Mkurugenzi Mtendaji
wa Mkuki na Nyota Publishers, Walter Bgoya.
KAMPUNI ya Uchapishaji wa Vitabu na machapisho anuai kwa
mara ya kwanza imezindua kitabu cha somo la Kemia kilichochapishwa kwa lugha
nyepesi ya kiswahili. Kitabu hicho kilichopewa jina la Furahiya Kemia (Enjoy
Chemistry) kilichochapishwa kwa ushirikiano na Taasisi ya HakiElimu
kimezinduliwa Mei 9, 2012 na Mkurugenzi Mtendaji wa HakiElimu, Bi. Elizabeth Missokia.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Bi. Missokia alisema
kuzinduliwa kwa kitabu hicho kutaleta chachu ya wanafunzi kupenda masomo ya
sayansi hasa Kemia ambayo yamekuwa yakiwatatiza wanafunzi wengi kutokana na
lugha ya kigeni inayotumiwa.
Alisema ndani ya kitabu hicho wanafunzi wataweza kusoma na
kuelewa vizuri somo la Kemia kwa lugha nyepesi ya Kiswahili jambo ambalo
linaibua morali ya wanafunzi kuona masomo ya sayansi ni ya kawaida kujifunza kama yalivyo masomo mengine.
Awali akizungumza kabla ya uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji
wa Mkuki na Nyota Publishers, Walter Bgoya alisema kitabu hicho kimechapishwa
kwa lugha mbili yaani Kiswahili na Kiingereza ili kuwarahisishia wanafunzi
kujifunza sayansi ya Kemia kwa lugha mama ya Kiswahili.
Aidha alisema kitabu hicho kimepitiwa na kukubaliwa na
Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA) kwamba kinaweza kutumika kutokana na kuwa
na maneno rahisi na sahihi ya Kiswahili ambayo yatawarahisishia wakati wa
kujifunza mada anuai za Kemia hasa kidato cha kwanza.
Pamoja na hayo, Bgoya aliishukuru taasisi ya HakiElimu kwa
kusaidia kuchapishwa kwa kitabu hicho na kuwataka wadau wengine waungane na
juhudi hizo za kuinua lugha ya Kiswahili katika matumizi ya kufundishia hata masomo
ya sayansi.
Naye akitoa maoni yake juu ya kitabu cha Furahiya Kemia mmoja
wa walimu wa Sayansi, John Bosco alisema kitabu hicho kitakuwa daraja litakalo
wawezesha wanafunzi kuvuka na kuyapenda masomo ya sayansi hasa kemia. Alisema
kitabu hicho kina mazoezi ya kutosha kiasi cha kumfanya mwanafunzi apende
kujifunza kwa dhati.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)