Dotto Kahindi na Boniface Meena
TUME
ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), imekana kukitambua Chuo Kikuu cha Japan
Bible Institute Graduate School of Theology kilichotoa Shahada ya
heshima kwa mfanyabiashara maarufu nchini, kutokana na kutotambulika
kisheria nchini.
Kwa
mujibu wa taarifa ya TCU kwa umma iliyotolewa jana kwenye gazeti la
moja la kila siku (siyo Mwananchi), chuo hicho kimekuwa kikitangaza
kutoa kozi mbalimbali za uzamivu (PhD) kwenye nyanja za dini na jamii.
Taarifa
ya TCU imekuja siku chache baada ya chuo hicho kuwatunuku Shahada ya
heshima ya udaktari watu mbalimbali akiwamo, Mwenyekiti Mtendaji wa
Makampuni ya IPP.
Katika
wasifu uliotolewa na chuo hicho kwa mwenyekiti huyo, ni kwamba hatua
hiyo imefikiwa baada ya juhudi zake za kusaidia makundi mbalimbali ya
watu wakiwamo walemavu, wajane na watu walioathirika na Ukimwi. Pia,
kutambua mchango wake katika kutumikia kanisa.
Kwa
mujibu wa taarifa ya TCU, chuo hicho kinatangaza kuwakilisha tawi la
taasisi iliyopo nchini Marekani na kwamba, makao yake makuu kwa bara la
Afrika yapo Dar es Salaam, huku eneo la ofisi likiwa halijulikani
kilipo.
“Tume
inachukua fursa hii kuuarifu umma kwamba chuo hiki hakitambuliki kwa
mujibu wa sheria na kwamba wamiliki wa Japan Bible Institute Graduate
School of Theology hawana kibali cha kutoa elimu ya chuo kikuu ambayo
inatambuliwa hapa nchini,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Tume hiyo ilitoa tahadhari kwa umma kuepuka ulaghai ambao unafanywa na watu eneo la elimu ya juu kwa kuwa vyeti vitakavyotolewa na chuo hicho havitatambulika na tume na haviwezi kutumika nchini.
Tume
ilitoa onyo kali kwa wamiliki wa chuo hicho , ikiwataka kuacha mara
moja kutoa matangazo ya shahada za aina hiyo nchini, bila kufuata
taratibu na kwamba hatua za kisheria zitachukuliwa kwa atakayekwenda
kinyume cha sheria.
Hata hivyo, wakati wa sherehe za kutunukiwa kwa mwenyekiti huyo zilizofanyika viwanja vya Mnazi Mmoja mwishoni mwa wiki iliyopita, Mkurugenzi wa Taasisi hiyo Kanda ya Afrika, Askofu Dk Paul Shemshanga, alisema chuo chake kinatambuliwa na taasisi mbalimbali ulimwenguni na kuishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuwapa ruhusu ya kutoa elimu hiyo nchini.
Msemaji wa Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Abdulhamid Njovu, alipoulizwa kuhusu suala hilo alisema anachokifahamu ni kuwa hakiingii kwenye mfumo wa TCU, kwa sababu kinahusiana na dini chenye misingi ya kikristo.
Njovu alisema TCU walitoa barua yenye kumbukumbu namba TCU/A60/25/ ya Machi 9, mwaka huu kuruhusu kufanyika kwa sherehe hizo za utoaji shahada za uzamivu (PhD).
”Huwa wanatoa shahada za heshima kwa watu wenye matendo ya kichungaji kwa kuwa, chuo chao ni cha masuala ya dini na wote waliokuwapo pale ni viongozi wa dini isipokuwa wale watunukiwa,” alisema Njovu na kuongeza: “Masuala hayo yote ni ya viongozi wa kidini.”
Source: www.mwananchi.co.tz






No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)