Katibu wa
Sekretarieti ya Ajira, Bw. Xavier Daudi akifafanua jambo kwa Waandishi
wa habari hawapo pichani na kushoto kwake ni Mwenyekiti wa Sekretarieti
ya Ajira, Bw. Bakari Mahiza.
Sekretarieti ya Ajira imetangaza ratiba ya usaili
kwa mwezi Agosti, 2012 kwa waombaji nafasi za kazi katika Taasisi za
Umma kwa wale waliokidhi vigezo. Tangazo hilo limetolewa leo na Katibu
wa Sekretarieti ya Ajira, Bw. Xavier Daudi alipokuwa akiongea na Waandishi
wa habari ofisi kwake.
Daudi amesema usaili huo utafanyika katika Mikoa
sita ambayo ni Dodoma, Morogoro, Manyara, Arusha, Dar es Salaam na mkoa
wa Pwani.
Amesema usaili umeanza tarehe 6 hadi 7 Agosti, mwaka
huu kwa mkoa wa Manyara, wilaya ya Babati kwa nafasi za Mtandaji wa
Kata, kijiji na Madereva, ilihali kwa mkoa wa Dodoma umeanza tarehe
7-9 Agosti, 2012 katika Chuo cha Serikali za Mitaa, Hombolo kwa nafasi
Wahadhiri wasaidizi, Afisa Utumishi, Afisa Tawala, Watunza kumbukumbu,
Madereva na Wasaidizi wa Ofisi.
Aidha, usaili utafanyika pia katika Chuo cha Mipango
Dodoma (IRDP) kuanzia tarehe 10-14 mwezi huu kwa kada za Afisa Ugavi,
Afisa Utumishi, Mkutubi na Afisa Mitaala. Wakati katika Shirika la Ukaguzi
na Usimamizi wa Biashara (COASCO) utaanza tarehe 15-16 Agosti kwa kada
za Wakaguzi wa hesabu wa ndani, Wakaguzi Wasaidizi wa hesabu wa ndani
na nafasi ya Katibu Mahususi.
“Kwa mkoa wa Morogoro usaili utafanyika tarehe
15-16 mwezi huu katika Taasisi ya Tanzania Official Seed Certification
Institute (TOSCI) kwa kada za Wakaguzi Wasaidizi wa hesabu wa ndani,
Afisa Kilimo, na kwa Katibu Mahususi”. Alisema Daudi.
Ameongeza kuwa kwa mkoa wa Arusha usaili utafanyika
tarehe 10-11 Agosti katika Tume ya Mionzi Tanzania (TAEC) kwa nafasi
za Wataalamu wa Mionzi, Fizikia, Uhasibu, Ukatibu Mahususi, Msaidizi
wa Ofisi na Ulinzi. Aidha, usaili utaendelea katika mkoa wa Pwani, wilaya
ya Bagamoyo katika Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TASUBA) kwa
nafasi ya Mkufunzi na Mkufunzi Msaidizi daraja la kwanza na la pili.
Katibu amesema usaili huo utamalizikia kwa mkoa wa
Dar es Salaam ambao unatarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 23 hadi 31
Agosti kwa awamu hii ambao utakuwa kwa Vyuo vya elimu ya juu ikiwemo
Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Chuo cha kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere
na Chuo cha Biashara (CBE). Aidha, utafanyika pia katika Taasisi ya
Utafiti wa Samaki Tanzania (TAFIRI) na Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) ambao
utahusisha nafasi za Wakufunzi, Afisa Utumishi, Afisa Mitaala, Afisa
Viwango, Madereva na Katibu Mahususi.
Katibu wa Sekretarieti ya Ajira amesema nia ya kufanya
usaili katika mikoa husika kwanza ni kufikisha huduma karibu na wateja
wetu na pia kuwapunguzia gharama za kusafiri mbali na eneo alilokuwa
ameomba kazi husika. Aliongeza kuwa ili kupata maelezo zaidi juu ya
usaili huo ni vyema wakatembelea tovuti ya Sekretarieti ya Ajira ambayo
ni www.ajira.go.tz ili kupata ufafanuzi zaidi.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)