NAIBU WAZIRI WA HABARI, VIJANA, UTAMADUNI NA MICHEZO AFANYA ZIARA TBC - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

NAIBU WAZIRI WA HABARI, VIJANA, UTAMADUNI NA MICHEZO AFANYA ZIARA TBC

Mtayarishaji  Mwandamizi  wa Vipindi vya Televisheni wa Shirika la   Utangazaji Tanzania (TBC), Jeff  Shellembi (kulia) akimwonesha Naibu Waziri wa Habari,Vijana, Utamaduni na Michezo, Amos Makalla (kushoto)  kaseti za kurekodi habari na vipindi mbalimbali yenye rangi nyekundu  na bluu  iliyo chini ya kiwango ambayo hudumu kwa miezi mitatu na kuathiri utendaji kazi wakati wa ziara ya Naibu  Waziri  huyo iliyofanyika leo kwenye  kituo hicho cha televisheni cha TBC, Mikocheni jijini Dares Salaam . Wa pili (kushoto) ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Joe Rugarabamu na  aliyevaa kitenge ni Mkurugenzi wa Habari na Matukio wa TBC, Suzan Mungy.
 Naibu Waziri wa Habari,Vijana, Utamaduni na Michezo Amos Makalla (katikati) akiagana na Mwenyekiti wa Bodi ya  Shirika la Utangazaji Tanzania ( TBC), Wilfred Nyachia  baada ya kumaliza ziara yake katika shirika hilo na kushoto ni Kaimu Mkurugenzi  Mkuu wa TBC, Joe  Rugarabamu.
 Fundi Mitambo wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Ally Kagomba (kushoto) akimwonesha Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Amos Makalla, mitambo ya kurushia vipindi mbalimbali  wakati Naibu Waziri huyo alipofanya ziara kwenye kituo cha televisheni cha TBC,leo Mikocheni jijini Dares Salaam.
Waziri Naibu Waziri wa Habari,Vijana, Utamaduni na Michezo Amos Makalla (katikati) akizungumza na  wajumbe wa Bodi  na uongozi wa   Shirika la Utangazaji Tanzania( TBC), mara baada kumaliza ziara yake katika shirika hilo. PICHA ZOTE NA MAGRETH KINABO – MAELEZO.
********************

Na Concilia Niyibitanga na Magreth Kinabo – HABARI

NAIBU Waziri wa Habari, Vijana Utamaduni na Michezo, Amos Makalla ameitaka Menejimenti ya Shirika la Utangazaji la Tanzania (TBC) na Bodi yake kushirikiana kwa karibu katika kukabiliana na changamoto mbalimbali ikiwa  ni pamoja na ukosefu wa vitendeakazi.

Mhe. Makalla ameyasema hayo leo (jana) wakati akizungumza na Menejimenti ya TBC na Bodi yake katika ofisi za kituo Televisheni ya Taifa (TBC1) cha  Mikocheni jijini Dar es Salaam.

Waziri  Makalla ameiagiza Menejimenti ya Shirika hilo kutengeneza  Mpango Mkakati wa kukabiliana na changamoto pamoja na matatizo ya Shirika hilo kwa kuzingatia vipaumbele na kuishauri  Bodi ya shirika kuutumia mpango huo.

‘Tengenezeni Mpango Mkakati wa namna ya kutatua matatizo  yanayolikabili Shirika,  ili mtoe ushauri kwa Bodi’. Amesema Makalla.

Aidha, Makalla amekiri kuwa amejionea matatizo na kuzisikia changamoto zilizopo TBC na ameahidi kuwa Serikali iko bega kwa bega na Shirika hilo ili kuhahikisha  kuwa matatizo hayo na changamoto hizo zinapatiwa Ufumbuzi.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi   wa TBC, Bw. Joe Rugarabamu  amesema, TBC inajitahidi kutekeleza majukumu yake ya kuhabarisha, kuelimisha na kuburudisha jamii ya Watanzania pamoja na changamoto ya uwezo mdogo wa kifedha, gharama kubwa za kukusanya habari, kuzihariri na kuzisambaza kwa Watanzania wote.

Amesema kuwa, Shirika linakabiliwa na tatizo la  uchakavu wa mitambo, gharama kubwa za upanuzi wa usikivu nchi nzima, uendeshaji wa mitambo hasa ukizingatia kupanda kwa gahrama za umeme na mafuta  na malipo ya wafanyakazi zaidi ya 600.

Bw. Rugarabamu  ameongeza kuwa, Shirika halina jengo moja la kuweka Ofisi za Radio na Televisheni pamoja hali inayofanya  kuwa na sehemu ya Radio, huko Barabara ya Nyerere  na Sehemu ya Televisheni, Mikocheni hivyo kusababisha  gharama za uendeshaji kuwa kubwa.

Naye Mtayarishaji  Vipindi  Mwandamizi wa  TBC, Bw.  Jeff Shellembi amesema, TBC1 inakabiliwa na uhaba wa kaseti za kisasa  kwa ajili ya habari za vipindi vya televisheni , hivyo kujikuta wakitumia kaseti zilizo chini ya kiwango hali inayosababisha kaseti hizo kuharibu deki na kuuwa kamera.

Bw. Ali Kagomba ni Fundi Mitambo  wa TBC naye ameeleza kuwa, mitambo  mingi ya Shirika hilo ya kurushia matangazo  ni chakavu na mingine ni mibovu kabisa ikizingatia kuwa imeshapitisha muda wake wa kutumika.

“Kwa Kitaalam na kiufundi mitambo inatakiwa kutumika kwa miaka  si zaidi ya 8, lakini mitambo yetu ina miaka  zaidi ya kumi na huathiri ubora wa matangazo.”  Amesema Bw. Kagomba.   

Hii ni mara ya kwanza kwa Naibu Waziri, Mhe. Makalla kufanya ziara ya kikazi katika Shirika la TBC mara baada ya kuteuliwa kuwa Naibu wa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages