Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad:Serikali Haitovumila Vitendo vya Uvunjaji Amani - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad:Serikali Haitovumila Vitendo vya Uvunjaji Amani

Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar na Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF Maalim Seif Sharif Hamad akiwahutubia wananchi wa Jimbo la Wete baada ya kukabidhi vifaa mbali mbali kwa jimbo hilo huko viwanja vya Jadida Wete.Picha na  Salmin Said-Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar
 ---
Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar na Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF Maalim Seif Sharif Hamad amesema serikali haitovulimia vitendo vyovyote vinavyoashiria uvunjifu wa amani vyenye lengo la kuvuruga umoja wa Zanzibar.
Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar amesema Zanzibar haitorudi tena nyuma, licha ya kuwepo baadhi ya watu wasiopenda maendeleo ya Zanzibar, na kwamba wanaotumiliwa kwa ajili ya kuendesha vitendo hivyo watapambana na mkono wa sheria.
Alitoa onyo hilo huko Jadida kisiwani Pemba, alipokuwa akizungumza na wananchi wa jimbo la Wete, mara baada ya kukabidhi vifaa kadhaa vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni ishirini na tisa (mil.29) vilivyotolewa na mbunge na mwakilishi wa jimbo hilo.

Hali hiyo imekuja kufuatia kujitokeza viashiria vya kuwepo kundi la watu wanaotumiliwa kwa lengo la kuvuruga umoja wa Zanzibar, baada ya kundi hilo kupachua bendera ya chama kimoja cha siasa katika eneo la Wawi hivi karibuni.

“Nchi yetu imetulia na hatutovumilia vitendo vyovyote vya uvunjifu wa amani, tena nasema hatutorudi nyuma”, alisisitiza Maalim Seif.

Akizungumzia kuhusu vifaa vilivyotolewa vikiwemo gari moja ya jimbo hilo, pasola moja na baiskeli 23 kwa ajili ya maendeleo ya chama na printers 5 kwa ajili ya skuli, Maalim Seif amewataka wananchi kuvitunza na kuvitumia kwa malengo yaliyokusudiwa. Pia alikabidhi vifaa mbali mbali vya michezo vikiwemo mipira 195 na jezi seti 11.
Amewapongeza viongozi wa jimbo hilo kwa kutekeleza kwa vitendo ahadi walizozitoa kwa wananchi, na kuwataka kuongeza mashirikiano kwa wananchi, ili mafanikio zaidi yaweze kupatikana.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Mhe. Dadi Faki Dadi alisema serikali bado haijapokea malalamiko hayo ya kupachuliwa bendera katika eneo la Wawi, lakini italifanyia kazi na kuwachukulia hatua watakaobainika kuhusika na vitendo hivyo.

Alipongeza maamuzi hekma na ya kijasiri yaliyofanywa na Rais mstaafu Dk. Amani Abeid Karume na Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad ya kufikia maridhiano ya kisiasa ambayo yamewawezesha wananchi wa Zanzibar kuishi kwa amani na utulivu na kurejesha mshikamano na umoja miongoni mwa wananchi.

Mbunge wa Jimbo la Wete Mhe. Mbarouk Salum Ali na mwakilishi Mhe. Assaa Othman Hamad wameahidi kuendeleza mashirikiano ya wananchi kwa lengo la kukabiliana na kero zinazowakabili wananchi wa jimbo hilo.

Na
 Hassan Hamad Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages