Waziri
wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Hussein Mwinyi akitoa ufafanuzi kwa
waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam kuhusu hatua
zilizochukuliwa na Serikali kufuatia kubainika kwa matumizi ya dawa
bandia za kupunguza makali ya Ukimwi zenye jina la Biashara TT –VIR 30.
Mmoja wa maafisa kutoka Mamlaka ya
Chakula na Dawa Nchini (TFDA) ambaye hakutaka jina lake liandikwe
kwenye vyombo vya habari akiwaonyesha waandishi wa habari Dawa badia za
kupunguza makali ya Ukimwi (ARVS) zilizoondolewa katika vituo vya
kutolea huduma mara baada ya kugundulika.
Makopo
ya dawa za kupunguza makali ya Ukimwi yakitofautiana vifungashio. Kopo
la kwanza kushoto linaonyesha dawa halisi ya kupunguza makali ya Ukimwi
iliyokidhi viwango ikifuatiwa na makopo 3 yenye dawa bandia ya
kupunguza makali ya Ukimwi yenye jina la biashara TT –VR 30 toleo namba
0c.01.85 yaliyotengenezwa na kiwanda cha Tanzania Pharmaceutical
Industries Ltd. Picha na Aron Msigwa – MAELEZO.
……………………………………………….
Na. Aron Msigwa –MAELEZO.
Serikali imewasimamisha kazi
mkurugenzi mkuu wa Bohari ya Dawa nchini (MSD) ,Mkuu wa kitengo cha
Udhibiti na Ubora na Afisa Udhibiti Ubora wa ohari hiyo ili kupisha
uchunguzi dhidi yao kufuatia kuruhusu kusambazwa kwa dawa bandia za
kupunguza makali ya UKIMWI aina ya TT –VIR 30 katika vituo mbalimbali
vya kutolea huduma za afya nchini.
Aidha imepiga marufuku usambazaji
na matumizi ya dawa aina ya TT –VIR 30 toleo na 0C .01.85
inayotengenezwa na kiwanda cha Tanzania Pharmaceutical Industries Ltd
(TPI) kufuatia dawa hiyo kutengenezwa chini ya kiwango na kutofaa kwa
matumizi ya binadamu.
Akizungumza leo jijini Dar es
salaam Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Hussein Mwinyi amesema
kuwa hatua hiyo imechukuliwa mara baada ya kubaini kuwepo kwa dawa
bandia ya kupunguza makali ya Ukimwi katika hospitali ya wilaya ya
Tarime kufuatia ukaguzi uliofanywa na Wizara ya Afya kupitia Mamlaka ya
Chakula na Dawa nchini (TFDA).
Amesema kuwa ukaguzi na uchunguzi
wa kimaabara dhidi ya dawa hiyo isiyokidhi viwango ulibainia kuwa
nyaraka zilizopo kuhusiana na dawa hizo unaonyesha kuwa Kiwanda cha
Tanzania Pharmaceutical Industries Ltd (TPI) waliiuzia Bohari ya Dawa
(MSD) dawa hiyo bandia toleo namba 0C. 01. 85 iliyotengenezwa nchini
mwezi Machi 2011 na kuonyesha mwisho wa matumizi yake mwezi Februari
2013.
Amefafanua kuwa dawa hiyo bandia
ilikua na dawa zenye rangi mbili tofauti njano na nyeupe na kuwa na
viambata tofauti vilivyopaswa kuwepo aina ya Efaverenz badala ya
Niverapine, Lamivudine na Stavudine na kuongeza kuwa vidonge
vilivyokutwa kwenye vifungashio vya dawa husika vilikua tofauti na
vifungashio vilivyosajiliwa na TFDA.
Dkt. Mwinyi amesema kuwa serikali
inahakikisha kuwa dawa zenye ubora unaotakiwa za kupunguza makali ya
UKIMWI zinaendelea kupatikana katika vituo vya kutolea huduma kote
nchini na kuwaagiza waganga wakuu wa mikoa, wilaya na kamati za dawa na
Tiba katika vituo vya huduma za afya kuhakikisha kuwa zinapokea,
kuhakiki na kusimamia kikamilifu ubora na matumizi sahihi ya dawa na
vifaa tiba nchini.
Kuhusu upatikanaji wa dawa hizo
amewatoa hofu wananchi na kuwahakikishia kuwa dawa za kutosha zenye
viwango stahili zitaendelea kupatikana katika vituo vya kutolea huduma
za afya nchini na kuwataka wananchi kutoa kushirikiana na mamlaka husika
kwa kutoa taarifa pale wanapobaini kuwepo kwa dawa zenye ubora wenye
mashaka au uvunjifu wa sheria inayosimamia ubora na usalama wa dawa.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)