Vijana wa Korea walioshiriki kambi ya kimataifa ya vijana wakitumbuiza wakati wa ufungaji wa kambi hiyo jana Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Waziri wa
Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dkt. Fenella Mukangara akipokea
tuzo kutoka kwa Katibu Mkuu wa International Youth Fellowship Bw. Lee
Hunmok jana wakati wa ufungaji wa kambi ya kimataifa ya vijana Jijini
Dar es Salaam. Tuzo hiyo ilitolewa kwa Wizara kama ishara ya kutambua
mchango wake katika kuhakikisha kuwa maendeleo ya vijana yanastawi
kikamilifu.
Na Concilia Niyibitanga
WHVUM
Tarehe 8/8/2012
Maendeleo
ya vijana ndiyo msingi wa maendeleo ya taifa letu, na ni muhimu vijana
wakatambua hilo kwa kutimiza wajibu wao kwa jamii inayowazunguka.
Hayo yalisemwa jana na Waziri wa Habari,
Vijana, Utamaduni na Michezo, Dkt. Fenella Mukangara wakati akifunga
kambi ya kimataifa ya vijana Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
iliyokaa kwa muda wa siku saba kwa lengo la kuzungumzia mstakabari wa
maendeleo ya vijana hususan kuwajengea vijana fikra chanya kwa ajili
ya kujiletea maendeleo.
Mukangara
alisema kuwa vijana wanatakiwa kuwa na moyo wa kujituma, kujitolea na
kufanya kazi kwa bidii ili kukabiliana na changamoto zinazowakabili
katika maisha yao ya ujana.
‘Fanyeni
kazi kwa bidii, kwa kujitolea, kwa kuzingatia muda na kujitegemea ili
kutimiza ndoto zenu za kujiletea maendeleo ya kiuchumi na kiafya’. Alisema Dkt. Mukangara
Aidha,
amewaasa vijana kuachana na fikra za kulalamika, kudai haki bila wajibu
na kunyosheana vidole na badala yake kijana mwenyewe ajiulize amefanya
nini kutatua kero inayomzunguka.
Vijana kataeni vitendo vya uchochezi,
chuki na kejeri kwa viongozi kwani kufanya hivyo kunaweza kuwaingiza
katika misuguano isiyo na tija na mkumbuke kuwa maendeleo
ya vijana hayawezi kushamiri na kustawi pasipo na amani, lindeni amani
kwa nguvu zenu zote na kusimamia sheria wakati wote’ Alisema Dkt.
Mukangara.
Alisema
kuwa Serikali inatambua umuhimu wa vijana na kupitia Wizara yake
imeweka mipango ambayo inatoa vipaumbele kwa maendeleo ya vijana.
Naye Katibu Mkuu wa International Youth
Fellowship (IYF), Bw.Lee Hunmok aliwataka vijana kuwatumikia wenzao na
kuwa mabalozi kwa vijana ambao hawakupata fursa ya kuingia kambini.
Bw. Vitus Faustin Mzale ni
kijana aliyeshiriki kambi hiyo kutoka mkoani Kagera alisema kuwa
ameweza kujifunza mambo mbalimbali kambini hapo na amewataka waandaaji
kushirikiana na Serikali ili kuwapa vijana mafunzo ya ujasiriamali ili
waweze kujikwamua kiuchumi.
Kwa upande wake Bi Mariza Vargas kijana
kutoka Peru alisema kuwa amefungua moyo wake kwa ajili ya kujitolea na
ameweza kujua namna ya kufanikisha malengo yake ya kujiletea maendeleo
kama kijana.
Kambi hiyo ya kimataifa iliyoandaliwa na
International Youth Fellowship ilishirikisha nchi mbalimbali ikiwemo
Tanzania, Kenya, Korea, Malawi, Peru na China.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)