Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo Azindua Rasmi Kituo Cha Kufua Umeme wa Gesi Asilia wa Megawati 105 Eneo la Ubungo Jijini Dar es Salaam. - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo Azindua Rasmi Kituo Cha Kufua Umeme wa Gesi Asilia wa Megawati 105 Eneo la Ubungo Jijini Dar es Salaam.

 Kituo cha Umeme wa gesi asili wa megawati 105.
  Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, akipata maelezo kutoka kwa Meneja wa Kituo cha Umeme wa gasi asili wa megawati 105, John Mageni wakati wa hafla uya uzinduzi wa kituo hicho uliofanyika Ubungo jijini Dar es Salaam jana
 Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo,akiendelea kupata maelezo kutoka kwa Meneja wa Kituo cha Umeme wa gasi asili wa megawati 105, John Mageni
 Baadhi ya Wageni Waalikwa
Wasanii kutoka THT wakitumbuiza katika hafla ya uzinduzi wa kituo cha Umeme wa gesi asili wa megawati 105 Ubungo jijini Dar es Salaam.Picha Zote na Mdau Dande Francis
--
DAR ES SALAAM,Tanzania

SHIRIKA la Ugavi wa Umeme Tanzania (Tanesco), limefungua rasmi kituo cha kufua umeme wa gesi asilia wa megawati 105 eneo la Ubungo jijini Dar es Salaam Jana.Akizungumza katika ufunguzi huo jana, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, alisema kituo hicho ni mali ya serikali ambacho kimegharimu dola za Marekani 124,895,988 huku akiishukuru Serikali ya Norway waliodhamini upatikanaji wa mkopo huo.

Prof. Muhongo alisema  hiyo ni dalili tosha kwamba wamedhamiria kubadili mtindo wa upatikanaji wa umeme kutoka chanzo kikubwa kimoja cha umeme wa maji ambao kwa sasa unazalisha MW 561 ya umeme wote.Alisema kufuatia uzinduzi huo, mitambo yote ya gesi iliyopo Mkoa wa Dar es Salaam na Mtwara itazalisha umeme wa jumla ya MW 1375 huku akieleza takwimu hizi zinaonesha ni jinsi gani serikali inavyojitahidi kupunguza utegemezi wa umeme wa maji.

Alisema hadi kufikia jana Tanzania imegundua gesi asili ya jumla  ya futi za ujazo trilioni 26.99 sawa na mapipa ya mafuta bilioni 4.86 huku akiahidi kuwa utafutaji huo wa gesi unaendelea.

“Iwapo tutatumia gesi iliyohakikiwa hadi leo hii ya wingi wa futi za ujazo trilioni 1.142 kwenye mitambo yetu yote inayofua umeme wa gesi kwa kutumia futi 150 kwa siku, gesi hiyo iliyohakikiwa tutaitumia kwa muda wa miaka miwili ijayo,” alisema Muhongo.
Alisema serikali inatayarisha sera ya gesi kwa kutumia wataalamu Watanzania ambayo itajadiliwa na wadau wengi wakiwamo wenyeji wa Mtarwa  na Lindi ili kuwezesha kuwa na msingi mzuri wa maandalizi ya muswada wa gesi na kanuni zake kwa manufaa ya nchi.
Prof. Muhongo aliongeza kuwa mbali ya gesi serikali pia imeamua kutumia makaa ya mawe kuzalisha umeme na ifikapo mwaka 2015/2016 umeme utaanza kutokana na makaa hayo yenye wingi usiokuwa chini ya MW 200.

Alisema serikali pia imeamua kutumia vyanzo vingine vya kupata umeme wa uhakika kutoka kwenye upepo, jua  na jotoardhi  jitihada zote ni kuhakikisha nishati ya uhakika inapatikana  ili kutimiza malengo ya maendeleo ambapo hadi kufikia mwaka 2025 nchi iwe ni miongoni mwa zenye kipato cha kati cha dola za Marekani 3,700-12,000.

“Ili kuwepo na maendeleo, tunahitaji umeme wa uhakika, tunahitaji taifa lenye kipato cha kati kuwepo na MW 3000-5000,  tuige mfano wa Kenya ambapo kwa sasa wenzetu wamepiga hatua ikiwa umeme wa upepo wanazalisha MW 1,000,” alisema Muhongo.
Naye  Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Injinia William Mhando, alisema kuwa hawatarudi nyuma kutokana na kupata fundisho katika athari kubwa za ukosefu wa umeme iliyotokea mwaka 2010 hadi 2011.

Alisema kuhakikisha uzinduzi wa kituo hicho unafikiwa ni jitihada kubwa zilizofanyika bega kwa bega na mhandisi mshauri kutoka nchini Norway na Ujerumani.
 
Alisema kituo hicho cha Ubungo kina mitambo mitatu ambayo kila mmoja unazalisha MW 35 kila mmoja na kufanya kufikia MW 105, iliyoingizwa katika gridi ya taifa.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages