Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amesema Zanzibar inahitaji kujipanga ili kulinda mafanikio yaliyopatikana kutokana na mradi wa kutokomeza malaria Zanzibar. - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amesema Zanzibar inahitaji kujipanga ili kulinda mafanikio yaliyopatikana kutokana na mradi wa kutokomeza malaria Zanzibar.

    Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akisalimiana na Waziri wa Afya Juma Duni Haji mara baada ya kuwasili katika bohari kuu ya madawa Maruhubi kuanza ziara yake ya kutembelea taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo
   Mfamasia Mkuu Dr. Habib Ali Sharif akitoa maelezo kuhusiana na hali ya upatikanaji wa dawa Zanzibar, wakati wa ziara ya Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad kwenye bohari hiyo. Katikati ni Mkurugenzi wa bohari hiyo Mayasa Salum Ali.
  Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akitembelea bohari kuu ya madawa Zanzibar huko Maruhubi wakati wa ziara yake katika taasisi za Wizara ya Afya.
  Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza na watendaji wa kitengo cha malaria Mwanakwerekwe wakati wa ziara yake katika kitengo hicho. Kushoto ni msaidizi meneja wa kitengo cha Malaria Zanzibar Bw. Mwinyi Msellem.Picha Salmin Said-Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais 
---
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amesema Zanzibar inahitaji kujipanga ili kulinda mafanikio yaliyopatikana kutokana na mradi wa kutokomeza malaria Zanzibar.
 
Amesema mafanikio yalipatikana yameiletea sifa kubwa Zanzibar, hali inayopelekea kuigwa na nchi nyengine duniani.
 
Maalim Seif ameeleza hayo katika kitengo cha kudhibiti malaria Zanzibar huko Mwanakwerekwe, akiwa katika siku ya kwanza ya ziara yake ya kutembelea taasisi zilizo chini ya Wizara ya Afya kwa upande wa Unguja.

Amesema mafanikio hayo yanapaswa kulindwa na kuhakikisha kuwa malengo yaliyotarajiwa ya kuifanya Zanzibar bila ya kuwa na Malaria yanafikiwa kwa wakati.
 
“Nataka hapa tulipofika tusirudi nyuma, serikali kwa upande wake itajitahidi kuweka mikakati ili kuona kuona kuwa tunasonga mbele hadi kutimiza malengo yetu”, alisistiza Maalim Seif.
 
Kwa upande wake msaidizi meneja wa kitengo cha Malaria Zanzibar Bw. Mwinyi Msellem amesema Zanzibar imepata mafanikio makubwa ya kupambana na malaria katika kipindi cha miaka kumi iliyopita ambapo kwa sasa ugonjwa huo upo chini ya asilimia moja kutoka asilimia 45 mwaka 2001.
 
Amesema mafanikio hayo yamepatikana kutokana na mchango mkubwa wa washirika wa maendeleo, pamoja na mipango imara ya taasisi hiyo ikiwemo ugawaji wa vyandarua vyenye dawa, utiaji wa dawa za kuulia mbu wa malaria majumbani pamoja kufuatilia kwa karibu wagonjwa wanaougua malaria ili kuwapatia matibabu yanayostahiki.
 
Hata hivyo ameishauri serikali kuweka mikakati imara ikiwa ni pamoja na kutenga bajeti kwa ajili ya mradi huo ili kuweza kuundeleza wakati wafadhili watakapoamua kuondoka.
 
“Hivi sasa baadhi ya wahisani wetu tayari wameanza kupunguza misaada yao kwetu, wengi wao wakidai kuwa tayari tumepiga hatua na misaada hiyo wanaielekeza kwengine, lakini hapa ni lazima tuwe makini vyenginevyo hali inaweza kujirejea kama ilivyokuwa mwaka
2001”,alitanabahisha Msellem.
 
Akiwa katika Bohari kuu ya madawa Zanzibar huko Maruhubi, Makamu wa Kwanza wa Rais ameelezea kufarijika kwake kutokana na mfumo wa kisasa unaotumika wa uhifadhi na utoaji wa dawa, sambamba na usambazaji wake katika vituo vya afya Unguja na Pemba.
 
Amesema mfumo huo wa kutumia teknolojia ya kisasa ya kompyuta utarahisisha mawasiliano baina Wizara na vituo vya afya, pamoja na kuweza kudhibiti ubadhirifu wa dawa unaodaiwa kufanywa na baadhi ya watendaji wasio waaminifu.
 
Amewataka watendaji wa ofisi hiyo kuwa makini katika utunzaji wa mitambo iliyowekwa, na kutoa wito wa kuwepo utaratibu wa mafunzo kwa watendaji ili waweze kuitunza mitambo hiyo na kuweza kudumu kwa muda mrefu.
 
Jumla ya dola za kimarekani milioni moja nukta mbili (1.2million USD) zimetumika kwa ajili ya matengezo ya jengo hilo la bohari kuu na uwekaji wa mitambo na vitendea kazi vyengine.
 
Akizungumza katika ziara hiyo Mfamasia mkuu wa serikali Dr. Habib Ali Sharif amesema dawa zinaweza kuhifadhiwa katika bohari hiyo kwa kipindi cha miezi sita, na wamekuwa wakitumia mfumo wa kupokea maombi kutoka vituo vya afya kwa ajili ya usambazaji wa dawa.
 
Amesema mfumo huo unatumika ili kuweza kutoa dawa kulingana na mahitaji, sambamba na kudhibiti matumizi mabaya ya dawa kutoka kwa baadhi ya watendaji kwenye vituo vya afya.
 
Hata hivyo amesema bohari hiyo inakabiliwa na tatizo la usafiri ambalo huzorotesha ufuatiliaji wake katika maeneo waliyopanga kufanya hivyo.
 
Katika bodi ya chakula, dawa na vipodozi, Makamu wa Kwanza wa Rais amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa bodi hiyo ili iweze kufanya kazi zake vizuri zenye lengo la kutunza afya ya jamii.
 
“Hii bodi inafanya kazi kwa ajili ya kulinda afya zetu, ni vizuri basi kuipa mashirikiano ili kuweza kuwadhibiti wafanyabiashara wanaoweza kuhatarisha afya zetu kutokana na kuingiza na kusambaza bidhaa zisizofaa kwa matumizi ya binadamu”,alitahadharisha Maalim Seif.
 
Kwa upande wake mrajis wa bodi hiyo Dr. Burhani Othman Simai amesema baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu wamekuwa wakiingiza bidhaa zilizopitwa na wakati pamoja na kubadilisha tarehe za kumaliza muda, hali ambayo ni hatari kwa afya ya jamii.
 
Dr. Simai ametaja baadhi ya changamoto zinazoikabili bodi hiyo kuwa ni pamoja na kuwpo bandari zisizo rasmi, upungufu wa wataalamu pamoja na uelewa mdogo wa jamii juu ya kazi zinazofanywa na bodi hiyo.
 
Ziara hiyo pia imewashirikisha watendaji wakuu wa Wizara ya Afya wakiwemo Waziri wa wizara hiyo Mhe. Juma Duni Haji na Katibu Mkuu Dr. Mohammed Saleh Jidawi.
 
Na
 Hassan Hamad
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages