WAZIRI WA HABARI AWATAKA WAFANYAKAZI WIZARA HIYO KUTEKELEZA VIPAUMBELE VYA WIZARA - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

WAZIRI WA HABARI AWATAKA WAFANYAKAZI WIZARA HIYO KUTEKELEZA VIPAUMBELE VYA WIZARA

Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dkt. Fenella Mukangara akiongea na wajumbe wa Baraza la wafanyakazi wa Wizara hiyo leo jijini Dar es salaam ambapo amewataka watekeleze vipaumbele muhimu vya wizara hiyo kufanikisha azma ya Serikali ya kuleta mabadiliko katika sekta ya habari, Vijana, Utamaduni na Michezo.
Baadhi ya wajumbe wa Baraza la wafanyakazi wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Habari leo jijini Dar es salaam.
Waziri wa Habari, Vijana Utamaduni na Michezo Dkt. Fenella Mukangara(mwenye koti jeupe) akisalimiana na wafanyakazi wa Wizara ya habari mara baada ya kufungua kikao cha Baraza la wafanyakazi leo jijini Dar es salaam. Picha na Aron Msigwa  - MAELEZO.

(NA VERONICA KAZIMOTO – MAELEZO)
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Mhe. Dkt. Fenella Mukangara amewataka wafanyakazi wa wizara hiyo kutekeleza vipaumbele muhimu vya wizara ili kufanikisha azma ya Serikali ya kuwajengea maisha bora wananchi wake. 
 
Akifungua mkutano wa baraza la wafanyakazi wa wizara hiyo leo jijini Dar es Salaam amesema kuwa ili kufanikisha malengo na vipaumbele vilivyowekwa wizara yake inawategemea wafanyakazi hao ambao ni nguvu kazi muhimu katika kuleta mabadiliko ya utendaji kazi.
 
Amesema kuwa wizara pamoja na mambo mengine inatekeleza masuala mbalimbali yakiwemo uandaji wa mpango wa miaka 5 wa maendeleo ya michezo nchini, kuunda baraza la taifa la vijana, kupatia ufumbuzi tatizo la maslahi ya wasanii na kukamilisha mchakato wa kupata vazi la taifa.
 
“Ili kufanikisha utekelezaji wa vipaumbele hivi kila mmoja wetu anawajibika kufanya kazi kwa bidii mahali pake pa kazi bila kutegea wala kusukumwa.” Amesema Mukangara.
 
Amesisitiza kuwa sekta ya michezo ikiimarishwa nchini vijana wengi watapata fursa ya kuendeleza vipaji vyao na hatimaye kupunguza tatizo la ajira  jambo ambalo likifanyika katika tasnia ya sanaa vijana wengi wataweza kujiajiri na kujiongezea kipato.
 
Naye kaimu mwenyekiti wa Baraza hilo ambaye pia ni naibu katibu mkuu wa wizara ya Habari, Vijana , Utamaduni na Michezo Bi. Sihaba Nkinga akizungumza kwa kwa niaba ya wajumbe wa baraza hilo amesema Baraza  litatekeleza maagizo yaliyotolewa kwa vitendo ili kuleta maendeleo ya wizara na jamii kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages