Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Msingi Kitopeni kutoka Wilaya ya Korogwe
Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Msingi Kitopeni ya Mjini Korogwe
Joachim Mushi, Thehabari.com
BAADHI ya walimu wa shule za
msingi wilaya za Korogwe na Moshi wamelalamikia mabadiliko ya mara kwa
mara ya mitaala kwa shule za msingi pamoja na idadi kubwa ya masomo kwa
wanafunzi wa madarasa ya chini, kuwa yamekuwa yakiwachanganya wanafunzi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti
hivi karibuni walisema mabadiliko ya mara kwa mara kwa mitaala
yanayofanywa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi bila maandalizi
yamekuwa chanzo cha vikwazo cha kufanya vizuri kwa sekta hiyo.
Akizungumza hivi karibuni na
mwandishi wa habari hizi, Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule ya Msingi
Gerezani, mjini Moshi, Khadija Mtui alisema mabadiliko ya mitaala ya
mara kwa mara yanawachanganya wanafunzi pamoja na walimu hivyo kuwa
kikwazo.
Alishauri kuwepo na maandalizi ya
kutosha ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha walimu ambao ni wadau wakubwa
wa sekta ya elimu kabla ya mabadiliko ya mitaala hiyo. Alisema pamoja
na hali hiyo mabadiliko ya vitabu vya masomo bila utaratibu mahususi ni
tatizo pia katika mafanikio ya sekta hiyo kitaaluma.
“Mabadiliko ya mitaala na
mchanganyiko wa vitabu bila utaratibu mahususi ni tatizo, kwa sasa hivi
kila shule ina kitabu chake katika somo fulani…hata hivyo licha ya
mabadiliko ya mara kwa mara hakuna maandalizi, mimi tangu nimalize chuo
1979 sijaenda semina yoyote wala mafunzo kujiandaa na mabadiliko ya
mitaala hii. Hili linachangia pia,” alisema mwalimu Mtui.
Akifafanua zaidi Mwalimu Mkuu
Msaidizi wa Shule ya Msingi Muungano, ya wilayani Moshi, Ashati Elihaki
alisema mbali na mchanganyiko juu ya suala la vitabu vya masomo
mabadiliko ya mitaala yamegeuza baadhi ya masomo kubaki kama ‘kiini
macho’ jambo ambalo ni tatizo kwa walimu.
“…angalia kwa mfano somo kama la
Tehama linaloanza kufundishwa darasa la tatu hadi la saba somo hili lipo
kinadharia zaidi, hakuna walimu ambao wameandaliwa kufundisha somo hili
lakini linatakiwa kufundishwa eti kwa kutumia mwongozo wa mwalimu
kimsingi hii si sawa,” alisema Elihaki.
Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya
Msingi Kitopeni ya Mjini Korogwe, Theodolph Karigita alisema tofauti na
ilivyokuwa hapo awali mitaala ya sasa imevurugwa kiasi kikubwa jambo
ambalo linawachanganya walimu na hata wanafunzi hivyo kushindwa kufanya
vizuri.
“…Mitaala imevurugwa sana,
kunamchanganyiko wa masomo nadhani unakumbuka kuna kipindi baadhi ya
masomo yaliunganishwa kama Jiografia, Historia na Uraia wakaita maarifa
ya jamii…kipindi hiki wanafunzi walifanya vibaya sana hivyo
ikabadilishwa sasa watoto wanafanya vizuri tofauti na awali,” alisema
Karigita.
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa
Shule ya Msingi Lwengera Darajani, Youze Mbwambo alisema idadi kubwa ya
masomo kwa wanafunzi wa darasa la kwanza hadi la tatu ni chanzo kingine
cha wanafunzi hao kufanya vibaya kwani wamekuwa wakibebeshwa mzigo
pasipo sababu za msingi.
Akizungumzia hoja hizo
zilizotolewa na baadhi ya walimu, Ofisa Elimu Taaluma, Halmashauri ya
Mji wa Korogwe, Elius Mkwizu alisema mabadiliko yanayofanywa na
wataalamu hufanywa kwa malengo mazuri licha ya kuwepo na changamoto
kadhaa maeneo tofauti.
*Habari hii imeandaliwa na Mtandao wa Thehabari.com (www.thehabari.com) kwa kushirikiana na Taasisi ya HakiElimu.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)