Misri yaahidi kusaidia kutangaza utalii wa Tanzania - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

Misri yaahidi kusaidia kutangaza utalii wa Tanzania


Marwa Tawfik (Kulia) mmoja wa wajumbe waliowakilisha vyombo vya habari nchini Misri kuja Tanzania kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii akifafanua jambo kwa wajumbe wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) na waandishi wa habari (hawapo pichani) juu ya kile walichojionea walipofanya ziara katika vivutio mbalimbali vya utalii Tanzania Bara na Zanzibar.Wengine ni baadhi ya wawakilishi kutoka Misri.
VYOMBO vya habari nchini Misri vimeahidi kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo nchini katika kuhakikisha Tanzania inapata watalii wengi zaidi jambo litakaloendelea kudumisha mahusiano mema yaliyopo kati ya nchi hizo.
Hayo yalisema Dar es Salaam juzi na mmoja wa wawakilishi wa vyombo vya habari nchini Misri, Marwa Tawfik alipozungumzia ziara waliyofanya katika vivutio vya utalii nchini ambapo waliahidi kutumia vyombo vyao kutangaza walivyoviona.
Ujumbe wa watu sita uliowakilisha vyombo mbalimbali vya habari nchini Misri yakiwemo magazeti na televisheni chini ya Ofisa wa Ubalozi wa Tanzania nchini humo Jestas Nyamanga walifanya ziara ya siku tano nchini kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii Tanzania Bara na Visiwani chini ya uratibu wa Bodi ya Utalii nchini (TTB).

Alisema wanaporudi nchini kwao watakaa na uongozi wa vyombo vyao na kuangalia jinsi ya kupata vipindi maalumu  katika televisheni na makala katika magazeti jambo litakalowezesha taarifa za utalii za Tanzania kuwafikia watu wengi zaidi nchini mwao na nchi nyingine za ukanda huo.
Tawfik alisema ana imani ziara hiyo pamoja na kazi watakayoifanya ya kuvitangaza vivutio husika itasaidia Tanzania kupata watalii wengi zaidi kutoka nchini mwao na katika nchi za ukanda wa kiarabu.
“Tumeona utajiri wa asili wa ajabu uliopo Tanzania,sisi tunaahidi kutumia vyombo vyetu kutangaza vivutio hivi katika kuhakikisha watu wengi zaidi wanahamasika kuja Tanzania na hatimaye kuwaongezea pato lenu kupitia utalii,” alisema Tawfik.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TTB Aloyce Nzuki alisema ziara hiyo pamoja na nyingine ni muendelezo wa jitihada za bodi hiyo ya kuhakikisha sekta ya utalii inakua ndani na nje ya nchi.
Alisema ujio wa ujumbe huo kutoka Misri utaongeza idadi ya watalii kutoka nchi hiyo pamoja na nyingize za ukanda huo ambapo takwimu za sasa zinaonyesha Tanzania inapata watalii 25,000 kutoka nchi za ukanda huo.

Nzuki alisema pamoja na ujumbe huo kuahidi kutumia vyombo vyao kutangaza walivyoviona pia bodi hiyo inaendelea na jitihada za kuhakikisha matangazo ya vivutio vilivyopo nchini yanawekwa katika lugha ya Kiswahili katika kukuza utalii wa ndani.
“Tumekuwa na jitihada endelevu za kuhakikisha vivutio tulivyonavyo vinajulikana ulimwenguni kote jambo litakalosaidia kupata watalii wengi zaidi kutoka nje lakini pia tunaendelea na jitihada za kuhakikisha utalii wa ndani unakua,” alisema Nzuki.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages