Kaimu Mkurugenzi na Mwenyekiti Mtendaji wa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) Paul Chizi akiongea na waandishi wa habari mara bada ya kuwasili kwa ndege mpya aina ya Boeing 737-500 iliyokodishwa na shirika hilo yenye uwezo wa kubeba abiria 108.Picha na Mpiga picha wetu
Wafanyakazi wa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) wakishuka katika ndege mpya aina ya Boeing 737-500 iliyokodishwa na shirika hilo yenye uwezo wa kubeba abiria 108. Ndege hiyo itaanza kuruka baada ya wiki moja. Picha na Mpiga picha wetu
Mmoja
wa wafanyakazi wa ATCL akiwaamebeba ujumbe wa kumkaribisha Waziri
Harisson Mwakyembe baada ya uteuzi uliofanywa na Rais Jakaya Kikwete
hivi karibuni.
Wahudumu wa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) wakipozi mbele ya kamera ya blogu hii.
Wafanyakazi wa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) wakikata keki kusherekea ujio wa ndege ndege mpya aina ya Boeing 737-500. Wapili kushoto ni Kaimu Mkurugenzi na Mwenyekiti Mtendaji wa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) Paul Chizi
Na Mwandishi Wetu.
NDEGE mpya aina ya Boeing 737-500 iliyokodishwa na Shirika
la ndege la AIR Tanzania (ATCL) imewasili nchini wikiendi hii na
itaanza safari za Dar-Mwanza-Kilimanjaro kabla ya kuanza safari za
kimataifa, Kaimu Mkurugenzi na Mwenyekiti Mtendaji wa ATCL Paul Chizi
amesema.
Akizungumza
mara baada ya kuwasili kwa ndege hiyo yenye uwezo wa kubeba abiria 108
iliyokodishwa toka kwa kampuni ya Aero Vista Dubai, Chizi alisema kuwa
ATCL itaanza safari zake katika kipindi cha wiki moja kuanzia sasa na
kuonyesha uwezekano wa kuiunganisha Dar es Salaam na Dubai katika safari
zake katika kipindi cha miezi mitatu ijayo.
“Watanzania
watarajie huduma bora waliyoikosa kwa kipindi kirefu sasa. Tutarudisha
safari zetu katika kipindi cha wiki moja. Tunaitaji watuunge mkono kama
ilivyokawaida yao katika siku za nyuma.
“Huduma
zetu ni za uhakika na ni kwa ajili ya wateja wetu. Muda ni kigezo chetu
kikubwa katika kazi na sasa tunatarajia kutoa huduma kwa wakati lakini
pia huduma zenye unafuu kwa wateja,” alisema.
Chizi
alisema kuwa kampuni inatarajia kuungana kibiashara na makampuni ya
kimataifa ya ndege katika lengo la kutanua safari zake lakini
alisisitiza kuwa hali hiyo itakuwa na faida na matunda pande zote mbili.
“Kupitia muungano huo wa kibiashara, tutahakikisha kuwa kila mmoja anafaidika. Ambapo katika muungano huo kampuni inapokosa faida, daima muungano huo wa kibiashara hauwezi kudumu,” alisisitiza.
Aliongeza kuwa ndege nyingine ya kampuni hiyo aina ya Dash 8 ambayo inafanyiwa matengenezo Terminal 1 nayo itakuwa tayari katika kipindi cha wiki sita zizajo na itasaidia kuboresha utoaji huduma zaidi wa kampuni hiyo.
Ndege
mpya ya ATCL Boeing 737-500 imeshafanyiwa uchunguzi na timu ya wataalam
kutoka katika Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) jijini Cairo
nchini Misri na tayari hati ya kibali cha ufanyaji kazi wa ndege hiyo
nchini kimeshatolewa.
Ndege
hiyo iliyonakshiwa na rangi za shirika la ndege la ATCL inachukua
abiria wapatao 12 katika daraja la kwanza (business class) pamoja na
abiria 96 katika daraja la kawaida (economy class)
ATCL
hivi karibuni ilizindua tovuti katika lengo la kuboresha utoaji wa
huduma kwa wateja pamoja na kukuza ubora katika utendaji kazi wa shirika
hilo la ndege la kitaifa.
Tovuti
hiyo inawawezesha wateja kupata huduma za ukataji tiketi bila ya kufika
katika ofisi za ATCL au kupitia mawakala na kuwasaidia wateja kutoa
maoni yao kupitia mitandao ya kijamii.










No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)