Askofu wa Kanisa Katoliki la Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhamam Kardinali Polycap Pengo,
---
UJUMBE WA BARAZA LA MAASKOFU KATOLIKI TANZANIA KWA WAAMINI WAKATOLIKI NA WATU WOTE WENYE MAPENZI MEMA
Sisi
Maaskofu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania tumekutana katika
Mkutano wetu Mkuu wa 65 wa kawaida tangu tarehe 23 – 30 Juni 2012
uliowajumuisha Wakuu wa Mashirika ya Kitawa, wakuu wa Idara, Tume na
Taasisi za Baraza pamoja na wawakilishi Walei. Lengo la
Mkutano huu lilikuwa kutathmini shughuli na kazi zetu za Kichungaji na
za huduma za jamii kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita (2009-2012) na
vile vile kupanga mikakati ya kuboresha shughuli hizo za Kichungaji na
za huduma za Jamii katika Nyanja za Afya, Elimu, Maji, misaada kwa
wasiojiweza, utetezi na ushawishi, kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo
(2012-2015).
Pamoja
na kufanya tathmini ya kina ya utendaji wa Baraza letu katika kipindi
hicho kilichopita, na kupanga mipango kabambe kwa ajili ya utendaji wa
Baraza kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo, Mkutano wetu
Mkuu umekuwa fursa ya kujadiliana na kushirikishana baadhi ya
matukio/mambo ambayo, kwa hakika, yameitikisa jamii yetu ya Watanzania
na kuidhalilisha mbele ya Jumuiya ya kimataifa.
Kwa
namna ya pekee kabisa, tumetafakari juu ya vuguru za kidini za hivi
karibuni zilizotokea katika Visiwa vya Zanzibar kuanzia 26-28 Mei, 2012
na kupelekea kuchomwa moto kwa baadhi ya Makanisa Visiwani humo pamoja
na uharibifu mkubwa wa mali na uvunjifu wa amani. Bila kupenda kurudia
matamko ya Wadau mbali mbali waliyoyatoa katika nyakati tofauti kulaani
bila kusita hali hiyo ya kutisha na kusikitisha iliyojitokeza Visiwani
humo, tunaunga mkono kwa nguvu zote kauli na jitihada za wale wote wenye
mapenzi mema walioguswa na vitendo hivyo na hivyo kuvilaani. Tunatoa
pole na kueleza mshikamano wetu wa kindugu kwa wale wote walioathirika
kwa namna moja au nyingine na vitendo hivyo vya vurugu ambavyo vimefanya
sehemu ya jamii ya wakazi wa Visiwani humo, hasa Wakristo, kuishi kwa
wasi wasi mkubwa kutokana na vitisho vinavyoendelea kutolewa na baadhi
ya vikundi pamoja na hali ya kutopewa ulinzi wa kutosha na vyombo
husika. Tunaendelea kuwaahidi Sala na mshikamano wetu katika kipindi hiki kigumu.
Pamoja
na hayo, tunapenda kuwakumbusha Watanzania wenzetu, hasa mamlaka husika
kutafakari na kuzingatia busara ya wahenga waliosema kwamba “mwanzo wa makubwa ni madogo” na kwamba “mdharau mwiba mguu huota tende”.
Kumbu kumbu zinatwambia kwamba, chuki za wazi za kidini zilianza
kuinyemelea nchi yetu miaka ya 1990, pale mihadhara ya kashfa za kidini
ilipoanza kuruhusiwa. Baraza la Maaskofu Katoliki
Tanzania, kwa kuongozwa na busara ya kichungaji, kwa nyakati tofauti,
liliandika barua kuziomba na kuzihimiza Mamlaka husika kuingilia kati na
kuhakikisha kwamba mihadhara kama hiyo haipati nafasi ya kuendelea
katika nchi yetu kwani kamwe haiwezi kuwa na tija isipokuwa kuamsha hisia
kali za kidini, jazba na kujenga chuki miongoni mwa waamini wa dini
tofauti. Kwa bahati mbaya, ushauri huo wa Baraza la Maaskofu ulipuuzwa
na mamlaka husika.
Hivi
karibuni, kumekuwa na ongezeko kubwa la vyombo vya habari ambavyo
vimeanzishwa na ambavyo badala ya kuzingatia malengo mazuri ya vyombo
vya habari ya kuhabarisha, kuelimisha na kuburudisha, vimeonyesha
malengo ya wazi ya kueneza uzushi, kashfa, chuki na uchochezi. Bado
kuna CD/DVD na Kanda chungu nzima zilizozagaa mitaani zenye malengo
kama hayo ambapo, kwa mshangao mkubwa wa raia wema wa nchi hii, licha ya
wahusika kufahamika na kuonekana wazi wazi, hakuna hatua za kisheria
zinazochukuliwa dhidi yao. Tunachelea hata kudhani kwamba mamlaka za
dola zinawakingia kifua wadau wa harakati hizo.
Mkusanyiko wa mambo yote haya ndio uliotufikisha hapa tulipo. Kwa
upendo tulio nao kwa nchi yetu na kwa kuzingatia historia ya mlolongo
wa matukio yaliyotufikisha hapa tulipo, tunahofu, lakini kwa uwazi
tunapenda kuziambia mamlaka husika, watu wote wenye mapenzi mema na
Watanzania wote kwa ujumla kwamba, iwapo hatua madhubuti hazitachukuliwa
mara moja ili kurekebisha hali hii, baada ya miaka michache, hakika kwamba nchi yetu inaweza kuingia katika machafuko makubwa ya kidini. Ili kuepuka hali hiyo isitokee, kwa moyo wa unyenyekevu kabisa, tunapendekeza hatua zifuatazo zichukuliwe:-
· Sisi Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania tutaendelea kusali ili kuiombea nchi yetu amani. Licha
ya sala na maombi ya kawaida kwa ajili ya lengo hilo, Mkutano Mkuu
umeamua kwamba, tutakuwa na siku moja ya kusali kitaifa kwa ajili ya
kuomba amani;
· Tutaendelea
kutumia sauti yetu ya kinabii kuonya, kukemea na kukaripia vitendo
vyote vile vinavyoashiria kueneza chuki miongoni mwa watu wa dini mbali
mbali;
· Kwa
kutumia Tume na Idara zetu, tutaendelea kujenga na kueneza mazungumzano
na Waamini wa dini mbali mbali tukiheshimu tofauti zilizopo. Hii ni kwa
sababu tunaamini kwamba, suala la dini ni wito na hiari ya mtu na
hakuna mtu yeyote aliye na haki ya kumlazimisha mwingine ajiunge na dini
yake.
Kwa upande wa wadau wengine na hasa kwa Serikali yetu pamoja na vyombo vyake vya usalama tunapendekeza yafuatayo:-
· Mihadhara, makongamano na mikutano yenye lengo la kutoa kashfa na kuchochea chuki miongoni mwa dini mbalimbali ipigwe marufuku;
· Vyombo
vya habari vinavyoeneza uzushi, kashfa na uchochezi vidhibitiwe kwa
kuchukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kufungiwa;
· Uzushi
na uongo unaoenezwa na vyombo vya habari na watu wenye lengo la
kuwachonganisha Watanzania na waamini wa dini mbali mbali utolewe
ufafanuzi mara moja na Wizara na vyombo vingine vinavyohusika;
· Kuweko
na mpango kabambe wa kutoa elimu ya uraia yenye kina na upana katika
nafasi zote, itakayowawezesha vijana wetu kuwa wazalendo kwa nchi yao na
kuepuka propaganda za kuwagawa Watanzania kwa misingi ya kidini;
· Suala
la ukosefu wa ajira, hasa miongoni mwa vijana, liangaliwe kwa makini
kwani linaweza kuwa moja ya sababu zinazowafanya vijana wengi kujiingiza
katika vikundi vya kidini vinavyojenga chuki na kutoa matumaini ya
uongo;
· Lakini,
zaidi ya yote, iwapo Serikali yetu na mamlaka husika inataka kuwa na
imani mbele ya jamii kwamba ina nia thabiti ya kuhakikisha kwamba vurugu
za kidini hazipati nafasi katika Nchi yetu, wale wote wanaohusika na
vurugu hizo wachukuliwe hatua za kisheria mara moja! Ni vigumu kuamini
kwamba katika kipindi cha kuanzia mwaka 2001 mpaka sasa, Makanisa 25
yamekwisha chomwa moto Visiwani Zanzibar lakini hakuna aliyekamatwa na kuchuliwa hatua za kisheria!
Tumefanya
mkutano wetu katika mazingira ya kuwepo mvutano kati ya madaktari na
serikali na kwa bahati mbaya sana, kama tulivyokwisha kutamka huko
nyuma, mvutano huu unaleta athari kubwa kwa raia wasio na hatia, athari
ambayo haiwezi kurudishwa. Uhai wa raia wa Tanzania unaangamia kwa
kukosa ulinzi wa tiba. Katika hili tunapenda kukumbusha kuwa kila mmoja ni mdau. Hakuna hata mmoja anayeweza kulikwepa hili. Tunapenda
kurudia himizo letu la awali kwamba ni bora ikapatikana njia nyingine
iliyo mwafaka zaidi ya kudai haki na mazingira yanayofaa ya kazi bila
kuleta madhara ya kupoteza uhai ambao ni haki msingi ya kila mwanadamu.
Tunaiasa Serikali yetu ikae tena pamoja na madaktari na kuchambua hoja zitakazowekwa mbele yao. Uwazi na ukweli vikitawala hakuna pande itakayokataa kuridhia eti kwa sababu ya kukataa tu bila hoja. Taifa letu limejipatia aibu mbele ya macho ya ulimwengu ya jinsi tunavyoshindwa kuishi kile tunachosema kwenye majukwaa.
Mwisho,
tunaendelea kuwaalika Watanzania wenzetu, hasa viongozi wa dini
mbalimbali kuwahamasisha waamini wao wawe raia wema wa nchi hii kwa
kuungana pamoja kuhamasisha upendo, haki, amani na maridhiano miongoni
mwa Watanzania wote. Licha ya tofauti zetu, tuzingatie hasa yale
yanayotuunganisha: ubinadamu wetu na uraia wetu wa nchi yetu Tukufu ya
Tanzania ambamo tutake tusitake, ni lazima wote tuishi! Tuepe ushindani
ambao hauna tija isipokuwa kutupeleka katika kujenga chuki na hali ya
kudhaniana vibaya miongoni mwa Waamini wetu. Iwapo kuna
sababu ya kushindana, tushindane katika kubuni mbinu za kujenga Upendo
na Amani miongoni mwa Watanzania katika kutafuta njia za kuwaletea
maendeleo yatakayowatoa kutoka katika Umaskini, Ujinga na Maradhi ambao
ndio adui wetu sote.
Tunaiombea Nchi yetu Amani na Usalama.
+Jude Thaddaeus Ruwai’chi
RAIS: BARAZA LA MAASKOFU KATOLIKI TANZANIA/
ASKOFU MKUU JIMBO LA MWANZA
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)