Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akiangalia kazi
za sanaa zinazofanywa na vijana wa nyumba ya sanaa mwanakwerekwe wakati
alipotembelea nyumba hiyo. Kulia (mwenye kofia) ni mkuu wa nyumba hiyo
Bw. Salum Muchi.
Wanafunzi
wa skuli za Mwanakwerekwe wakiwa na hamu ya kumsalimia Makamu wa Kwanza
wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad alipofika kwenye Kamisheni
ya Utamaduni na Michezo huko Mwanakwerekwe.
Kamishna
wa Utamaduni na Michezo Bw.Hamad Bakari Mshindo akijiandaa kukabidhi
kitabu kwa Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad. Kitabu
hichi kiliandikwa na kamishna huyo wa utamaduni.
Meneja
wa uwanja wa Amaan Bw. Khamis Ali Mzee akimuonesha Makamu wa Kwanza wa
Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, maeneo yaliyoharibiwa kwa
uchimbaji wa mchanga karibu na uzio wa uwanja huo.Picha na Salmin
Said-Ofisi Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar
--
Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad ameitaka
kamisheni ya utamaduni na michezo kuweka mikakati imara ili kulinda
utamaduni na maadili ya Zanzibar yasiathiriwa na utandawazi.
Amesema
utamaduni ni kielelezo mahsusi cha taifa ambacho kinapaswa kulindwa kwa
nguvu zote, na kwamba kamisheni hiyo ina jukumu kubwa la kuhakikisha
kuwa vitu hivyo vinalindwa.
Maalim
Seif ameeleza hayo katika kamisheni hiyo iliyoko Mwanakwerekwe wakati
alipofanya ziara ya kutembelea taasisi mbali mbali zilizo chini ya
Wizara ya habari, utamaduni, utalii na michezo.
Amefahamisha
kuwa wakati serikali ikijiandaa kutekeleza mpango wake wa kuwa na
utalii kwa wote, ni vyema kujiwekea mikakati ya kulinda utamaduni wa
Zanzibar ambao kwa kiasi kikubwa unachangia maendeleo ya sekta hiyo
nchini.
Katika
ziara hiyo Maalim Seif alitembelea maeneo mbali mbali yakiwemo uwanja
wa Amaan ambapo ameuagiza uongozi wa Wizara ya habari kuchukua hatua za
haraka kudhibiti uchafuazi wa mazingira katika eneo hilo unaotokana na
uchimbaji wa mchanga karibu na uzio wa uwanja Amaan.
Amesema
iwapo hatua za haraka hazitochukuliwa, eneo hilo litazidi kuharibiwa na
kupoteza hadhi yake, hasa ikizingatiwa kuwa tayari wamejitokeza
wafadhili watakaoiendeleza hoteli ya uwanjani Amaan kuwa ya kimataifa.
Katika
idara ya makumbusho na mambo ya kale, Maalim Seif ameitaka idara hiyo
kufanya utafiti wa kina ili kuieleza kwa usahihi historia ya Zanzibar
kwa wenyeji na wageni wanaotembelea makumbusho hiyo.
Amesema
wageni wengi wamekuwa na hamu ya kuifahamu historia ya Zanzibar lakini
watu wengine huipotosha kutokana na kutofanya utafiti wakati wanapotoa
historia hiyo.
Mkurugenzi
wa Idara hiyo bibi Amina Ameir Issa amesema idara hiyo imeweka mkazo wa
kuyaendeleza maeneo ya kihistoria yakiwemo majengo, ambapo hadi sasa
tayari majengo 85 Unguja na Pemba yameshatangazwa kuwa ya hifadhi.
Bi
Amina amesema wanakusudia kuifanya makumbusho ya viumbe hai iliyopo
Mnazi mmoja kuwa makumbusho ya mazingira ambayo itasaidia kuhifadhi
viumbe mbali mbali vikiwemo vya baharini.
Amesema
changamoto kubwa wanayokamiliana nayo kwa sasa ni mwamko mdogo wa
wananchi kutembelea maeneo ya kihistoria ambayo ni muhimu katika
kufahamu ukweli kuhusu historia na kujionea mambo mbali mbali ya
kihistoria yaliyotunzwa katika makumbusho hizo.
Maeneo
mengine aliyoyatembelea ni pamoja makumbusho ya kasri Mtoni pamoja na
pango la kisima cha chini kwa chini lililoko mangapwani ambalo
linasadikiwa kuwa lilifanyika kiasi cha miaka milioni moja na nusu
iliyopita.
Na
Hassan Hamad
Ofisi Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar





No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)