Naibu Waziri wa Chakula na Ushirika, Adam Malima na Naibu Waziri wa
Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Ummy Mwalimu, jana wamezindua
shindano la Maisha Plus/Mama Shujaa wa Chakula 2012.
Uzinduzi huo umeshuhudia wanawake 14 waliongia kambini kwenye kijiji
cha Maisha Plus ambao baadaye wataungana na vijana watakaoshiriki kwenye
shindano la Maisha Plus.
Akizungumza baada ya kuwatambulisha Mama Shujaa 14 watakaoshiriki
kwenye shindano hilo kumpata mshindi mmoja, Mheshimiwa Malima alisema
serikali itahakikisha kuwa mwanamke ambaye ni mzalishaji mkuu wa chakula
kwenye jamii ya Tanzania anawekewa mazingira mazuri ambayo yatasaidia
shughuli za kilimo ziwe na tija zaidi.
Kwa upande wake Mheshimiwa Mwalimu alisema wanawake wamekuwa
wakikumbwa na changamoto nyingi kwenye jamii ambapo pamoja na kushiriki
katika uzalishaji wa chakula wamekua wakikosa mamlaka na uamuzi wa kile
wanachokitayarisha kutokana na kuendelea kuwepo kwa mfumo dume ambapo
mwanaume huwa juu ya mwanamke.
Alisema wanatambua kuwa kipato kinachopatikana kutokana na shughuli
za kilimo kinamilikiwa na wanaume ambapo pia wanawake wengi hawamiliki
ardhi.
Aliongeza kuwa serikali inazitambua changamoto hizo na inafanya kazi kuziondoa kabisa.
Mheshimiwa Mwalimu alisisitiza kuwa shindano la Mama Shujaa lengo
lake ni kuikumbusha jamii umuhimu wa mwanamke katika uzalishaji wa
chakula na kwamba sheria inasema mwanamke na mwanaume wana haki ya sawa
katika maamuzi ya kile wanachozalisha.
Naye Mkurugenzi mkazi wa shirika la OXFAM ambalo ni wadhamini wa
shindano hilo Bi. Monica Gorman alisema wanawake ni waendeshaji wa
uchumi wa Tanzania lakini umuhimu wao umefunikwa kwa muda mrefu hivyo
kwa kutumia shindano la Mama Shujaa wa Chakula, wanawake wanamulikwa ili
wapate kile wanachostahili.
Shindano hilo lina lengo la kuwainua wanawake, kuwapa moyo na
kuwaunga mkono wakulima wadogo wanawake nchini na kuongeza kukubalika
kwa mchango wao katika kilimo.
Uzinduzi wa Maisha Plus/Mama Shujaa wa Chakula 2012 ulioneshwa live kupitia kituo cha TBC1.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)