Na Innocent Mungy - Doha, Qatar
Balozi Maalumu wa Umoja wa Posta Duniani, Mh. Prof. Anna Tibaijuka, ameyahimiza Mataifa yote duniani kuhakikisha wanaboresha maisha ya watu wake kwa kuweka anwani za makazi na posti kodi zenye kukidhi mahitaji mbalimbali ya maendeleo ya raia wake.
Akiwasilisha Tamko la Doha La Umoja wa Posta Duniani la Kutoa anwani kwa watu wote, Mh. Tibaijuka ambae pia ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, amezishauri nchi wanachama wa UPU kuhakikisha kila raia anatambuliwa alipo na kuhakikishiwa usalama wake na kujumuishwa kwenye mipango ya maendeleo ya nchi yake.
Amesema, watu kukosa anwani za makazi kunawakwamisha katika shughuli za maendelo kama vile uwezo wa kutambuliwa ili kupata huduma za msingi za maisha yao kama vile shule, maji na huduma mbalimbali za jamii. Amezitaja huduma zingine kuwa ni pamoja na utambulisho wa makazi rasmi ili kuweza kupata mikopo kutoka katika mabenki yanayoshindwa kutoa mikopo kutokana na wengi wa raia kukosa utambulisho wa wanakokaa.
Aidha amesema, kutokana na watu wengi zaidi kuhamia mijini kutoka vijijini, Serikali hazina budi kujipanga kupitia program za mipango miji ili kudhibiti makazi holela ambayo hayawezi kutambuliwa rasmi kutokana na kutokuwa na miundo mbinu yeye ubora KWA maisha ya watu.
Prof. Tibaijuka pia amezihimiza nchi wanachama wa UPU kuwekeza katika kuwa na mfumo thabiti wa anwani za makazi na posti kodi ili mfumo huo uwezo kuboresha maisha ya watu hata kwa huduma za afya za dharura, usalama na urahisi wa kutoa huduma za uokoaji wa watu wakati wa dharura.
Nchi mbalimbali zimezungumza kufungua mkono Tamko hilo, ikiwemo Costarica iliyopendekeza kuwashurikisha wananchi, wafanyibiashara na taasisi mbalimbali ili kufanikisha mpango wa anwani za makazi kwa kila mwananchi duniani.
Leo jioni, Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Mh. Prof. Makame Mbarawa anatarajia kuhutubia mkutano huu kutoa taarifa ya maendeleo ya huduma za Posta Tanzania na jinsi ya kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoikumba sekta ndogo ya Posta duniani, hasa nchi kama Tanzania.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)