.
“Ukiona panafuka moshi ujue kuna moto”
IMEANDALIWA NA
ALEX NICHOLAUS THOMAS MUSHI
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)