Mwenyekiti wa baraza la michezo Taifa Bi Sherry Khamis akitoa ufafanuzi
mbele ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad
kuhusiana na mwendelezo wa ligi ya Central Taifa. Kushoto ni Waziri wa
Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Said Ali Mbarouk
Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akisalimiana na
baadhi ya wajumbe wa kamati ya ligi ya vijana “Central Taifa”
waliofika ofisini kwake Migombani kwa ajili ya kubadilishana nae
mawazo. Katikati ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Said
Ali Mbarouk na pembeni (kulia) ni mwenyekiti wa Baraza la Michezo
Zanzibar Bi Sherry Khamis.Picha na Salmin Said,Ofisi ya Makamu wa Kwanza
wa Rais wa Zanzibar
--
--
Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Zanzibar imesema
itafanya kila liwezekanalo ili kuiwezesha ligi ya vijana Zanzibar iweze
kusonga mbele.
Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Said Ali Mbarouk alitoa ahadi hiyo mbele ya
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, wakati
kamati ya ligi hiyo Central Taifa ilipokutana na Maalim Seif ofisini
kwake Migombani.
Aliahidi kuwa Wizara ya habari itatafuta fedha kwa njia yoyote ili
kuhakikisha kuwa fainali za ligi hiyo inayotarajiwa kufikia kilele chake
July mwaka huu kwa timu za Juvinail, Junior na Central zinafanikiwa.
Alisema ligi hiyo ni muhimu katika kuibua vipaji vya vijana ambavyo
vitasaidia kuinua soka la Zanzibar. Kwa upande wake Makamu wa Kwanza wa
Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amewataka viongozi wa ligi
hiyo kuwa na dhamira ya kweli katika kuendeleza ligi hiyo, sambamba na
kuepukana na vitendo vyovyote vya udanganyifu katika kuibua vipaji vya
wanasoka vijana. “Sisi serikali tuko very serious na mimi binafsi niko
interested kuona hadhi ya michezo inarejea Zanzibar, kwa hiyo na nyinyi
viongozi muwe serious kwa hili”, alisistiza Maalim Seif.
Amewatahadharisha viongozi hao kuzitumia fedha wanazopewa kwa kutimiza
malengo yaliyokusudiwa na sio kuzitumia kwa maslahi binafsi. “ Wakati
mwengine tunakosa ufadhili kwa kuwa hatuko serious, hao wafadhili nao
wanaangalia ni kwa kiasi gani fedha zao zinatumika kwa malengo
yanayokusudiwa, vyenginevyo ndio wanaona hakuna haja ya kutoa ufadhili”
aliongeza.
Nao viongozi wa chama cha soka Zanzibar ZFA wakiwemo kaimu Rais wa ZFA
Haji Ameir na mwenyekiti wa Baraza la Michezo Zanzibar Bi Sherry
Khamis, wamesifu utendaji wa Waziri mpya wa Wizara hiyo Mhe. Said Ali
Mbarouk, na kwamba unawapa changamoto katika utendaji wao.
Wamesema Waziri huyo amedhamiria kweli kufanya kazi aliyotumwa na kamwe
hakuna mzaha wala muhali, kama ambavyo mwenyewe amekuwa akieleza mara
kwa mara. Ligi ya vijana kwa ngazi za Juvenile, Junior na Central
inazishirikisha timu za mitaani za vijana zilizopata usajili ambazo
hushindana hadi ngazi ya Wilaya Unguja na Pemba ambapo hupatikana
mshindi mmoja kwa kila Wilaya, na kuanzia hapo ndio kamati ya Central
Taifa hushughulikia kwa ajili ya kuandaa fainali ambazo hufanyika
Unguja na Pemba.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)