Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal,
akizungumza na Seneta Christopher Coons (wa pili kushoto kwa Makamu)
aliyeongozana na ujumbe wake kutoka nchini Marekani, wakati walipofika
Ofisini kwake Ikulu jijini Dar es Salaam leo, kwa mazungumzo.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal,
akiwa katika picha ya pamoja na Seneta Christopher Coons (wa pili
kushoto) na ujumbe wake kutoka nchini Marekani, baada ya mazungumzo yao
yaliyofanyika Ofisini kwa Makamu Ikulu Dar es Salaam leo.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib
Bilal, akiagana na Seneta Christopher Coons, baada ya mazungumzo yao
yaliyofanyika Ofisini kwa Makamu Ikulu Dar es Salaam leo.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed
Gharib Bilal,akizungumza jambo na Seneta Christopher Coons, baada ya
kumaliza mazungumzo yao yaliyofanyika Ofisini kwa Makamu Ikulu Dar es
Salaam leo.
**********************************
DKT. BILAL AFANYA MAZUNGUMZO NA UJUMBE WA MAREKANI
Makamu
wa Rais Dkt. Mohammed Gharib Bilal leo Ijumaa Juni Mosi, 2012 amekutana
na kufanya mazungumzo na ujumbe wa watu saba kutoka Marekani ukiongozwa
na Seneta kutoka Delaware Christopher Coons.
Katika
mazungumzo hayo, Makamu wa Rais alielezea kufurahishwa kwake na
uhusiano mzuri ulipo kati ya Tanzania na Marekani na pia akafafanua kuwa
Marekani imekuwa ni rafiki wa kweli kwa Tanzania kutokana na michango
yake ya maendeleo iliyopo nchini.
Dk.
Bilal aliueleza ujumbe huo uliomtembelea Ikulu leo kuwa, serikali ya
Tanzania inaona faraja kushirikiana na Marekani na kueleza kuwa mchango
wa Marekani kwa Tanzania ni mkubwa na Tanzania inakaribisha uhusiano
zaidi hasa katika sekta za Kilimo na Nishati.
“Waziri
wa Mambo ya Nje wa Marekani Bibi Hillary Clinton alikuja hapa, akatupa
matumaini ya kuondokana na tatizo la umeme. Tayari wapo wawekezaji wengi
kutoka Marekani ambao wana nia ya kuwekeza katika nishati,” alisema
Makamu wa Rais.
Kwa
upande wake Seneta Coons alimueleza Makamu wa Rais kuwa, jimboni kwake
Delaware wapo wakulima wengi ambao wangependa kuja nchini kuwekeza
katika kilimo. Pia alifafanua namna Tanzania inavyoweza kuzalisha umeme
wa ‘Geothermal’ kwa kushirikiana na wawekezaji kutoka Marekani.
Seneta
Coons amewahi kuishi Afrika Mashariki katika miaka 25 iliyopita
sambamba na mambo mengine ni seneta mwenye uwezo wa kuzungumza
Kiswahili.
Seneta
huyu anatokea katika eneo la uwakilishi ambalo pia anatokea Makamu wa
Rais wa Marekani Joe Biden na amepata nafasi ya Useneta baada ya Biden
kuachia kiti hicho.
Hata
hivyo, Makamu wa Rais alisema pamoja na juhudi zote za kuhifadhi
mazingira na viumbe hai bado Tanzania inakabiliwa na matatizo ya
ujangiri, uvuvi haramu, magugu maji kufunika kabisa baadhi ya maziwa na
mito.
Alipotakiwa
kutoa maoni yake kuhusu vurugu za hivi karibuni za Zanzibar Dkt. Bilal
alisema haoni sababu yoyote ile kwa watu wanaohubiri kuwa hawataki
Muungano kisha wakakimbilia kuchoma makanisa na kuvunja baa.
Alisema kuwa, kikundi hiki kimekuwepo siku nyingi na kinatumia kivuli cha dini katika kufanya siasa.
Vile
vile Makamu wa Rais alieleza kuwa, Zanzibar ni kisiwa kidogo na kupitia
Muungano wananchi wa Zanzibar wananufaika na kamwe serikali ya awamu ya
nne haiwezi kuvumilia kuona watu wachache wenye agenda iliyojificha
wakiharibu jambo bora kabisa lililofanyiwa kazi kwa zaidi ya miaka 48.
“Kila
ukipita mikoani unakutana na Wazanzibar wanaishi. Kupitia Muungano
tumefungua fursa nyingi. Sioni sababu ya watu kuibuka sasa kuupinga
Muungano na tena kwa kufanya fujo. Tutaendelea kudhibiti hali hii na
kuhakikisha kuwa amani inabakia katika nchi yetu,” alisema.
Dar es salaam
Ijumaa - Juni 1, 2012
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)